Tuesday, April 18, 2017

WAWILI WANAOFANANA

“Jihadharini na kila aina ya tamaa; maana uhai wa mtu hautegemei wingi wa vitu alivyo navyo”
(Luka 12:15, Biblia Habari Njema)..

Laana ambayo Balaamu hakuwa ameruhusiwa kuitamka dhidi ya watu wa Mungu, hatimaye alifanikiwa kuwasababishia kwa kuwashawishi waingie dhambini..
Balaamu alishuhudia mafanikio ya njama zake za kishetani. Aliona laana ya Mungu ikipatilizwa kwa watu Wake, na maelfu wakianguka chini ya hukumu Zake; lakini haki ya Mungu iliyoadhimu dhambi katika Israeli haikuwaruhusu wale wajaribu kusalimika. Katika vita Israeli ya dhidi ya Wamidiani, Balaamu aliuawa kwa upanga….
Mauti ya Balaamu yalikuwa yanafanana na yale ya Yuda, na tabia zao hubeba ufanano bayana kabisa wa mmoja kwa mwenzake. Watu hawa wawili walijaribu kuunganisha utumishi wa Mungu na mali, na wakashindwa vibaya sana. Balaamu alimkiri Mungu wa kweli, na akadai kumtumikia; Yuda alimwamini Yesu kama Masihi, na akaungana na wafuasi Wake. Lakini Balaamu alitafuta kuufanya utumishi wa Yehova kuwa kama njia ya kujipatia utajiri na heshima ya kidunia; na aliposhindwa katika hili, alijikwaa na kuanguka na akavunjika. Yuda alitegemea kwamba katika kujihusianisha na Kristo angejipatia mali na kupandishwa hadhi ya juu katika ufalme huo wa kiulimwengu, ambao, kama alivyoamini, Masihi alikuwa akielekea kuuanzisha. Kushindwa kutimia kwa matarajio yake kulimsukuma kwenda katika uasi na uangamivu. Balaamu na Yuda walikuwa wamepokea nuru kuu na walifurahia fadhila maalumu, lakini dhambi moja iliyoendekezwa iliharibu kabisa tabia yote na kusababisha uangamivu wao….
Dhambi moja ambayo mtu hataki kuiacha, kidogo kidogo, huhafifisha tabia, ikisababisha uwezo wake wote wa uadilifu kutawaliwa na shauku zake ovu. Kuondolewa kwa ulinzi mmoja toka katika dhamiri, uendekezaji wa tabia moja ya uovu, upuuziaji mmoja wa madai ya juu ya wajibu, huvunja ulinzi wa roho na humfungulia Shetani njia ya kuingia ndani na kutuongoza kwenye ukengeufu. Njia pekee salama ni kuyafanya maombi yetu yamiminike kila siku kutoka katika moyo mnyofu, kama alivyofanya Daudi, “Zishikilie nyayo zangu katika njia Zako, ili hatua zangu zisiteleze” (Zaburi 17:5, NKJV).

No comments: