Saturday, August 19, 2017

HAKUNA MKAMILIFU

Hakuna familia isiyo na mapungufu, Hatuna wazazi wasio na mapungufu, sisi pia si wakamilifu, hatuoi au kuolewa na mtu asiye na mapungufu, kadhalika watoto wetu nao si wakamilifu.
Tunayo manung'uniko au malalamiko kila mmoja dhidi ya mwenzake. Tumevunjana moyo na kukatishana tamaa. Kwa hiyo, hakuna ndoa iliyokamilika wala familia iliyoboreka bila kuwa na mazoea au utamaduni wa kusameheana.
Msamaha ni nguzo au msingi wa utulivu wa akili na uhai wa roho zetu. Kama hakuna msamaha, familia inakuwa uwanja wa migogoro na mlipuko wa ugomvi. Panapokosekana msamaha, familia inaugua. Msamaha unahuisha moyo, kwa kusafisha fikra na kuufanya moyo kuwa huru. Binadamu asiyesamehe hana amani moyoni na wala hana urafiki au muunganiko na Mungu.
Maumivu ni sumu inayodhuru na kuua. Hebu kiponye kidonda hicho cha moyo endapo kuna dalili za kujiumiza. Mtu asiyesamehe anajisababishia mwenyewe ugonjwa wa mwili, kiakili na kiroho. Ndiyo maana familia inapaswa kuwa sehemu ya uhai na si kifo; eneo la uponyaji na sio mahali pa magonjwa; jukwaa la msamaha na si la uovu.
Msamaha huleta furaha pale uchungu ulipoleta maumivu, huleta uponyaji hata pale ambapo maumivu yalisababisha magonjwa.

YEREMIA, MSEMAJI WA MUNGU

Ni vema mtu autarajie wokovu wa Bwana Na kumngojea kwa utulivu. Maombolezo 3:26.

Kati ya wale waliotumaini kuwa na uamsho wa kudumu wa kiroho ikiwa matokeo ya matengenezo chini ya Yosia alikuwa Yeremia, aliyeitwa na Mungu ili aingie katika nafasi ya kuwa nabii akiwa bado kijana…
Ndani ya kijana Yeremia, Mungu aliona mtu ambaye angeaminika na ambaye angesimama katika haki dhidi ya upinzani mkubwa… Bwana akamwambia mjumbe wake aliyemchagua; “Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru.”….
Kwa miaka arobaini ilimpasa Yeremia kusimama mbele za taifa kama shahidi ya ukweli na uadilifu. Katika wakati wa uasi usio na kifani ilimpasa aoneshe ibada ya Mungu pekee wa kweli katika mfano wa maisha na tabia. Wakati wa utekwaji wa kutisha wa Yerusalemu ilimpasa awe msemaji wa Yehova.
Akiwa kwa asili na silika ya kuwa mwoga na mwenye kunywea, Yeremia alitamani amani na utulivu wa maisha ya kujitenga, ambapo asingelazimika kushuhudia maendeleo ya mioyo migumu ya taifa lake alilolipenda. Moyo wake ulikamuliwa kwa maumivu kutokana na uharibifu ulioletwa na dhambi….
Uzoefu aliopitia Yeremia siku za ujana wake na pia katika siku za mbeleni za huduma yake, ulimpa fundisho kwamba “njia ya mwanadamu haimo katika nafsi yake; kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu. Ee Bwana, unirudi kwa haki; si kwa hasira yako, usije ukaniangamiza” (Yeremia 10:23, 24).
Alipoitwa kukinywea kikombe cha mateso na huzuni na alipojaribiwa wakati wa shida yake kusema, “Nguvu zangu zimepotea, na tumaini langu kwa Bwana,” alikumbuka majaliwa ya Mungu kwa ajili yake na kwa kushangilia akasema, “Ni huruma za Bwana kwamba hatuangamii, kwa kuwa rehema zake hazikomi…Bwana ndiye fungu langu, husema nafsi yangu, kwa hiyo nitamtumaini yeye.”