“Wakiiacha njia iliyonyoka, wakapotea, wakiifuata njia ya
Balaamu, mwana wa Beori, mtu ambaye hakuwa na kipingamizi chochote kwa
uovu ilimradi ungelimpatia ujira” (2 Petro 2:15, Fasiri ya Phillips).
Wakati fulani Balaamu alikuwa mtu mwema na pia nabii wa Mungu;
lakini sasa alikuwa ameasi, na alikuwa amejiingiza katika tamaa; hata
hivyo bado alidai kuwa mtumishi wa Mungu Mkuu. Hakuwa mtu asiyejua
utendaji wa Mungu kwa ajili ya Israeli; na wale wajumbe
walipomweleza ujumbe waliokuja nao, alifahamu vyema kuwa ulikuwa wajibu
wake kukataa zawadi za Balaki na kuwaondosha hao mabalozi. Lakini
alithubutu kuchezacheza na majaribu, akawahimiza wajumbe hao wakae
pamoja naye usiku huo, huku akitamka kuwa asingeliweza kutoa jibu lolote
la hakika hadi atakapokuwa ameomba mashauri ya Bwana. Balaamu alijua
kuwa laana yake isingeweza kuwadhuru Israeli. Mungu alikuwa katika
upande wao, na kadiri walivyodumu kuwa waaminifu Kwake hakuna uwezo
wowote mwovu wa kidunia au jehanamu ambao ungeweza kuwashinda. Lakini
kiburi chake kilidanganywa kwa maneno ya wale wajumbe, “Yeye umbarikiye
hubarikiwa, na yeye umlaaniye hulaaniwa.” Rushwa ya zawadi za thamani na
matarajio ya kutukuzwa viliamsha tamaa yake. Alikubali kwa ulafi hazina
zilizoahidiwa kwake, na kisha, wakati akidai kuwa mtii kamili kwa
mapenzi ya Mungu, alijaribu kukubaliana na matakwa ya Balaki….
Dhambi ya tamaa ya mali, ambayo Mungu anaitaja kama ibada ya
sanamu, ilikuwa imemfanya kuwa mhanga wa mazingira, na kupitia kosa hili
moja Shetani alipata nafasi ya kumtawala kabisa. Hili ndilo
lililosababishia uangamivu wake. Daima yule mjaribu anaendelea
kuwasilisha manufaa na heshima za kiulimwengu ili kuwashawishi watu
waache utumishi wa kazi ya Mungu. Anawaambia kwamba uangalifu wao
uliopita kiasi ndio unaowazuia wasipate mafanikio. Kwa namna hiyo wengi
wanashawishika ili kuthubutu kutoka kwenye njia ya uadilifu kamili.
Hatua moja mbaya huifanya nyingine kuwa rahisi zaidi, na huendelea kuwa
na ufidhuli zaidi na zaidi. Watafanya na kuthubutu mambo ya kutisha sana
mara wanapokuwa wamejiingiza mara moja chini cha utawala wa ulafi na
tamaa ya ukuu. Wengi hujidanganya kwamba wanaweza kutoka kwenye uadilifu
kamili kwa muda fulani,… na baada ya kufanikisha lengo lao, wanaweza
kubadilisha mwenendo wao wakati watakapoona kuwa vyema. Watu wa namna
hiyo wanajifunga wenyewe katika mtego wa Shetani, na ni kwa nadra kwamba
watajinasua.
No comments:
Post a Comment