Kwa kawaida watu hupenda kile kinachowaongezea furaha au faida
fulani. Ni vigumu kwa binadamu kupenda kisichomvutia na kinachomtia
hasara au kumpenda kiumbe aliyejitangaza mwenyewe kuwa adui. “Bali Mungu
aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa
kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.” (Warumi 5:8) Tangu
dhambi ilipoingia duniani, sisi wanadamu tumekuwa adui wa Mungu.
Tumekuwa tukimkimbia Mungu kila anapotusogelea. “Bwana Mungu akamwita
Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini,
nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha.” (Mwanzo 3:9-10)
Maagizo ya Mungu yamejenga uadui nafsini mwetu. “Kwa kuwa ile nia ya
mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala
haiwezi kuitii.” (Warumi 8:7) Hali hiyo ilipelekea maisha kuwa yasiyo
na amani jambo lililohitaji uingiliaji kati wa haraka. Mungu aliuondoa
uadui huo kwa kifo cha Yesu pale msalabani. “Akiisha kuifuta ile hati
iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu;
akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na
mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika
msalaba huo.” (Wakolosai 2:14-15)
Upendo huu wa kuwapenda rafiki
zako ambao bado wanakuchukulia kuwa ni adui yao unapatikana kwa Mungu
pekee. “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai
wake kwa ajili ya rafiki zake.” (Yohana 15:13) Upendo huu hauangalii
kama anayependwa ataitikia upendo huo na kukubali kurejeshwa kwa
mahusiano ama ataendelea na dhana yake ya uadui. Upendo ulio tayari
kutoa uhai kwa ajili ya wengine. Mungu hatupendi kwa matarajio kuwa
tutampenda. Anawapenda wote wema kwa wabaya na angependa nasi tupendane
kwa bila kubagua. “Ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni;
maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye
haki na wasio haki.” (Mathayo 5:45)
Upendo wa Mungu ni tabia yake
ambayo haitegemei mazingira. “Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu
kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo,
hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake.” (1 Yohana 4:16).
Upendo wa kibinadamu ungekuwa kama ule wa Mungu ungekuwa haulazimishwi
na faida utakazozipata kwa unayempenda. Tabia yetu ya upendo ungejengwa
juu uthamani wa kila kiumbe kilichoumbwa na Mungu na wala si mwonekano
wa nje tu wa viumbe hivyo, tusingeshuhudia unyanyapaa uliopo. “Maana
mkiwapenda wale wawapendao ninyi, mwaonyesha fadhili gani? Kwa kuwa hata
wenye dhambi huwapenda wale wawapendao.” (Luka 6:32)
Mwanadamu
ni kiumbe anayestahili kupendwa kwa sababu kuu mbili. Anastahili
kupendwa kwa sababu aliumbwa katika viwango vya juu vya ubora. “Mtu ni
kitu gani hata umkumbuke, Na binadamu hata umwangalie? Umemfanya mdogo
punde kuliko Mungu; Umemvika taji ya utukufu na heshima.” (Zaburi 8:4-5)
Mwanadamu amefanyika katika viwango vya ubora ulio chini kidogo ya ule
wa Mungu. “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu;
wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi
yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.” (Mwanzo
1:26)
Sababu ya pili kwa nini mwanadamu ni wa thamani na
anayestahili kupendwa ni ule ukweli kuwa alikombolewa kwa thamani kubwa
kuliko thamani zote za duniani na mbinguni. “Nanyi mfahamu kwamba
mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate
kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa
damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani,
ya Kristo.” (1 Petro 1:18-19). Amgusaye mwanadamu ni sawa na yule
aigusaye mboni ya jicho la Mungu. “Kwa maana Bwana wa majeshi asema
hivi, Ili nitafute utukufu amenituma kwa mataifa wale waliowateka ninyi;
maana yeye awagusaye ninyi aigusa mboni ya jicho lake.” (Zekaria 2:8)
Mungu anatualika kujifunza upendo wake mkuu kwa wanadamu. “Kristo akae
mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili
mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu,
na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi
ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu.” (Waefeso
3:17-19) Mungu anatupenda tulivyo.
No comments:
Post a Comment