Friday, April 14, 2017

HAKUNA UDHURU WA KUTENDA DHAMBI

“Wakamghadhibisha penye maji ya Meriba, Hasara ikampata Musa kwa ajili yao, Kwa sababu waliiasi roho yake, Akasema yasiyofaa kwa midomo yake”
(Zaburi 106:32, 33).

Kama Musa na Haruni wangelikuwa wanaendekeza hali ya kujistahi au kuendekeza roho ya hasira licha ya onyo na karipio la Mungu, hatia yao ingelikuwa kubwa sana. Lakini hawakuwa na hatia ya dhambi ya kukusudia au kudhamiria; walikuwa wameangushwa na jaribu la ghafla, na majuto yao yalifanyika mara moja, tena toka moyoni. Bwana aliikubali toba yao, ingawa kwa sababu ya madhara ambayo dhambi yao ingeliweza kuyasababisha miongoni mwa watu, asingeliweza kufutilia mbali adhabu hiyo…..
Mungu alikuwa amewasamehe watu maasi makubwa zaidi, lakini asingeliweza kushughulikia dhambi ya viongozi hawa kama alivyofanya kwa wale waliokuwa wakiongozwa. Alikuwa amempatia Musa nafasi ya heshima kubwa kuliko mwanadamu yeyote duniani…. Ukweli kwamba Musa alikuwa amepata nuru na maarifa makubwa kiasi hicho uliifanya dhambi yake kuwa mbaya zaidi. Uaminifu wa wakati uliopita hautaweza kuwa udhuru wa kusamehe kosa hata moja. Kadiri nuru na fursa anazopewa mwanadamu zinapokuwa kubwa zaidi, ndivyo pia wajibu wake unavyokuwa mkubwa zaidi, kadiri kosa lake linavyokuwa baya zaidi, na pia ndivyo adhabu yake huwa kali zaidi..
Musa hakuwa na hatia ya kufanya uovu mkubwa, kama ambavyo watu wanaweza kuliangalia suala hili…. Lakini endapo Mungu alishughulikia dhambi hii vikali sana kiasi hicho kwa mtumishi wake huyu mwaminifu na aliyeheshimiwa kuliko wote, hatawezi kuipuuzia dhambi kwa wengine…. Wote wanaodai kuwa wacha Mungu wako chini ya wajibu mtakatifu sana wa kulinda roho zao, na kujitawala wanapokabiliwa na uchokozi mkubwa zaidi. Wajibu uliowekwa juu ya Musa ulikuwa mkuu sana; ni wanadamu wachache ndio watakaojaribiwa kama ilivyokuwa kwake; hata hivyo hili halikuruhusiwa kuwa udhuru wa kupuuzia dhambi yake. Mungu aliandaa mpango wa kutosha kwa ajili ya watu Wake; na kama wakitumainia nguvu zake, kamwe hawataweza kuwa wahanga wa mazingira. Jaribu zito sana kuliko yote haliwezi kuwa udhuru wa dhambi. Hata kama shinikizo lililoletwa ili kuikabili roho litakuwa kubwa kiasi gani, uasi ni tendo letu sisi wenyewe. Haipo katika nguvu ya dunia wala jehanamu kumshurutisha yeyote kutenda uovu. Shetani anatushambulia katika maeneo yale ambayo tu dhaifu, lakini hatupaswi kushindwa. Hata kama shambulizi ni kali au lisilotarajiwa kiasi gani, Mungu ametupatia msaada, na katika uwezo wake tunaweza kushinda.

No comments: