Thursday, April 13, 2017

ALIPOTEZA SUBIRA YAKE

"Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno” (Yakobo 1:4).

Bila kujali ukweli kuwa Musa alikuwa mwanadamu mpole zaidi miongoni mwa wanadamu walioishi usoni pa nchi, katika tukio mojawapo alijiletea ghadhabu ya Mungu….
Shutuma za watu zilizompata na asizozistahili, zilimfanya kwa muda kitambo asahau kwamba manung’uniko yao hayakuwa juu yake, bali dhidi ya Mungu; na badala ya kuhuzunika kwa sababu Roho wa Mungu alikuwa akitukanwa, alikasirishwa, akachukizwa, na katika namna ya ushupavu na pupa, aliupiga ule mwamba mara mbili akisema: “Sikieni sasa, enyi waasi; je! Tuwatokezee maji katika mwamba huu?”…
Musa alidhihirisha udhaifu mkuu mbele ya watu. Alionesha bayana kukosa kujitawala, roho inayofanana na ile waliyokuwa nayo wale wanung’unikaji. Angelipaswa kuonesha mfano wa ustahimilivu na saburi mbele ya umati huo, waliokuwa tayari kujipatia udhuru wa makosa yao, chuki, na manung’uniko yasiyokuwa na maana, kwa ajili ya udhihirisho wa kosa hili kwa upande wake.
Dhambi kubwa kabisa ilikuwa kujitwalia nafasi ya Mungu. Nafasi ya heshima ambayo Musa alikuwa ameshikilia hadi hapa haikuhafifisha hatia yake, bali iliikuza zaidi. Mpaka hapa alikuwa mtu asiyekuwa na hatia, lakini sasa ameanguka. Wengi katika nyadhifa za namna hiyo wangeweza kudhani kwamba dhambi yao ingesamehewa kwa sababu ya maisha yao ya muda mrefu ya uaminifu usioyumba.
Lakini hapana; lilikuwa ni jambo baya kabisa kwa mtu ambaye alikuwa ameheshimiwa na Mungu kuonesha udhaifu wa kitabia katika kudhihirisha hisia ya hasira kali kuliko kama vile ambavyo angelikuwa na wadhifa mwingine wa madaraka chini ya hapo. Musa alikuwa mwakilishi wa Kristo, lakini inahuzunisha kiasi gani jinsi taswira hiyo ilivyoharibiwa! Musa alikuwa ametenda dhambi, na uaminifu wake uliopita usingeweza kumponya katika dhambi ya sasa….
Musa na Haruni wafe bila kuingia Kanaani, wakabiliwe na adhabu ileile iliyowapata wale waliokuwa katika nyadhifa za chini. Walisujudia katika kujisalimisha, ingawa kwa uchungu wa moyo ambao haukuelezeka; lakini upendo wao na imani yao kwa Mungu havikutikiswa…. Lakini ni wachache wanaotambua ubaya wa dhambi…. Uzoefu wa Musa na Haruni… huonesha kwamba siyo jambo salama kutenda dhambi katika neno au wazo au tendo.

"Rehema za Bwana ni mpya kila siku asubuhi.”
(Maombolezo 3:22, 23).

No comments: