Sunday, April 16, 2017

TOKA KABURI HADI UTUKUFU

“Nikamnyenyekea Bwana wakati huo, nikamwambia,… Nami nakuomba nivuke, nikaione hiyo nchi nzuri iliyoko ng’ambo ya Yordani, mlima ule mzuri, na Lebanoni. Lakini Bwana alikuwa amenikasirikia kwa ajili yenu, asinisikize; Bwana akaniambia, Na ikutoshe, usinene nami zaidi jambo hili”
(Kumbukumbu 3:23-26).

Kamwe haikuwahi kutokea, hadi pale vilipodhihirishwa katika kafara ya Kristo, ndipo ambapo haki na upendo wa Mungu vilioneshwa kwa kiwango kikubwa sana kuliko katika kushughulika Kwake na Musa. Mungu alimzuia Musa asiingie Kanaani, ili afundishe somo ambalo kamwe halipaswi kusahaulika—kwamba Yeye anahitaji utii kamili, na kwamba wanadamu wanapaswa kujihadhari ili wasijitwalie utukufu unaomstahili Muumba wao. Asingeweza kujibu ombi la Musa aliposihi apewe nafasi ya kushiriki urithi wa Israeli, lakini Mungu hakumsahau wala kumwacha mtumishi Wake. Mungu wa mbinguni alielewa mateso ambayo Musa alikuwa ameyastahimili; alikuwa ametazama kila tendo la utumishi wenye uaminifu katika miaka hiyo yote ya mapambano na majaribu. Juu ya Mlima Pisga, Mungu alimwita Musa kuingia katika urithi mtukufu sana usio na ukomo ukilinganishwa na ule wa Kanaani ya duniani..

Katika ule mlima ambako Yesu alibadilikia sura, Musa alikuwepo pamoja na Eliya, waliokuwa wamehamishwa kwenda mbinguni. Walitumwa kama wabeba-nuru na utukufu kutoka kwa Baba hadi kwa Mwanawe. Kwa hiyo, dua ya Musa, iliyotamkwa karne nyingi hapo kabla, hatimaye ilijibiwa. Alisimama kwenye “mlima ule mzuri,” ndani ya urithi wa watu wake….

Musa alikuwa mfano wa Kristo…. Mungu aliona vyema kumfunza Musa katika shule ya mateso na umaskini kabla hajaandaliwa kuliongoza jeshi la Israeli hadi Kanaani ya duniani. Israeli wa Mungu, wanaosafiri kuelekea Kanaani ya mbinguni, wanaye Amri Jeshi asiyehitaji mafundisho ya wanadamu ili kumwandaa kwa ajili ya utume Wake kama kiongozi wa kimbingu; hata hivyo alikamilishwa kupitia mateso; na “kwa kuwa [Yesu] Mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa” (Ebr. 2:10, 18). Mkombozi wetu hakuonesha udhaifu au kasoro yoyote ya kibinadamu; hata hivyo alikufa ili kutununulia sisi urithi wa kuingia katika ile Nchi ya Ahadi.

“Na Musa kweli alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu kama mtumishi,… bali Kristo, kama mwana, juu ya nyumba ya Mungu; ambaye nyumba Yake ni sisi, kama tukishikamana sana na ujasiri wetu na fahari ya taraja letu mpaka mwisho” (Ebr. 3:5, 6).

No comments: