Sunday, June 10, 2012

YESU ANAKUJA TENA.

UJIO WA YESU MARA YA PILI NI FURAHA KWA WOTE WANAOMTAZAMIA KWA WOKOVU.

 

Fungu la tafakari: “Nitakuja tena niwakaribishe kwangu, ili nilipo mimi, nanyi muwepo.” Yohana 14:3.

Makusudi ya somo hili: Kufahamu sababu inayomleta Kristo na jinsi atakavyokuja. Nilazima kuwa tayari kwa siku ile.

UTANGULIZI..
Ishara za mbingu na nchi zinatuonyesha kuwa Yesu anakuja tena. Na kwa sababu ya kifo chake msalabani ni lazima arudi kuwapatia waliomwamini tunu za imani zao.

Tunauhakika kuwa Yesu anakuja tena, tunarejea kauli yake mwenyewe alisema, “Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.” Yohana 14:3.
Ebrania 9:28 anasema, “kadhalika Kristo naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu.”

Lakini pia kunaunabii uliotabiliwa juu ya Yesu kuja tena mara ya pili katika agano la kale na jipya. (Yuda 1:14,15) Na Henoko, mtu wa saba baada ya Adamu, alitoa maneno ya unabii juu ya hao, akisema, Angalia, Bwana alikuja na watakatifu wake, maelfu maelfu, ili afanye hukumu juu ya watu wote, na kuwaadhibisha wote wasiomcha Mungu, kwa ajili ya kazi zao zote za upotevu walizozitenda bila kumcha Mungu, na kwa ajili ya maneno magumu yote ambayo hao wenye dhambi wasiomcha Mungu wameyanena juu yake.
(Zaburi 50:3) Mungu wetu atakuja wala hatanyamaza, Moto utakula mbele zake, na tufani yavuma sana ikimzunguka pande zote. (Ayubu 19:25-27) Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi. Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi, Lakini, pasipokuwa na mwili wangu nitamwona Mungu; Nami nitamwona mimi nafsi yangu, Na macho yangu yatamtazama, wala si mwingine. Mtima wangu unazimia ndani yangu.

Moja ya ukweli makini kuliko kweli zote, na wemye utukufu mwingi ndani ya Biblia ni ule wa kurudi kwake mara ya pili, ili kumaliza kazi kubwa ya ukombozi. Watakatifu wa zamani walitazamia kurejea kwa Masihi katika utukufu, kuwa ni kilele cha matumaini yao. “Anakuja kukusanya watakatifu wake waliofanya agano naye kwa dhabihu.” Zaburi 50:5
 Atawatuma Malaika zake nao watawakusanya wateule wake toka pande kuu nne za dunia, na waliokufa katika krito watafufuliwa kwanza, kisha sisi tulio hai tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu. Mathayo 24:31; 1Watesalonike 4:16,17.

Kuja kwa Yesu sio siri, Biblia imeweka bayana kuwa kila jicho litamwona, pia katika kitabu cha Matendo 1:9-11, Hapa kuna kisa cha Yesu alivyopaa kwenda kwa Baba, wakati wanafunzi wakikaza macho yao kuelekea Mbinguni, 
Malaika akawambia jinsi mlivyomwona akienda zake mbinguni, atakuja jinsi hiyo hiyo. Ufunuo 1:7.

Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Mathayo 24:27; 26:27;24:30, Luka 9:26.

Kristo atakuja katika utukufu wake mwenyewe, katika utukufu wa Baba yake, na katika utukufu wa Malaika watakatifu. Elfu kumi mara elfu kumi na maelfu elfu ya malaika. Kila jicho litamwona na hao waliomchoma watamwona. Mahali pa taji ya miiba, atavaa taji ya utukufu. Mahali pa lile vazi la kifalme la zambarau lililochakaa, atavikwa mavazi meupe sana, Marko 9:3. Na katika vazi lake na kwenye paji la uso wake limeandikwa jina, “Mfalme wa wafalme, na Bwana wa Mabwana.

Lakini matokeo ya kuja kwake Mwokozi, kwa waovu itakuwa ni kilio na kusaga meno, Ufunuo 6:15-17; 2Wathesalonike 1:6.

Kuja kwa Yesu mara ya pili kwa watakatifu itakuwa ni furaha isiyoelezeka, Isaya 25:9; Mathayo 25:34-40. na watafanana naye 1Yohana 3:2,3.

WITO: MPOKEE YESU AWE BWANA NA MWOKOZI WA MAISHA YAKO BINAFSI, HUTA JUTA FURAHA KAMILI ITAKUJAZA NA UTAFURAHIA MAISHA YA MILELE.

No comments: