Friday, June 8, 2012

AHADI KWA WASHINDI WA DHAMBI.


PAMOJA NA YESU USHINDI NI WA HAKIKA.

Fungu la tafakari: “Yeye ashindaye atayarithi haya” Ufunuo 21:17.

Makusudi ya somo hili: Kujua kwamba juhudi ya kushinda inahitajika na kufaa  zaidi.

UTANGULIZI..
Maisha haya yanatakiwa kuwa matayarisho ya maisha yajayo. Lakini maonyo juu ya hatari ya maisha haya ni lazima yazingatiwe. Tabia inapasa kukamilika. Kila dhambi ni lazima ishindwe. Mungu ameweka mambo haya kama sharti, ili iwezekane kupata thawabu ya mshindaji.

Biblia inasema katika kitabu cha Warumi 12:21; Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.
Ubaya unaonekana ulimwenguni. Unaelezwa katika 1Yohana 2:16 kuwa ni “tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima” Tunapaswa kujihadhari daima ili kwamba mambo haya yasitushinde.

Kushindwa mara moja kunamwacha mtu bila ulinzi wa Mungu. Kawaida moja mbaya, kama haipingwi kwa nguvu, itatia nguvu minyororo ya chuma ya shetani, na kufunga nyanja zote za mtu kamili.

Lazima tuzaliwe na mungu ndipo tutakuwa na uwezo wa kuushinda ulimwengu, maana tutakuwa na nguvu ndani yetu. Tusalimishe nia na mapenzi yetu kwake. 1Yohana 5:4.

Kama wakristo lazima waidhibiti na kuitawala miili yao, kuziweka hamu zao za chakula na tamaa zao zote chini ya dhamiri zilizoelimishwa, waone kuwa ni wajibu wao kwa Mungu kuzitii sheria ambazo zinatawala afya na maisha, watapata mbaraka wa nguvu za kimwili na kiakili. Watapata nguvu za kimaadili (moral power) za kupigana na shetani.

Watu wanaweza kushinda kwa njia ya Yesu Kristo peke yake. “ Pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote. Yohana 15:5.
Kinga ya pekee dhidi ya uovu ni uwepo wa Kristo ndani ya moyo kwa njia ya imani kwa haki yake. Hatuwezi kamwe kuyazuiya matokeo mabaya ya kujipenda nafsi, kujifurahisha kwa  anasa , na kujaribiwa kutenda dhambi, isipokuwa tumeunganishwa kabisa na Mungu. ... Pasipo kuwa na ujuzi binafsi wa Kristo, na kuwa na ushirika naye unaoendelea, tunakuwa bado tuko chini ya hatarti ya kuvamiwa na adui, na tutaishi kuyafanya matakwa ya adui.
Lakini Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo. 1Wakorintho 15:57; Ufunuo 12:11.
Wengi wanataka thawabu ya mwisho na ushindi ambao unatolewa kwa washindi, lakini hawako tayari kustahimiri magumu, taabu, na kujikana nafsi, kama alivyofanya Mwokozi. Tutashinda tu kwa njia ya utii na juhudi zinazoendelea.

Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa kula matunda ya mti wa uzima, ulio katika bustani ya Mungu.
Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili.
Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa, nami nitampa jiwe jeupe, na juu ya jiwe hilo limeandikwa jina jipya asilolijua mtu ila yeye anayelipokea.
Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake. Ufunuo 2:7,11,17;3:5.
Ukiwa mshindi:
...“Utapata jina jipya” Ufunuo 3:12.
...”Utaketi pamoja na Kristo” Ufunuo 3:21;21:7.
Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu, mambo ambayo Mungu amewaandalia wampendao 1Wakorintho 2:9.

RAFIKI YANGU NINAKUALIKA TUUNGANE NA MWOKOZI WETU ILI TUPATE UZIMA, MAMBO AMBAYO JICHO “HALIKUYAONA” YATAKUWA YETU. KILA MTU ANAPASWA AWE MSHINDI ILI ASIYAKOSE MEMA HAYA.

 

 

 

 

 

BWANA AKUBARIKI SANA! KARIBU TENA KWA MASOMO YAJAYO.

No comments: