Friday, April 21, 2017

MAMBO YANAYOONDOA FAHAMU ZA MWANADAMU:

"Imeandikwa hivii; "Uzinzi na Divai na Divai mpya huondoa fahamu za mwanadamu" Hosea 4:11.
 
Dhambi ya uzinzi licha ya kwamba sio uzinzi peke yake utakaowakosesha wengi wasiingie mbinguni; lakini neno la Mungu limeizungumza kwa uchungu madhara yake kama mwanadamu angeliielewa. Paulo katika Wakorintho pia alisema mtu akizini msichangamane naye na kwa baadhi ya makanisa mtu anayefumwa katika uzinzi huondolewa katika ushirika wa kanisa. Dhambi hii ni kweli ni sawa tu na dhambi zingine; lakini imetajwa katika dhambi kuu mbili zinazoondoa fahamu za mwanadamu.
 
Biblia inaelewa kwa uwazi kupitia nabii Hosea kwamba Uzinzi na Divai huundoa fahamu za mwanadamu. Mtumishi wa Mungu Sulemani ingawa aliandika yeye mwenyewe katika Kitabu cha Mithali kwamba; "Mtu aziniye na mwanamke hana akili, afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake" Bado kama mwanadamu anayo historia ya kutenda kosa hilo kwa kuoa akina mama 700+300 masuria jumla akawa na 1,000 wake wa kulala nao kimapenzi.
 
Uzinzi na ulevi ni dhambi kuu zinazovuma na zimeshika nafasi ya kwanza katika ulimwengu wa sasa. Wachungaji, mapadre, maaskofu, watumishi wengi wa Mungu, wainjilisti, wahubiri, na waumini wa madhehebu mbalimbali hatuko nyuma katika kujishughulisha na dhambi ya uzinzi na ulevi( Divai) ingawa dhambi ni dhambi bila kujali ni uongo, majungu, masengenyo, wizi wa zaka, ulawiti, ubakaji, uchonganishi, dharau, kiburi, majivuno na kiola aina ya ubaya unaomwandama mwanadamu; ila katika kuondoa ufahamu wa mwanadamu (yaani anakuwa punguwani asiyejielewa kiroho na kuwa mtumwa wa uovu huo) ni Uzinzi na ulevi kama asemavyo Mungu kupitia nabii Hosea, na mtume Paulo.
 
Angalia mtu akilewa anavyokosa adabu, asivyojiheshimu, anavyopiga kelele, anavyosumbua mke au mme wake, anavyotishia watu, anavyopiga mke, anavyopiga mume, anavyopiga watoto! Je, ulevi na kunywa japo kidogo mbele za Mungu ni halali? imeandikwa nini katika Isaya 28:7? ni kosa kumpa mtu kileo. Katika Biblia yaani maandiko matakatifu hakuna fungu linalosema kunywa kidogo ila usilewe, halipo ila ni fundisho miongoni mwa mafundisho ya shetani kwamba watu wanywe kidogo ila wasilewe!
 
Niliwahi kuona mtu mmoja aliyejiita mtumishi wa Mungu akiwa amevalia kanzu akienda katika tukio la ujenzi wa makaburi akawa akizibariki pombe! wakati huo nikiwa gizani kama yeye niliona ni jambo jema; baada ya kupata mafunuo ya Mungu kupitia neno lake nikagundua yule alikuwa mtumishi wa shetani aliyevaa kanzu ya kondoo.
Ulevi umekatazwa kabisa; wapendwa wakristo wenzangu; Uzinzi na ulevi tumwombe Mungu atusaidie dhambi hizi zinaondoa fahamu za mwanadamu; na ujue ya kwamba Fahamu za mtu zikiondoka mtu huyo huitwa mwendawazimu. Soma tena Hosea 4:11 ujue mambo yanayoondoa fahamu za mwanadamu. Mungu halazimishi, ila anaonya ili isiwe siku ya kutupwa katika ziwa la moto ukamlaumu kwamba hukumu zake si za haki. Ni lazima siku zote Mungu aonye ukatae ili siku ya hukumu maneno yaleyale uliyoyakataa yawe sheria mbele zake ya kukugeuka. Amua leo kumtii Mungu katika kila jambo ili uwe salama. Haleluya!

No comments: