Monday, June 16, 2014

HIVI MWISHO WA DUNIA UTAKUWAJE?



DANIEL NA SIKU ZETU

                (SOMA DANIELI 12 YOTE)

Yapo mawazo mengi wanayosema watu kuhusu mwisho wa dunia. Wengine wanasema watakatifu watanyakuliwa kwenda mbinguni na waovu wote wataangamizwa; dunia itabaki tupu. Wengine wanasema kanisa peke yake ndilo litanyakuliwa; watu waliobaki wataendelea kuishi duniani, na injili itahubiriwa kwa Wayahudi; ndipo Mpinga Kristo atakuja na kufanya mambo yake. Wengine wanasema mbinguni watakwenda tu wale 144,000, watu wengine wote waliobaki makao yao ni hapa duniani; na ya Kwamba dunia hii haiwezi kuharibiwa. Kwa hiyo wanaangalia majengo mazuri na kusema moyoni "Nitarithi jumba hili". Je! Biblia inatupa picha gani juu ya mwisho wa dunia? Na tunaposema tunaishi siku za mwisho tuna maana gani? Zilianza lini kuhesabiwa? Hebu Danieli atuambie katika Sura hii ya 12.
Mwanzo wa siku za mwisho (Dan. 12:5-7): Tunaona kipindi kile kile cha Danieli 7:25 kinatajwa hapa tena na "mtu yule aliyevikwa nguo za kitani" [Kristo] anayeonekana pia katika Ufu. 10:1-7. Soma pia Mt. 17:1,2; Mk. 9:2,3. Anasema hivi, "Itakuwa wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati; tena watakapokuwa wamekwisha kuvunja nguvu za hao watu watakatifu, ndipo mwisho wa mambo hayo yote yatakapotimizwa" (fungu la 7). Maneno hayo aliyatoa akijibu swali la mmoja aliyemwuliza, "Je! itakuwa muda wa miaka
mingapi hata mwisho wa mambo haya ya ajabu? (fungu la 6). "Mambo ya ajabu" ni mauaji yaliyofanywa na Upapa katika Zama zile za Giza ulipoua zaidi ya watakatifu milioni 50, ambayo yalimshangaza pia hata Yohana (Ufu. 17:6). Kanisa kuua kanisa ni ajabu kuu!
Litakwenda mbingu ya nani? Nyakati 3 1/2 ni miaka 3 1/2 au miezi 42 au siku 1260 za unabii ambazo ni miaka 1260 ya Ufalme wa Papa wa Awamu ya Kwanza (538-1798). Kipindi hicho kimetajwa tena na tena katika unabii (Dan. 7:25; Ufu. 12:6,14; 13:5; 11:2,3; Mt. 24:21,22). Katika Dan. 11:33,34 anasema, "... wataanguka kwa upanga, na kwa moto, na kwa kufungwa, na kwa kutekwa nyara, siku nyingi [538-1798]. Upapa ulitumia upanga, moto, kifungo, kuteka nyara kama unabii unavyosema katika kuwaua watakatifu. Mateso yalikuwa mabaya mno kuliko ya watu wasiomjua Mungu. Ufalme wa Papa ulioitawala dunia (Ulaya Magharibi) ulivunjwa na Wafaransa mapema mwaka 1798. Kuanzia hapo fungu la Dan. 12:4 likaanza kutimia. Maarifa ya kidini, kisayansi na kiteknolojia yaliongezeka kasi kwa namna ya ajabu. Zama za Giza hazikuwa na maendeleo yo yote. Wana-sayansi na Wanadini waliofuata Biblia walikuwa wanauawa. Mwaka 1798 ndio mwanzo wa "Siku za Mwisho". Mwisho wake utakuwa katika Awamu ya Pili inayokuja ya Ufalme wa Papa ----- "tena watakapokuwa wamekwisha kuvunja nguvu za hao watu watakatifu" (Dan. 12:7). Historia inajirudia yenyewe. Mateso na mauaji ya watakatifu yatakuja tena atakapotawala Papa (Ufu. 6:9-11) ----- "wakaambiwa wastarehe bado muda mchache, hata itakapotimia hesabu ya wajoli wao na ndugu zao, watakaouawa vile vile kama wao." Wengi hawaamini maneno hayo; lakini wanapaswa kungoja mpaka yatakapotimia ndipo watakapoamini (Yoh. 14:29).
Kusimamishwa kwa Chukizo la Uharibifu au Mwanzo wa Ufalme wa Papa (Upapa):
Rumi ya Kipagani iliangushwa na makabila ya kipagani ya Ulaya Kaskazini mwaka 476 B.K. Tangu siku za Mfalme Konstantino, mwaka 330, Askofu wa Roma au Papa aliachiwa kutawala mji wa Roma. Kwa hiyo Dola ya Magharibi ya Rumi ilipoanguka, Papa aliendelea kutawala mji ule. Alishika hatamu za utawala juu ya Ulaya Magharibi kuanzia mwaka 538 baada ya kuzing'oa falme tatu - Waheruli (493), Wavandali (534), na Waostrogothi (mapema 538).
Mataifa yale mengine ya Ulaya yalipokea Ukatoliki kwa upanga wa Mfalme Clovis wa Ufaransa. Kwa hiyo, yakajikuta yako tena chini ya Papa, (538-1798). Clovis alifanikiwa kuyafanya Wakatoliki mwaka 508 (Dan. 12:11,12). Kuanzia mwaka huo wa 508 zinahesabiwa siku au miaka 1290 na 1335. Chukizo la Uharibifu lilisimamishwa [lilitawala] kuanzia 538 - 1798 (yaani, miaka 508 + 1290 = 1798 barabara). Mwaka ule wa 1798 ukawa ndio mwanzo wa siku za mwisho. Hukumu ikawekwa mbinguni kumpimia adhabu yake mwaka 1844, yaani, mwisho wa miaka ile 2300 ya Dan. 8:14 (yaani, miaka 508 + 1335 = 1843-1844). Mwaka ukianza tarehe 2 Januari unamalizika katika mwaka unaofuata.
Kuna heri gani kwa watu watakaoufikia mwaka 1844, mwaka ambao Hukumu ilianza mbinguni? Wale walio na hekima "watajitakasa na kujifanya weupe" (Dan. 12:3,9,10); tena watasimama kama Danieli katika "kura" yao, yaani, majina yao yatabaki katika Kitabu cha Uzima mbinguni pamoja na watakatifu wote waliotangulia (Dan. 12:13). Isitoshe heri nyingine ni ile ya kufufuliwa katika ufufuo wa pekee (Dan. 12:2; Ufu. 14:13) kwa wale wote walioshiriki kuihubiri Injili ya Milele kwa uaminifu (Ufu. 14:6-12). Injili hiyo inayoitwa "Ujumbe wa Malaika Watatu" ilianza kuhubiriwa 1840-1844 na bado inahubiriwa. Ufufuo wa watakatifu wote utafuata mara tu baada ya ufufuo huo wa mseto utakaokuwa na wale waliomchoma pamoja na wale waliowatesa sana watu wa Mungu (Ufu. 1:7; 1 The. 4:16,17[18]).

MWISHO WA DUNIA UTAKUWAJE?
 Tumeona jinsi Ufalme wa Papa ulivyotawala katika Awamu ya Kwanza (538-1798) na ya kwamba unakwenda kutawala dunia tena. Hiyo itakuwa ni awamu yake ya pili na ya mwisho. Maangamizi ndiyo yatakayokuwa mwisho wa Ufalme huo. Mfuatano wa matukio ni huu ----- Papa atawala awamu ya pili, mateso na mauaji ya watakatifu yaanza tena kwa kipindi kifupi sana, Kristo, Kuhani wetu Mkuu, anamaliza kazi yake ya Maombezi katika Hekalu la Mbinguni na kuufunga mlango wa kutubu au wa rehema kwa tamko la Ufu. 22:11. Watu wa Mungu wametiwa muhuri wa Mungu katika vipaji vya nyuso zao; na watu wa Mnyama wamepata alama ya mnyama vipajini mwao na katika mikono yao. Wakati wa taabu unaanza (Dan. 12:1) Mikaeli (Kristo) anapotawazwa (anaposimama) katika Jiji la Yerusalemu juu; pepo za vita zilizozuiwa zaachiliwa na vita inatapakaa kila mahali ikileta maafa mengi(Ufu. 7:1-4), vimbunga na maafa mengine yanatokea, ndipo silaha ya Mungu ya kutisha sana kwa wale walioikanyaga Sabato yake itakapotumika (Mapigo 7 ya Ufunuo 16). Wale wote watakaomfuata Papa majina yao yataondolewa katika kitabu cha uzima (Kut. 32:32,33; Ufu. 13:8). Mtihani wa siku za mwisho ni Amri ya Nne [Sabato](Ufu. 3:10; 14:9,10).
Mchezo wa kuiweka Jumapili badala ya Sabato [Jumamosi] utakuwa na athari mbaya mno kwa dunia nzima (Isa. 24:1-6,19,20; Ufu. 19:11-21). Ole kwa wafalme wa dunia hii! Ole kwa kila mtu asiyesimama upande wa Yesu Kristo katika Pambano hili Kuu! Karibu sana litafikia mwisho wake. Watoto wa Mungu wamechoka na dunia hii wanataka kwenda kupumzika mbinguni kwa miaka 1000, na Yesu anasema. " Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo" (Ufu. 22:11). Je! u tayari kumlaki Bwana? Je! utasimama imara hata kama mbingu zikianguka, na kuiinua juu Bendera ya Imanueli [Kristo] iliyoandikwa "Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao Amri [Kumi] za Mungu, na Imani ya Yesu" (Ufu. 14:12). Hivi karibuni dunia hii itabaki tupu, ndugu yangu. Kuanzia leo chagua kuingia Paradiso pamoja na Kristo (Luka 23:42,43; 2 Kor. 6:2). Huenda usisikie mwito mwingine kama huu. Amua leo!


AMRI ZA MUNGU NA SHERIA ZA MUSA



MARA NYINGI WATU WANASHINDWA KUTOFAUTISAHA KATI YA AMRI ZA MUNGU NA SHERIA ZA MUSA ZIFUATAZO NI TOFAUTI
1. ZA MUNGU Ziliandikwa na Mungu mwenyewe Kwa kidole chake [Torati 31:18]
ZA MUSA Ziliandikwa na Musa mwenyewe kwa k wa kidole
2.Ziliandikwa kwenye mbao mbili za mawe yaliyochongwa, Torati 10:1-4
ZA MUSA Ziliandikwa kwenye chuo(kitabu cha dini), Torati 31:24
3., ZA MUNGU Ziliwekwa ndani ya Sanduku la Agano Torati 10:1-4
ZA MUSA Baada ya kuandikwa, ziliwekwa nje pembeni ya Sanduku la Agano,
Torati 31:24-27
4 . Waliozivunja, walionekana kutenda dhambi 1Yoh. 3:4, na iliwapasa kufa. Torati 17:2-5
ZA MUSA Waliozivunja, hawakuonekana na dhambi wala haikuwapasa kufa kwani zilikuwa ni kivuli cha Kristo Wakolosai 2:14-17
5. Yesu alikuja kuzitimiliza wala si ku zitangua. Watu wote wanapaswa kuzifundisha…Mathayo 5:17-19 -
ZA MUSA Yesu aliziondoa pale msalabani maana zilikuwa ni sheria za maa gizo
tu yaliyosimama kama kivuli cha mema yajayo. Kolosai 2:15
6. Sheria(torati) ya Bwana ni takatifu njema na ya haki, nayo yadumu mi lele na milele, Warumi 7:12-
ZA MUSA Zilikuwa ni kivuli cha kazi ya Yesu aliyoifanya msalabani, nazo zilikomea hapo. Ebran. 10:1-12
7. Sheria za Bwana ni kamilifu, za adili, kweli na za milele Zaburi 111:7-8
ZA MUSA Ziliishia pale Kristo alipokufa Msalabani. Waebran. 9:10-12, Luka 22:37
A. Mfano wa sheria ya Musa
1. Kuchinja kondoo kama mbadala wa mdhambi. Kutoka 29…, Walawi, Torati, Nyakati nk
2. Kifo yeyote aliyevunja mojawapo au Amri zote 10 za Mungu
Kutoka 31:14… Basi mtaishika hiyo Sabato; kwa kuwa ni takatifu kwenu; kila mtu atakayeitia unajisi hakika yake atauawa; kwa kuwa kila mtu afanyaye kazi katika siku hiyo, nafsi hiyo itakatiliwa mbali na watu wake.
B. Sheria za Mungu, Kutoka 20 :1-17
Hivyo basi Yesu alipokufa Msalabani sheria za kuchinja kondoo tena ziliisha maana mwanakondoo wa Mungu (Yesu) aichukuaye dhambi ya ulimwengu alikuwa ameshachinjwa tayari.
Yohana 1:29 Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu!

HIVI KWELI KIFO CHA YESU MSALABANI KILIIONDOA SABATO YA AMRI YA NNE?

EBU TUANGALIE MITUME WA YESU KAMA WALIENDELEA KUISHIKA SABATO BAADA YA YESU KUFA NA KUPAA MBINGUNI AU HAWAKUISHIKA?
Matendo ya Mitume 13:14 Lakini wao wakatoka Perge, wakapita kati ya nchi, wakafika Antiokia, mji wa Pisidia, wakaingia katika sinagogi siku ya sabato, wakaketi.
Matendo ya Mitume 13:27 Kwa maana wakaao Yerusalemu, na wakuu wao, kwa kuwa hawakumjua yeye, wala maneno ya manabii yanayosomwa kila sabato, wameyatimiza kwa kumhukumu.
Matendo ya Mitume 13:42 Na walipokuwa wakitoka, wakawasihi waambiwe maneno haya sabato ya pili.
Matendo ya Mitume 13:44 Hata sabato ya pili, watu wengi, karibu mji wote, wakakusanyika walisikie neno la Mungu.
Matendo ya Mitume 15:21 Kwa maana tangu zamani za kale Musa anao watu wahubirio mambo yake; katika kila mji husomwa kila sabato katika masinagogi.
Matendo ya Mitume 16:13 Hata siku ya sabato tukatoka nje ya lango, tukaenda kando ya mto, ambapo tukadhani ya kuwa pana mahali pa kusali; tukaketi, tukasema na wanawake waliokutana pale.
Matendo ya Mitume 17:2 Na Paulo, kama ilivyokuwa desturi yake, akaingia mle walimo, akahojiana nao kwa maneno ya maandiko sabato tatu,
Matendo ya Mitume 18:4 Akatoa hoja zake katika sinagogi kila sabato, akajaribu kuwavuta Wayahudi na Wayunani.
• Paulo bado anasisitiza
Waebrania 4:9 Basi, imesalia raha ya sabato kwa watu wa Mungu.
• Isaya anasema hadi mbinguni, tutaitunza Sabato ya Bwana
Isaya 66 :22 Kama vile mbingu mpya na nchi mpya, nitakazofanya, zitakavyokaa mbele zangu, asema Bwana, ndivyo uzao wenu na jina lenu litakavyokaa. 23 Na itakuwa, mwezi mpya hata mwezi mpya, na sabato hata sabato, wanadamu wote watakuja kuabudu mbele zangu, asema Bwana.
Kwani siku ya Sabato in Ipi ??
Mathayo 28:1 Hata sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi.
Marko 16:2 Hata alfajiri mapema, siku ya kwanza ya juma, wakaenda kaburini, jua lilipoanza kuchomoza;
Marko 16:9 Naye alipofufuka alfajiri siku ya kwanza ya juma, alimtokea kwanza Mariamu Magdalene, ambaye kwamba alimtoa pepo saba.
Luka 24:1 Hata siku ya kwanza ya juma, ilipoanza kupambazuka, walikwenda kaburini, wakiyaleta manukato waliyoweka tayari.
Yohana 20:1 Hata siku ya kwanza ya juma Mariamu Magdalene alikwenda kaburini alfajiri, kungali giza bado; akaliona lile jiwe limeondolewa kaburini.
Yohana 20:19 Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu.
Yesu alifufuka siku ya jumapili ambayo Biblia inaiita kuwa ni siku ya kwanza ya juma. Kama Yesu alifufufuka siku ya kwanza ya juma(jumapili), Sabato itakuwa lini??
Jibu: Jumamosi
Karibu tujiunge kwenye kundi dogooo. Kundi dogo liendalo Uzimani.
Matt 7:13 Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo.
14 Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache.
 
MWENYE MASIKIO NA ASIKIE.