Sunday, April 23, 2017

MSAIDIZI ASIYEONEKANA

“Hapatakuwa mtu yeyote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha”(Yoshua 1:5).

Jifunze kwa kina uzoefu wa Israeli katika safari zao kuelekea Kanaani…. Tunahitaji kudumisha moyo na akili katika mafunzo, kwa kurejesha upya kumbukumbu ya masomo ambayo Bwana aliwafundisha watu wake wa zamani. Na hivyo, kama alivyokusudia iwe kwao, mafundisho ya Neno lake yataendelea daima kutuvutia na kuwa na mguso wa pekee kwetu.

Yoshua alipoondoka asubuhi kabla ya kuuhusuru Mji wa Yeriko, palitokea mbele yake shujaa aliyekuwa amejiandaa tayari kabisa kwa ajili ya vita. Na Yoshua akauliza, “Je! Wewe u upande wetu, au upande wa adui zetu? Naye akajibu, La, lakini nimekuja sasa, nili Amiri wa jeshi la Bwana. Kama macho ya Yoshua yangalikuwa yamefumbuliwa kwa jinsi ile ambayo mtumishi wa Elisha alifumbuliwa pale Dothani, na kama angaliweza kustahimili tukio hilo, angaliweza kuwaona malaika wa Bwana wakiwa wamewazunguka wana wa Israeli; kwa maana jeshi imara la mbinguni lilikuwa limekuja ili kupigana kwa niaba ya watu wa Mungu, na Kapteni wa jeshi la Bwana alikuwa hapo ili kuongoza. Yeriko ilipoanguka, hakuna mkono wowote wa mwanadamu uliogusa hizo kuta za mji, kwa maana malaika wa Bwana waliziangusha ngome zake, na kuingia ndani ya maboma hayo ya adui. Hawakuwa Israeli, bali Yule Kapteni wa jeshi la Bwana ndiye aliyeiporomosha na kuitwaa Yeriko. Lakini Israeli ilikuwa na sehemu yake ya kutenda ili kuonesha imani yao kwa Kapteni wa wokovu wao.

Vita vinapaswa kupiganwa kila siku. Pambano kuu linaendelea ndani ya kila roho, kati ya mkuu wa giza na Mkuu za uzima…. Kama mawakala wa Mungu ni sharti mjisalimishe chini Yake, ili aweze kupanga na kuelekeza na kupigana vita kwa ajili yenu, mkishirikiana Naye. Mkuu wa uzima ndiye anayeongoza kazi Yake. Anapaswa kuwa pamoja nanyi katika vita vyenu vya kila siku dhidi ya nafsi, ili mweze kuwa waaminifu na watiifu kwa kanuni; ili tamaa ya mwili, inapopambana ili kutawala, iweze kutiishwa kwa njia ya neema ya Kristo; ili mweze kujitokeza mkiwa zaidi ya washindi kupitia Kwake ambaye ametupenda. 

Yesu amekuwa kwenye eneo hasa la vita. Anajua nguvu ya kila jaribu. Anajua kabisa jinsi ya kukabiliana na kila dharura, na jinsi ya kukuongoza kupitia kila njia ya hatari. Kwa hiyo, kwa nini usimtumaini Yeye?

No comments: