Tuesday, June 5, 2012

KUMFAHAMU MUNGU WETU


KUMFAHAMU MUNGU WETU NI JMBO LA MSINGI SANA: KARIBU KATIKA SOMO HILI.

Fungu la tafakari: “Bali BWANA ndiye Mungu wa Kweli; Ndiye Mungu aliye hai, Mfalme wa milele.” Yeremia 10:10.

Makusudi ya somo hili: Ni kufahamu kuwa tunaye Mungu mmoja na kuwa si kama mifano inayofanywa na mwanadamu.

UTANGULIZI..
Mungu ni nini? Na ni nani? Hili ni swali la msingi kabisa unaloweza kuuliza. Majibu kwa maswali muhimu maishani mwako hupatikana kwa kutegemea unamwelewaje Mungu. Fikira zako juu ya Mungu zinaathiri mtazamo wako wa kila jambo; muhimu zaidi, ni namna unavyojitazama. Maisha yanathamani yoyote? Kuna sababu ya kuhangaika leo? Je, lipo tumaini la kesho? Bila shaka, utambuzi wako wa Mungu utapelekea kupata majibu kwa maswali haya, na kupata mengine zaidi. Ikiwa ni muhimu kiasi hicho kuwa na maarifa sahihi ya Mungu, unawezaje kumfahamu Mungu.

Je, inawezekana kwa mwanadamu kumjua Mungu?
Ndiyo, inawezekana kabisa. Yohana 17:3, Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.
Tutapata uzima wa milele ikiwa tayari tunao ufahamu kamili wa huyu tunaye mtumikia (Mungu) na Kristo Mwokozi wetu.
Yesu alikuja.....”naye ametupa akili kwamba tumjue yeye aliye wa kweli,.... huyu ndiye Mungu wa kweli na uzima wa milele. 1Yohana 5:20.
Tukimwamini Yesu tutamjua na Baba, maana atatufunulia Mathayo 11:27.
1Wakorintho 1:21.

Kumjua Mungu hakupatikani kwa kutegemea ubongo wa mwanadamu bali moyo wa mwanadamu. Ujuzi wa mambo ya kidunia hutegemea uwezo wa wa kiakili wa mtu, lakini kumfahamu Mungu hakutafutiki kwa njia za kibinadamu. Kutumia akili za kibinadamu kujaribu kumjua Mungu  kunafananishwa na kujaribu kutumia tochi kulichunguza jua, jambo lisilowezekana kabisa.
Wasioamini hawawezi kabisa kumjua Mungu. Ujuzi wa Mungu unapatikana pale mtu anapoamini na kufanyia kazi kila ujuzi anaoupata. (Yohana 7:17).
  Hakuna mawazo ya mwanadamu yanayoweza kumtambua Mungu. Hebu mwanadamu dhaifu na mwenye ukomo asijaribu kumtafsiri au kubashiri habari za Mungu. ... Mwenye maarifa yote hajadiliwi.
Kadri tunavyojifunza zaidi na zaidi jinsi Mungu alivyo, na jinsi sisi  wenyewe tulivyo mbele zake, tutaweza kuogopa na kutetemeka  mbele zake. 8T. Uk, 283

Kama kila kilichoko duniani kina msanii basi hata ulimwengu huu na vyote vilivyomo kunamsanii aliye sanifu. Zaburi 19:1, Na vyote vinatangaza utukufu wake, na nikazi ya mikono yake.
Warumi 1:20; Zaburi 14:1; Warumi 1:18-22,28.

Viumbe vya asili na Maandiko matakatifu ni vyanzo vikubwa viwili vya ushahidi wa uwepo wa Mungu.

Unaweza ukawa unajiuliza maswali mengi kuhusu Mungu, maana kuna Yesu, na Roho Mtakatifu,  je, kuna Mungu watatu mbinguni? Swali la msingi sana hili.

Maelezo: Maandiko Matakatifu yanasisitiza juu ya kuwepo kwa Mungu Mmoja; Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu, umoja wa nafsi tatu za milele. Katika mashirika ya kibinadamu madaraka ya mwisho huwa juu ya mtu mmoja – Raisi, Mfalme, au Waziri mkuu.
Katika Utatu Mtakatifu, madaraka ya mwisho yapo kwa wote Watatu. Pamoja na kwamba Utatu Mtakatifu si nafsi moja, Mungu ni mmoja. Umoja huu hauondoi nafsi tatu huru zinazojitegemea za Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Na pia utofauti wa nafsi Uungu haziharibu mkazo wa maandiko matakatifu kwamba Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu ni Mungu Mmoja.
Torati 6:4; Waefeso 4:4-6; Mwanzo 1:26;3:22;11:7; Isaya 48:16; Yohana 14:16.

Majina ya Mungu:
(a) El na Elohim, yaani ‘Mungu’ Jina hili huonyesha nguvu ya kiungu ya Mungu. Humuonyesha Mungu kuwa mwenye nguvu na Muumbaji (Mwanzo1:1; Kutoka 20:2; Daniel 9:4)
(b) Elyon, yaani ‘Aliye juu sana’ na El Elyon, yaani ‘Mungu Aliye juu sana’ Jina hili huelezea jinsi alivyotukukuka. (Mwanzo 14:18-20; na Isaya 14:14)
(c) Adonai, yaani ‘Bwana’ Jina hili humwelezea Mungu kama Mtawala Mwenye Enzi (Isaya 6:1; Zaburi 35:23)

Yako majini mengine ambayo huonyesha utayari wa Mungu wa kufanya urafiki na watu wake. Majina hayo ni pamoja na Shaddai, yaani ‘Mwnyezi’ na El Shaddai. Yaani ‘Mungu Mwenyezi’ Jina hili humwelezea Mungu Mwenyezi kuwa ni chanzo cha baraka na faraja (Isaya 6:3; Zaburi 91:1). Jina jingine ni Yahweh, ambalo hufasiliwa kama Yehovah au BWANA, ambalo husisitiza uaminifu na neema za agano la Mungu. (Kutoka 15:2; Hosea 12:5,6)

Kuna mabo mengi kumhusu Muumbaji wetu hata vitabu havitoshi kuelezea, kulingana na akili zetu finyu zilizoathiriwa kwa kiwango kikubwa na dhambi, kwaleo tuishie hapa. Natumai somo hili limekutoa sehemu moja na kukusogeza sehemu nyingine karibu na Mungu wetu.

WITO: KWA MUNGU YOTE YANAWEZEKANA (MATHAYO19:26).



No comments: