“Wakamghadhibisha penye maji ya Meriba, Hasara ikampata Musa kwa
ajili yao, Kwa sababu waliiasi roho yake, Akasema yasiyofaa kwa midomo
yake”
(Zaburi 106:32, 33).
(Zaburi 106:32, 33).
Kama Musa na Haruni wangelikuwa wanaendekeza hali ya kujistahi au
kuendekeza roho ya hasira licha ya onyo na karipio la Mungu, hatia yao
ingelikuwa kubwa sana. Lakini hawakuwa na hatia ya dhambi ya kukusudia
au kudhamiria; walikuwa wameangushwa na jaribu la ghafla, na majuto yao
yalifanyika mara moja, tena toka moyoni. Bwana aliikubali toba yao,
ingawa kwa sababu ya madhara ambayo dhambi yao ingeliweza kuyasababisha
miongoni mwa watu, asingeliweza kufutilia mbali adhabu hiyo…..
Mungu alikuwa amewasamehe watu maasi makubwa zaidi, lakini
asingeliweza kushughulikia dhambi ya viongozi hawa kama alivyofanya kwa
wale waliokuwa wakiongozwa. Alikuwa amempatia Musa nafasi ya heshima
kubwa kuliko mwanadamu yeyote duniani…. Ukweli kwamba Musa alikuwa
amepata nuru na maarifa makubwa kiasi hicho uliifanya dhambi yake kuwa
mbaya zaidi. Uaminifu wa wakati uliopita hautaweza kuwa udhuru wa
kusamehe kosa hata moja. Kadiri nuru na fursa anazopewa mwanadamu
zinapokuwa kubwa zaidi, ndivyo pia wajibu wake unavyokuwa mkubwa zaidi,
kadiri kosa lake linavyokuwa baya zaidi, na pia ndivyo adhabu yake huwa
kali zaidi..
Musa hakuwa na hatia ya kufanya uovu mkubwa,
kama ambavyo watu wanaweza kuliangalia suala hili…. Lakini endapo Mungu
alishughulikia dhambi hii vikali sana kiasi hicho kwa mtumishi wake huyu
mwaminifu na aliyeheshimiwa kuliko wote, hatawezi kuipuuzia dhambi kwa
wengine…. Wote wanaodai kuwa wacha Mungu wako chini ya wajibu mtakatifu
sana wa kulinda roho zao, na kujitawala wanapokabiliwa na uchokozi
mkubwa zaidi. Wajibu uliowekwa juu ya Musa ulikuwa mkuu sana; ni
wanadamu wachache ndio watakaojaribiwa kama ilivyokuwa kwake; hata hivyo
hili halikuruhusiwa kuwa udhuru wa kupuuzia dhambi yake. Mungu aliandaa
mpango wa kutosha kwa ajili ya watu Wake; na kama wakitumainia nguvu
zake, kamwe hawataweza kuwa wahanga wa mazingira. Jaribu zito sana
kuliko yote haliwezi kuwa udhuru wa dhambi. Hata kama shinikizo
lililoletwa ili kuikabili roho litakuwa kubwa kiasi gani, uasi ni tendo
letu sisi wenyewe. Haipo katika nguvu ya dunia wala jehanamu
kumshurutisha yeyote kutenda uovu. Shetani anatushambulia katika maeneo
yale ambayo tu dhaifu, lakini hatupaswi kushindwa. Hata kama shambulizi
ni kali au lisilotarajiwa kiasi gani, Mungu ametupatia msaada, na katika
uwezo wake tunaweza kushinda.
No comments:
Post a Comment