Friday, April 14, 2017

ANATUPENDA JINSI TULIVYO

Kwa kawaida watu hupenda kile kinachowaongezea furaha au faida fulani. Ni vigumu kwa binadamu kupenda kisichomvutia na kinachomtia hasara au kumpenda kiumbe aliyejitangaza mwenyewe kuwa adui. “Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.” (Warumi 5:8) Tangu dhambi ilipoingia duniani, sisi wanadamu tumekuwa adui wa Mungu. Tumekuwa tukimkimbia Mungu kila anapotusogelea. “Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha.” (Mwanzo 3:9-10)

Maagizo ya Mungu yamejenga uadui nafsini mwetu. “Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.” (Warumi 8:7) Hali hiyo ilipelekea maisha kuwa yasiyo na amani jambo lililohitaji uingiliaji kati wa haraka. Mungu aliuondoa uadui huo kwa kifo cha Yesu pale msalabani. “Akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.” (Wakolosai 2:14-15)

Upendo huu wa kuwapenda rafiki zako ambao bado wanakuchukulia kuwa ni adui yao unapatikana kwa Mungu pekee. “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.” (Yohana 15:13) Upendo huu hauangalii kama anayependwa ataitikia upendo huo na kukubali kurejeshwa kwa mahusiano ama ataendelea na dhana yake ya uadui. Upendo ulio tayari kutoa uhai kwa ajili ya wengine. Mungu hatupendi kwa matarajio kuwa tutampenda. Anawapenda wote wema kwa wabaya na angependa nasi tupendane kwa bila kubagua. “Ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.” (Mathayo 5:45)

Upendo wa Mungu ni tabia yake ambayo haitegemei mazingira. “Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake.” (1 Yohana 4:16). Upendo wa kibinadamu ungekuwa kama ule wa Mungu ungekuwa haulazimishwi na faida utakazozipata kwa unayempenda. Tabia yetu ya upendo ungejengwa juu uthamani wa kila kiumbe kilichoumbwa na Mungu na wala si mwonekano wa nje tu wa viumbe hivyo, tusingeshuhudia unyanyapaa uliopo. “Maana mkiwapenda wale wawapendao ninyi, mwaonyesha fadhili gani? Kwa kuwa hata wenye dhambi huwapenda wale wawapendao.” (Luka 6:32)
Mwanadamu ni kiumbe anayestahili kupendwa kwa sababu kuu mbili. Anastahili kupendwa kwa sababu aliumbwa katika viwango vya juu vya ubora. “Mtu ni kitu gani hata umkumbuke, Na binadamu hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; Umemvika taji ya utukufu na heshima.” (Zaburi 8:4-5) Mwanadamu amefanyika katika viwango vya ubora ulio chini kidogo ya ule wa Mungu. “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.” (Mwanzo 1:26)

Sababu ya pili kwa nini mwanadamu ni wa thamani na anayestahili kupendwa ni ule ukweli kuwa alikombolewa kwa thamani kubwa kuliko thamani zote za duniani na mbinguni. “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo.” (1 Petro 1:18-19). Amgusaye mwanadamu ni sawa na yule aigusaye mboni ya jicho la Mungu. “Kwa maana Bwana wa majeshi asema hivi, Ili nitafute utukufu amenituma kwa mataifa wale waliowateka ninyi; maana yeye awagusaye ninyi aigusa mboni ya jicho lake.” (Zekaria 2:8)

Mungu anatualika kujifunza upendo wake mkuu kwa wanadamu. “Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu.” (Waefeso 3:17-19) Mungu anatupenda tulivyo.

No comments: