Saturday, April 29, 2017

GHARAMA YA UONGO

"Midomo ya uongo ni chukizo kwa Bwana; Bali watendao uaminifu ndio furaha yake" (Mithali 12:22)
 
Kutoka Shekemu, wana wa Israeli walirejea katika kambi lao huko Gilgali. Muda si mrefu walipokuwa hapa walitembelewa na wajumbe wa ajabu, waliotamani kufanya mkataba pamoja nao. Mabalozi hawa walieleza kuwa walitokea nchi ya mbali, na hili lilionekana kuthibitishwa na hali ya mwonekano wao. Mavazi yao yalikuwa makuukuu na yalikuwa yameraruka, viatu vyao vilikuwa vimetobokatoboka, chakula chao kilikuwa kimekauka na kuvunda, na vibuyu vyao vya mvinyo vilikuwa vikuukuu vilivyorarukararuka na kutiwa viraka, kana kwamba vilirekebishwa haraka njiani wakiwa safarini…. Mionekano hii ilifanikiwa kuwashawishi wenyeji…. “Naye Yoshua akafanya amani pamoja nao, na kufanya agano nao, ili kwamba waachwe hai; na wakuu wa mkutano wakawaapia.” Hivyo ndivyo mkataba huu ulivyofanyika….
 
Lakini mambo yangeliwaendea vyema Wagibeoni endapo wangezu-ngumza na Israeli kwa uaminifu. Wakati ambapo kujinyenyekesha kwao na kumfuata Yehova kuliwapatia ulinzi wa maisha yao, udanganyifu wao uliwaletea fedheha na utumwa. Mungu alikuwa ameandaa mpango kwamba wote ambao wangeukana upagani, na kujifungamanisha na Israeli, wangeshiriki baraka za agano lake. Walihusishwa kwa namna hiyo katika masharti yaliyosema, “mgeni akaaye kati yenu,” na isipokuwa mambo mengine machache, wageni hawa walipaswa kupata fadhila na fursa sawa na Israeli. Maelekezo ya Bwana yalikuwa—“Na mgeni akikaa pamoja nawe katika nchi yako, usimdhulumu. Mgeni akaaye pamoja nawe atakuwa kama mzalia kwenu; mpende kama nafsi yako; kwa maana ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri; Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu” (Law. 19:33, 34).
 
Hayo ndiyo masharti ambayo kwayo Wagibeoni wangeliweza kupokelewa, kama isingelikuwa ule udanganyifu ambao walikuwa wameutumia. Haikuwa fedheha ndogo kwa raia hao wa “miji ya kifalme,” “tena watu wake wote walikuwa ni mashujaa,” kuwa wapasua-kuni, na wateka-maji kwa ajili ya Israeli wakati wote. Lakini walikuwa wamejitwalia vazi la umaskini kwa ajili ya kusudi la udanganyifu, na lilifungamanishwa juu yao kama nembo ya utumwa wa kudumu. Kwa hiyo katika vizazi vyao vyote hali yao ya utumwa ingeliweza kushuhudia chuki ya Mungu dhidi ya udanganyifu.

No comments: