Monday, April 17, 2017

WAJIBU AU SHAUKU

“Bali mmebatilisha shauri Langu, Wala hamkutaka maonyo Yangu” (Mithali 1:25).

Wakati wa usiku malaika wa Mungu alimjia Balaamu akiwa na ujumbe, “Usiende pamoja nao; wala usiwalaani watu hawa, maana wamebarikiwa.”…
Kwa mara ya pili Balaamu alijaribiwa tena. Katika kujibu ushawishi wa wale wajumbe alidai kuwa makini na mwenye uadilifu mkubwa mno, akiwahakikishia kwamba hakuna kiasi chochote cha dhahabu na fedha ambacho kingeweza kumshawishi kwenda kinyume na mapenzi ya Mungu. Lakini alitafuta kukubaliana na ombi la mfalme huyo; na licha ya kwamba alikuwa amedhihirishiwa bayana mapenzi ya Mungu, aliwahimiza wale wajumbe wangoje, ili aweze kuulizia tena kwa Mungu; kana kwamba Yeye Asiye na Ukomo alikuwa mwanadamu, awezaye kughilibiwa.
Wakati wa usiku Bwana alimtokea Balaamu na kusema, «Kwa kuwa watu hawa wamekuja kukuita, enenda pamoja nao; lakini neno lile nitakalokuambia ndilo utakalolitenda, basi.» Huo ndio umbali ambao Bwana angeliweza kumruhusu Balaamu ayafuate mapenzi yake mwenyewe, kwa sababu alikuwa amedhamiria juu ya hilo. Hakutafuta kuyatenda mapenzi ya Mungu, bali alichagua njia yake mwenyewe, na kisha akajitahidi kujipatia kibali cha Bwana.

Wapo maelfu hivi leo wanaoenenda katika njia ya namna hiyo. Wasingeliweza kuwa na ugumu wowote wa kuuelewa wajibu wao kama ungelipatana na mielekeo yao. Umeleezwa bayana mbele yao katika Biblia au umeoneshwa waziwazi kwa mazingira na mawazoni. Lakini kwa sababu ushahidi huu hupingana na shauku na mielekeo yao mara kwa mara wanauweka pembeni na kuthubutu kumwendea Mungu ili kutafuta kujua wajibu wao. Kwa uangalifu mkubwa unaoonekana dhahiri wanaomba kwa muda mrefu na kwa bidii ili wapate nuru. Lakini Mungu hatadhihakiwa. Kwa kawaida huwaruhusu watu wa namna hiyo wafuate shauku zao wenyewe na kukabiliana na matokeo husika…. 

Mtu anapouona wajibu wake bayana, hebu asithubutu kumwendea Mungu akiwa na ombi kwamba asamehewe ili asiufanye. Badala yake anapaswa, kwa roho na unyenyekevu na kujisalimisha, aombe nguvu na hekima ya kimbingu ili kutimiza madai yake.

No comments: