Thursday, April 13, 2017

ZAHAMA KATIKA ISRAELI

“Walifanya ndama huko Horebu, Wakaisujudia sanamu ya kuyeyuka. Wakaubadili utukufu wao Kuwa mfano wa ng’ombe mla majani” Zaburi 106:19, 20.

Wakati Musa akiwa hayupo, mamlaka ya kufanya maamuzi yalikasimishwa kwa Haruni, na umati mkubwa ukakusanyika kulizunguka hema lake, wakiwa na dai hili: “Haya! Katufanyizie miungu itakayokwenda mbele yetu, kwa maana Musa huyo… hatujui yaliyompata.” Kuhusu lile wingu, walisema, . . . sasa limetulia kabisa pale mlimani; na lisingeendelea tena kuelekeza safari zao. . . . Zahama kama hiyo ilimhitaji mtu thabiti, mwenye uamuzi imara, na ujasiri usioyumba; yule ambaye ameinua juu heshima ya Mungu kuliko umaarufu wa kupendwa na watu, usalama binafsi, au uhai wenyewe. Lakini kiongozi huyu wa Israeli hakuwa na sifa hizi za kitabia.
Haruni alipingana na watu hawa kinyonge, lakini tabia yake ya kutetereka na woga katika wakati huo hatari sana uliwafanya tu watu hao kuwa washupavu zaidi…. Wapo baadhi walioendelea kuwa waaminifu kwa agano lao pamoja na Mungu, lakini sehemu kubwa sana ya watu hao ilijiunga katika uasi….
Haruni alihofia usalama wake mwenyewe; na badala ya kusimama kwa uadilifu ili kutetea heshima ya Mungu, alikubaliana na madai ya umati huo. . . .
Alitengeneza sanamu ya ndama wa kuyeyusha, kwa kuiga mfano wa miungu ya Misri. Watu hao wakatangaza, “Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri.” Na Haruni kwa uovu akaruhusu tu fedheha hii dhidi ya Yehova. Na alifanya zaidi ya hili. Baada ya kuona jinsi mungu huyo wa dhahabu alivyopokelewa kwa ridhaa, alijenga madhabahu mbele yake, kisha akatangaza akisema, “Kesho itakuwa sikukuu kwa Bwana.”
Tangazo hili lilienezwa kwa matarumbeta toka kundi moja hadi lingine katika mahema yao yote…. Chini ya kisingizio cha kuadhimisha “sikukuu kwa Bwana,” walijiingiza katika shamrashamra za ulafi na ufisadi.
Ni mara nyingi kiasi gani, hata katika siku zetu, ambapo kupenda anasa kunafunikwa kwa “mtindo wa utauwa!” Dini inayowaruhusu wanadamu wajihusishe katika uendekezaji wa ubinafsi au tamaa za kimapenzi, huku wakiendelea kufanya taratibu zao za ibada, huwavutia watu wengi sana wakati huu kama ilivyokuwa katika siku za Israeli.
Na bado wapo akina Haruni wanaoshawishika kirahisi, ambao, wakati wakiendelea kushikilia nyadhifa za uongozi kanisani, watakubaliana na shauku za wale ambao hawajaongoka, na hivyo huwahamasisha katika dhambi.

No comments: