Saturday, April 29, 2017

GHARAMA YA UONGO

"Midomo ya uongo ni chukizo kwa Bwana; Bali watendao uaminifu ndio furaha yake" (Mithali 12:22)
 
Kutoka Shekemu, wana wa Israeli walirejea katika kambi lao huko Gilgali. Muda si mrefu walipokuwa hapa walitembelewa na wajumbe wa ajabu, waliotamani kufanya mkataba pamoja nao. Mabalozi hawa walieleza kuwa walitokea nchi ya mbali, na hili lilionekana kuthibitishwa na hali ya mwonekano wao. Mavazi yao yalikuwa makuukuu na yalikuwa yameraruka, viatu vyao vilikuwa vimetobokatoboka, chakula chao kilikuwa kimekauka na kuvunda, na vibuyu vyao vya mvinyo vilikuwa vikuukuu vilivyorarukararuka na kutiwa viraka, kana kwamba vilirekebishwa haraka njiani wakiwa safarini…. Mionekano hii ilifanikiwa kuwashawishi wenyeji…. “Naye Yoshua akafanya amani pamoja nao, na kufanya agano nao, ili kwamba waachwe hai; na wakuu wa mkutano wakawaapia.” Hivyo ndivyo mkataba huu ulivyofanyika….
 
Lakini mambo yangeliwaendea vyema Wagibeoni endapo wangezu-ngumza na Israeli kwa uaminifu. Wakati ambapo kujinyenyekesha kwao na kumfuata Yehova kuliwapatia ulinzi wa maisha yao, udanganyifu wao uliwaletea fedheha na utumwa. Mungu alikuwa ameandaa mpango kwamba wote ambao wangeukana upagani, na kujifungamanisha na Israeli, wangeshiriki baraka za agano lake. Walihusishwa kwa namna hiyo katika masharti yaliyosema, “mgeni akaaye kati yenu,” na isipokuwa mambo mengine machache, wageni hawa walipaswa kupata fadhila na fursa sawa na Israeli. Maelekezo ya Bwana yalikuwa—“Na mgeni akikaa pamoja nawe katika nchi yako, usimdhulumu. Mgeni akaaye pamoja nawe atakuwa kama mzalia kwenu; mpende kama nafsi yako; kwa maana ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri; Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu” (Law. 19:33, 34).
 
Hayo ndiyo masharti ambayo kwayo Wagibeoni wangeliweza kupokelewa, kama isingelikuwa ule udanganyifu ambao walikuwa wameutumia. Haikuwa fedheha ndogo kwa raia hao wa “miji ya kifalme,” “tena watu wake wote walikuwa ni mashujaa,” kuwa wapasua-kuni, na wateka-maji kwa ajili ya Israeli wakati wote. Lakini walikuwa wamejitwalia vazi la umaskini kwa ajili ya kusudi la udanganyifu, na lilifungamanishwa juu yao kama nembo ya utumwa wa kudumu. Kwa hiyo katika vizazi vyao vyote hali yao ya utumwa ingeliweza kushuhudia chuki ya Mungu dhidi ya udanganyifu.

Sunday, April 23, 2017

KIZAZI KIPYA!!

Ni dhahiri kweli kizazi kipya kinazidi kuwa na nguvu sana miongoni mwetu hasa miaka ya hivi karibuni, wamekuwa na Television zao, radio zao na kumbi mbalimbali kwa ajili ya matamasha yao mbali mbali.
 
Je umewahi kujiuliza nyuma ya kizazi kipya pamoja na style mbali mbali za uimbaji, mavazi na aina ya maisha waishiyo nani aongozaye????
Leo nitapenda kuongelea aina ya maisha ya kizazi kipya kupitia style mpya ya uvaaji wa vazi la jeans kama wengi walijuavyo japo yako mengi hayo tutazidi kuyaongea kadri Mungu atupatiavyo pumzi ya uhai.

Miaka ya nyuma hasa miaka ya 80 na 90 hapo tulizoea kuwaona watoto ama watu wavaao nguo zilizopasuka matakoni ama magotini ni jamii ya watu maskini sana, lakini leo hizo nguo huvaliwa na watu matajiri sana tena imekuwa kama fasion siku hizi kina kaka na dada uzivaa sana....
Sikia ndugu yangu Shetani ni adui wa mwanadamu amejifunza mbinu nyingi sana na namna ya kukamata mioyo ya watu na kuiongoza apendapo kwa kutumia wasanii na watu maarufu amefanikisha kukamata akili za vijana na wazee wengi nao uiga aina fulani ya maisha ama mavazi kupitia wasanii maarufu huo ni mtego wa adui kuongoza watu kwa siri bila kujua.
Uvaaji huu wa hizi nguo zilizotoboka kwanza zinakushusha heshima na kukuweka mvaaji katika viwango vya chini vya kitabia, pili kwa madada zetu wazivaapo uachia sehemu baadhi ya viungo vyao kuwa wazi kama mapaja na sehemu zingine za siri ambazo hakupaswa mwanamme mwingine kumuona isipokuwa mume wake, kwa njia hiyo Shetani amefanikisha kuwafanya madada wengi kuwa mabango ya kuwafanya wanaume kuingia kwenye tamaa ya ngono kwa aina ya hizo nguo hivyo si salama kwa wale wampendao Mungu kuzivaa....

Television ama runinga.... Shughuli zetu huathiri IQ na EQ zetu. Kadri tunavyoangalia burudani ktk runinga, ndivyo ubunifu unavyoshuka pamoja na alama ktk mitihani. Pamoja na hayo, hushindwa kudhibiti mihemko - pamoja na hayo huwa kuna ongezeko la uhalifu wa kutumia nguvu na wa ngono. Mtandao ya burudani, video na michezo ya video pia vina athari hasi. Kama alivyosema Mtume Paulo; huwa tunabadilishwa kwa kuona. (soma 2 Wakorintho 3:18).

Tuko vitani na uwanja wa mapambano ni ndani ya mioyo yetu ruhusu Roho Mtakatifu akuongoze soma sana neno la Mungu hapo ndipo salama yetu ilipo...


MSAIDIZI ASIYEONEKANA

“Hapatakuwa mtu yeyote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha”(Yoshua 1:5).

Jifunze kwa kina uzoefu wa Israeli katika safari zao kuelekea Kanaani…. Tunahitaji kudumisha moyo na akili katika mafunzo, kwa kurejesha upya kumbukumbu ya masomo ambayo Bwana aliwafundisha watu wake wa zamani. Na hivyo, kama alivyokusudia iwe kwao, mafundisho ya Neno lake yataendelea daima kutuvutia na kuwa na mguso wa pekee kwetu.

Yoshua alipoondoka asubuhi kabla ya kuuhusuru Mji wa Yeriko, palitokea mbele yake shujaa aliyekuwa amejiandaa tayari kabisa kwa ajili ya vita. Na Yoshua akauliza, “Je! Wewe u upande wetu, au upande wa adui zetu? Naye akajibu, La, lakini nimekuja sasa, nili Amiri wa jeshi la Bwana. Kama macho ya Yoshua yangalikuwa yamefumbuliwa kwa jinsi ile ambayo mtumishi wa Elisha alifumbuliwa pale Dothani, na kama angaliweza kustahimili tukio hilo, angaliweza kuwaona malaika wa Bwana wakiwa wamewazunguka wana wa Israeli; kwa maana jeshi imara la mbinguni lilikuwa limekuja ili kupigana kwa niaba ya watu wa Mungu, na Kapteni wa jeshi la Bwana alikuwa hapo ili kuongoza. Yeriko ilipoanguka, hakuna mkono wowote wa mwanadamu uliogusa hizo kuta za mji, kwa maana malaika wa Bwana waliziangusha ngome zake, na kuingia ndani ya maboma hayo ya adui. Hawakuwa Israeli, bali Yule Kapteni wa jeshi la Bwana ndiye aliyeiporomosha na kuitwaa Yeriko. Lakini Israeli ilikuwa na sehemu yake ya kutenda ili kuonesha imani yao kwa Kapteni wa wokovu wao.

Vita vinapaswa kupiganwa kila siku. Pambano kuu linaendelea ndani ya kila roho, kati ya mkuu wa giza na Mkuu za uzima…. Kama mawakala wa Mungu ni sharti mjisalimishe chini Yake, ili aweze kupanga na kuelekeza na kupigana vita kwa ajili yenu, mkishirikiana Naye. Mkuu wa uzima ndiye anayeongoza kazi Yake. Anapaswa kuwa pamoja nanyi katika vita vyenu vya kila siku dhidi ya nafsi, ili mweze kuwa waaminifu na watiifu kwa kanuni; ili tamaa ya mwili, inapopambana ili kutawala, iweze kutiishwa kwa njia ya neema ya Kristo; ili mweze kujitokeza mkiwa zaidi ya washindi kupitia Kwake ambaye ametupenda. 

Yesu amekuwa kwenye eneo hasa la vita. Anajua nguvu ya kila jaribu. Anajua kabisa jinsi ya kukabiliana na kila dharura, na jinsi ya kukuongoza kupitia kila njia ya hatari. Kwa hiyo, kwa nini usimtumaini Yeye?

Friday, April 21, 2017

MAMBO YANAYOONDOA FAHAMU ZA MWANADAMU:

"Imeandikwa hivii; "Uzinzi na Divai na Divai mpya huondoa fahamu za mwanadamu" Hosea 4:11.
 
Dhambi ya uzinzi licha ya kwamba sio uzinzi peke yake utakaowakosesha wengi wasiingie mbinguni; lakini neno la Mungu limeizungumza kwa uchungu madhara yake kama mwanadamu angeliielewa. Paulo katika Wakorintho pia alisema mtu akizini msichangamane naye na kwa baadhi ya makanisa mtu anayefumwa katika uzinzi huondolewa katika ushirika wa kanisa. Dhambi hii ni kweli ni sawa tu na dhambi zingine; lakini imetajwa katika dhambi kuu mbili zinazoondoa fahamu za mwanadamu.
 
Biblia inaelewa kwa uwazi kupitia nabii Hosea kwamba Uzinzi na Divai huundoa fahamu za mwanadamu. Mtumishi wa Mungu Sulemani ingawa aliandika yeye mwenyewe katika Kitabu cha Mithali kwamba; "Mtu aziniye na mwanamke hana akili, afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake" Bado kama mwanadamu anayo historia ya kutenda kosa hilo kwa kuoa akina mama 700+300 masuria jumla akawa na 1,000 wake wa kulala nao kimapenzi.
 
Uzinzi na ulevi ni dhambi kuu zinazovuma na zimeshika nafasi ya kwanza katika ulimwengu wa sasa. Wachungaji, mapadre, maaskofu, watumishi wengi wa Mungu, wainjilisti, wahubiri, na waumini wa madhehebu mbalimbali hatuko nyuma katika kujishughulisha na dhambi ya uzinzi na ulevi( Divai) ingawa dhambi ni dhambi bila kujali ni uongo, majungu, masengenyo, wizi wa zaka, ulawiti, ubakaji, uchonganishi, dharau, kiburi, majivuno na kiola aina ya ubaya unaomwandama mwanadamu; ila katika kuondoa ufahamu wa mwanadamu (yaani anakuwa punguwani asiyejielewa kiroho na kuwa mtumwa wa uovu huo) ni Uzinzi na ulevi kama asemavyo Mungu kupitia nabii Hosea, na mtume Paulo.
 
Angalia mtu akilewa anavyokosa adabu, asivyojiheshimu, anavyopiga kelele, anavyosumbua mke au mme wake, anavyotishia watu, anavyopiga mke, anavyopiga mume, anavyopiga watoto! Je, ulevi na kunywa japo kidogo mbele za Mungu ni halali? imeandikwa nini katika Isaya 28:7? ni kosa kumpa mtu kileo. Katika Biblia yaani maandiko matakatifu hakuna fungu linalosema kunywa kidogo ila usilewe, halipo ila ni fundisho miongoni mwa mafundisho ya shetani kwamba watu wanywe kidogo ila wasilewe!
 
Niliwahi kuona mtu mmoja aliyejiita mtumishi wa Mungu akiwa amevalia kanzu akienda katika tukio la ujenzi wa makaburi akawa akizibariki pombe! wakati huo nikiwa gizani kama yeye niliona ni jambo jema; baada ya kupata mafunuo ya Mungu kupitia neno lake nikagundua yule alikuwa mtumishi wa shetani aliyevaa kanzu ya kondoo.
Ulevi umekatazwa kabisa; wapendwa wakristo wenzangu; Uzinzi na ulevi tumwombe Mungu atusaidie dhambi hizi zinaondoa fahamu za mwanadamu; na ujue ya kwamba Fahamu za mtu zikiondoka mtu huyo huitwa mwendawazimu. Soma tena Hosea 4:11 ujue mambo yanayoondoa fahamu za mwanadamu. Mungu halazimishi, ila anaonya ili isiwe siku ya kutupwa katika ziwa la moto ukamlaumu kwamba hukumu zake si za haki. Ni lazima siku zote Mungu aonye ukatae ili siku ya hukumu maneno yaleyale uliyoyakataa yawe sheria mbele zake ya kukugeuka. Amua leo kumtii Mungu katika kila jambo ili uwe salama. Haleluya!

Tuesday, April 18, 2017

WAWILI WANAOFANANA

“Jihadharini na kila aina ya tamaa; maana uhai wa mtu hautegemei wingi wa vitu alivyo navyo”
(Luka 12:15, Biblia Habari Njema)..

Laana ambayo Balaamu hakuwa ameruhusiwa kuitamka dhidi ya watu wa Mungu, hatimaye alifanikiwa kuwasababishia kwa kuwashawishi waingie dhambini..
Balaamu alishuhudia mafanikio ya njama zake za kishetani. Aliona laana ya Mungu ikipatilizwa kwa watu Wake, na maelfu wakianguka chini ya hukumu Zake; lakini haki ya Mungu iliyoadhimu dhambi katika Israeli haikuwaruhusu wale wajaribu kusalimika. Katika vita Israeli ya dhidi ya Wamidiani, Balaamu aliuawa kwa upanga….
Mauti ya Balaamu yalikuwa yanafanana na yale ya Yuda, na tabia zao hubeba ufanano bayana kabisa wa mmoja kwa mwenzake. Watu hawa wawili walijaribu kuunganisha utumishi wa Mungu na mali, na wakashindwa vibaya sana. Balaamu alimkiri Mungu wa kweli, na akadai kumtumikia; Yuda alimwamini Yesu kama Masihi, na akaungana na wafuasi Wake. Lakini Balaamu alitafuta kuufanya utumishi wa Yehova kuwa kama njia ya kujipatia utajiri na heshima ya kidunia; na aliposhindwa katika hili, alijikwaa na kuanguka na akavunjika. Yuda alitegemea kwamba katika kujihusianisha na Kristo angejipatia mali na kupandishwa hadhi ya juu katika ufalme huo wa kiulimwengu, ambao, kama alivyoamini, Masihi alikuwa akielekea kuuanzisha. Kushindwa kutimia kwa matarajio yake kulimsukuma kwenda katika uasi na uangamivu. Balaamu na Yuda walikuwa wamepokea nuru kuu na walifurahia fadhila maalumu, lakini dhambi moja iliyoendekezwa iliharibu kabisa tabia yote na kusababisha uangamivu wao….
Dhambi moja ambayo mtu hataki kuiacha, kidogo kidogo, huhafifisha tabia, ikisababisha uwezo wake wote wa uadilifu kutawaliwa na shauku zake ovu. Kuondolewa kwa ulinzi mmoja toka katika dhamiri, uendekezaji wa tabia moja ya uovu, upuuziaji mmoja wa madai ya juu ya wajibu, huvunja ulinzi wa roho na humfungulia Shetani njia ya kuingia ndani na kutuongoza kwenye ukengeufu. Njia pekee salama ni kuyafanya maombi yetu yamiminike kila siku kutoka katika moyo mnyofu, kama alivyofanya Daudi, “Zishikilie nyayo zangu katika njia Zako, ili hatua zangu zisiteleze” (Zaburi 17:5, NKJV).

Monday, April 17, 2017

WAJIBU AU SHAUKU

“Bali mmebatilisha shauri Langu, Wala hamkutaka maonyo Yangu” (Mithali 1:25).

Wakati wa usiku malaika wa Mungu alimjia Balaamu akiwa na ujumbe, “Usiende pamoja nao; wala usiwalaani watu hawa, maana wamebarikiwa.”…
Kwa mara ya pili Balaamu alijaribiwa tena. Katika kujibu ushawishi wa wale wajumbe alidai kuwa makini na mwenye uadilifu mkubwa mno, akiwahakikishia kwamba hakuna kiasi chochote cha dhahabu na fedha ambacho kingeweza kumshawishi kwenda kinyume na mapenzi ya Mungu. Lakini alitafuta kukubaliana na ombi la mfalme huyo; na licha ya kwamba alikuwa amedhihirishiwa bayana mapenzi ya Mungu, aliwahimiza wale wajumbe wangoje, ili aweze kuulizia tena kwa Mungu; kana kwamba Yeye Asiye na Ukomo alikuwa mwanadamu, awezaye kughilibiwa.
Wakati wa usiku Bwana alimtokea Balaamu na kusema, «Kwa kuwa watu hawa wamekuja kukuita, enenda pamoja nao; lakini neno lile nitakalokuambia ndilo utakalolitenda, basi.» Huo ndio umbali ambao Bwana angeliweza kumruhusu Balaamu ayafuate mapenzi yake mwenyewe, kwa sababu alikuwa amedhamiria juu ya hilo. Hakutafuta kuyatenda mapenzi ya Mungu, bali alichagua njia yake mwenyewe, na kisha akajitahidi kujipatia kibali cha Bwana.

Wapo maelfu hivi leo wanaoenenda katika njia ya namna hiyo. Wasingeliweza kuwa na ugumu wowote wa kuuelewa wajibu wao kama ungelipatana na mielekeo yao. Umeleezwa bayana mbele yao katika Biblia au umeoneshwa waziwazi kwa mazingira na mawazoni. Lakini kwa sababu ushahidi huu hupingana na shauku na mielekeo yao mara kwa mara wanauweka pembeni na kuthubutu kumwendea Mungu ili kutafuta kujua wajibu wao. Kwa uangalifu mkubwa unaoonekana dhahiri wanaomba kwa muda mrefu na kwa bidii ili wapate nuru. Lakini Mungu hatadhihakiwa. Kwa kawaida huwaruhusu watu wa namna hiyo wafuate shauku zao wenyewe na kukabiliana na matokeo husika…. 

Mtu anapouona wajibu wake bayana, hebu asithubutu kumwendea Mungu akiwa na ombi kwamba asamehewe ili asiufanye. Badala yake anapaswa, kwa roho na unyenyekevu na kujisalimisha, aombe nguvu na hekima ya kimbingu ili kutimiza madai yake.

Sunday, April 16, 2017

MIPANGO YA AMANI NA MAANDALIZI YA VITA

Tunaishi katika ulimwengu huu wa ajabu. Kila mmoja anaafiki kwamba tungeipatia nafasi amani; lakini basi, zile chuki zilizokandamizwa kwa kipindi cha karne fulani zilizopita, zinalipuka na kuwa vita ya wazi. Nabii Mika na Yoeli walitabiri kwamba wakati ule ule mataifa yatakapokuwa yanasema juu ya shauku yao ya kuwa na amani (Mika 4:1-3) WATALAZIMIKA KUJIANDAA KWA VITA...kutokana na shauku yao waliyo nayo dhidi ya majirani zao (Yoeli 3:9-13).....

Marekani imefanya shambulizi la makombora takriban 50 ,yalipigwa katika kambi ya jeshi la anga mjini Homs nchini Syria.
Awali maafisa wa Marekani walisema wana mpango wa kuchukua hatua za kijeshi baada ya Syria kushutumiwa kutumia silaha za kemikali katika mji unaodhibitiwa na waasi, ambapo watu kadhaa wamepoteza maisha.Rais wa Marekani Donald Trump amesema ameamuru kutekelezwa kwa mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Syria huku akitoa wito kwa mataifa yote yaliyostaarabika kukomesha vitendo vya mauaji na umwagaji damu nchini humo
URUSI YACHUKIZWA NA MAREKANI KUISHAMBULIA SYRIA
Urusi imechukizwa na uamuzi wa Marekani wa kuishambulia kambi ya jeshi la anga mjini Homs nchini Syria kwa makombora.Urusi inaunga mkono serikali ya Rais Bashar al-Assad[SYRIA] na imekashifu shambulizi hilo ambalo linadaiwa kuua watu sita.

CHINA,KOREA KUSINI zimeionya kuiadhibu Pyongyang iwapo itarusha kombora lolote
Mataifa mawili ya bara Asia, yametoa onyo kali dhidi ya utawala wa Pyongyang, kwamba itaadhibiwa vikali, iwapo itadhubutu tena kufanyia majaribio zana zake za kinuklia.

Mataifa hayo, Korea Kusini na China, yamekiri kuchukua hatua kali dhidi ya Korea Kaskazini, ikiwa tena itafanyia majaribio zana zake za kitonoradi zinazovuka mipaka ya kimataifa.

MAREKANI YATISHIA kuiadhibu Korea KaskaziniTrump: "tutaidhibiti Korea Kaskazini".." HATUTAIVUMILIA KOREA KASKAZINI"
Rais Trump amesema kuwa Marekani imejiandaa kibinafsi kukabiliana na tishio la nyuklia linaloletwa na Korea Kaskazini.
KOREA KASKAZINI : Tutatumia ''silaha kali'' kujilinda dhidi ya US

Korea Kaskazini imesema kuwa itajitetea kwa kutumia silaha kali ili kujibu hatua ya Marekani kupeleka wanamaji wake katika rasi ya Korea.
Wizara ya maswala ya kigeni ilinukuu shirika la habari la serikali KCNA lililosema kuwa hatua hiyo ya Marekani inaonyesha uvamizi wa kijinga uliofika awamu yenye hatari kubwa.

Jeshi la Marekani katika maeneo ya Pacific limesema kuwa hatua hiyo inalenga kuonyesha Marekani imejiandaa kwa lolote lile.
Zamani sana Biblia ilionyesha picha hii ya mgogoro wetu wa sasa wa kuwa na AMANI au VITA, kisha ikatangaza kwamba amani ya kudumu itatawala katika dunia hii wakati ule tu YESU ATAKAPOKUJA.

Nanyi mtasikia habari za vita na matetesi ya vita; angalieni, msitishwe; maana hayo hayana budi kutukia; lakini ule mwisho bado.
- Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na njaa, na matetemeko ya nchi mahali mahali.Mathayo 24 :6- 7
Luka 21 : 28 - Basi mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia.

IJUE VIZURI PASAKA, USITEKWE NA DUNIA

Basi, kabla ya sikukuu ya pasaka ,Yesu,hali akijua kwamba saa yake imefika,atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba,naye amewapenda watu wake katika ulimwengu,aliwapenda upeo,Yesu hali akijua ya kwamba Baba amempa vyote mikononi mwake,na ya kuwa anatoka kwa Mungu naye anakwenda kwa Mungu,aliondoka chakulani,akaweka kando mavazi yake,akatwaa, kitambaa akajifunga kiunoni.Kisha akatia majia katika bakuli,akaanza kuwatawadha miguu na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga….Basi alipokwisha kuwatawadha miguu, na kuyatwaa mavazi yake, na kuketi tena,akawaambia, Je! Mmeelewa na hayo niliyowatendea? Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu,nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo KUTAWADHANA miguu ninyi kwa ninyi...Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo. YOHANA 13:1-151

Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate,Naye akiisha kushukuru akaumega, akasema,Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa UKUMBUSHO wangu. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa UKUMBUSHO wangu. Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, MWAITANGAZA MAUTI YA BWANA HATA AJAPO WAKORINTHO 11:23-26
KUHUSU (EASTER)?

Easter Ni sherehe inayojulikana sana ambayo,inaadhimishwa na makanisa yetu ya siku hizi. Walakini hii pia ilisherehekewa na wapagani muda mrefu kabla ya ufufuo wa Kristo.
Siku zote Pasaka inaangukia Jumapili ya kwanza baada ya mwezi mpevu (full moon) mara tu baada ya jua kuwa kichwani kaskazini ya Ikweta (Equinox ---March 2l).Wapagani wale wa zamani za kale waligundua ya kwamba kila kitu kilionekana kupata uzima mpya mapema katika majira yale ya kuchipua (Spring), mara tu baada ya jua kupita mstari wa ikwinoksi (equinox) kaskazini ya Ikweta. Basi wakachagua siku moja katika majira ya kuchipua [Machi, Aprili, Mei] ili KUMHESHIMU mungu WA KIKE WA UZAZI. Siku ile ikatolewa kwa ISHTA (ISHTAR), mungu wa kike wa uzazi, kwa sababu ya uhai mpya na kukua kwa mimea ya asili.

Neno lilo hilo ISTA (EASTER) limeandikwa kwa herufi nyingine zisizokuwa za lugha yenyewe kutokana na jina la mungu huyo wa kike ISHTA (ISHTAR), ambaye ibada yake iliwekewa ukumbusho wake kwa kutumia sikukuu ya Ista (Easter) [Pasaka]. Mara nyingi Wakristo walei [wa kawaida] wameuliza ya kwamba ule mkate mdogo kama sungura (bunny rabbit) na yai la Ista (Easter egg) vina uhusiano gani na ufufuo wa Kristo. Kusema kweli, havina uhusiano wo wote na [ufufuo] huo. Sungura alichaguliwa kwa sababu alikuwa anazaa sana. Yai pia lilichaguliwa kwa sababu lilikuwa nembo ya kuzaa sana. Hata nembo hizo zenyewe, mkate mdogo kama sungura na mayai, vinatunzwa kama ukumbusho wa asili yake ya kipagani [ya siku hiyo]. Mifano hii imetolewa ili kuonyesha tu jinsi ilivyokuwa rahisi kwa Mwovu kulazimisha mawazo yale ya kipagani juu ya kanisa lile. Swali linakuja mawazoni mwetu, Hivi ni kweli tunaifuata Biblia katika mafundisho yetu yote ya dini? Iwapo MAPOKEO na DESTURI za kipagani zimeweza kuteleza kwa urahisi na kuingia kanisani, ni vipi kuhusu mafundisho mengine ya dini?

Hatuna amri yo yote kuhusu uadhimishaji wa ufufuo au kuzaliwa kwa Kristo. Tunaweza kutafakari juu ya ufufuo Wake na kuzaliwa Kwake kwa wakati wo wote ule na katika siku yo yote ile ya mwaka. Macho yetu na yafumbuke ili tupate kuyatambua mafundisho hayo ya uongo na kuendelea kuwa watiifu kwa ile kweli halisi katika mfumo wake wa asilia.

TOKA KABURI HADI UTUKUFU

“Nikamnyenyekea Bwana wakati huo, nikamwambia,… Nami nakuomba nivuke, nikaione hiyo nchi nzuri iliyoko ng’ambo ya Yordani, mlima ule mzuri, na Lebanoni. Lakini Bwana alikuwa amenikasirikia kwa ajili yenu, asinisikize; Bwana akaniambia, Na ikutoshe, usinene nami zaidi jambo hili”
(Kumbukumbu 3:23-26).

Kamwe haikuwahi kutokea, hadi pale vilipodhihirishwa katika kafara ya Kristo, ndipo ambapo haki na upendo wa Mungu vilioneshwa kwa kiwango kikubwa sana kuliko katika kushughulika Kwake na Musa. Mungu alimzuia Musa asiingie Kanaani, ili afundishe somo ambalo kamwe halipaswi kusahaulika—kwamba Yeye anahitaji utii kamili, na kwamba wanadamu wanapaswa kujihadhari ili wasijitwalie utukufu unaomstahili Muumba wao. Asingeweza kujibu ombi la Musa aliposihi apewe nafasi ya kushiriki urithi wa Israeli, lakini Mungu hakumsahau wala kumwacha mtumishi Wake. Mungu wa mbinguni alielewa mateso ambayo Musa alikuwa ameyastahimili; alikuwa ametazama kila tendo la utumishi wenye uaminifu katika miaka hiyo yote ya mapambano na majaribu. Juu ya Mlima Pisga, Mungu alimwita Musa kuingia katika urithi mtukufu sana usio na ukomo ukilinganishwa na ule wa Kanaani ya duniani..

Katika ule mlima ambako Yesu alibadilikia sura, Musa alikuwepo pamoja na Eliya, waliokuwa wamehamishwa kwenda mbinguni. Walitumwa kama wabeba-nuru na utukufu kutoka kwa Baba hadi kwa Mwanawe. Kwa hiyo, dua ya Musa, iliyotamkwa karne nyingi hapo kabla, hatimaye ilijibiwa. Alisimama kwenye “mlima ule mzuri,” ndani ya urithi wa watu wake….

Musa alikuwa mfano wa Kristo…. Mungu aliona vyema kumfunza Musa katika shule ya mateso na umaskini kabla hajaandaliwa kuliongoza jeshi la Israeli hadi Kanaani ya duniani. Israeli wa Mungu, wanaosafiri kuelekea Kanaani ya mbinguni, wanaye Amri Jeshi asiyehitaji mafundisho ya wanadamu ili kumwandaa kwa ajili ya utume Wake kama kiongozi wa kimbingu; hata hivyo alikamilishwa kupitia mateso; na “kwa kuwa [Yesu] Mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa” (Ebr. 2:10, 18). Mkombozi wetu hakuonesha udhaifu au kasoro yoyote ya kibinadamu; hata hivyo alikufa ili kutununulia sisi urithi wa kuingia katika ile Nchi ya Ahadi.

“Na Musa kweli alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu kama mtumishi,… bali Kristo, kama mwana, juu ya nyumba ya Mungu; ambaye nyumba Yake ni sisi, kama tukishikamana sana na ujasiri wetu na fahari ya taraja letu mpaka mwisho” (Ebr. 3:5, 6).

UNABII WA UJIRA

“Wakiiacha njia iliyonyoka, wakapotea, wakiifuata njia ya Balaamu, mwana wa Beori, mtu ambaye hakuwa na kipingamizi chochote kwa uovu ilimradi ungelimpatia ujira” (2 Petro 2:15, Fasiri ya Phillips).

Wakati fulani Balaamu alikuwa mtu mwema na pia nabii wa Mungu; lakini sasa alikuwa ameasi, na alikuwa amejiingiza katika tamaa; hata hivyo bado alidai kuwa mtumishi wa Mungu Mkuu. Hakuwa mtu asiyejua utendaji wa Mungu kwa ajili ya Israeli; na wale wajumbe walipomweleza ujumbe waliokuja nao, alifahamu vyema kuwa ulikuwa wajibu wake kukataa zawadi za Balaki na kuwaondosha hao mabalozi. Lakini alithubutu kuchezacheza na majaribu, akawahimiza wajumbe hao wakae pamoja naye usiku huo, huku akitamka kuwa asingeliweza kutoa jibu lolote la hakika hadi atakapokuwa ameomba mashauri ya Bwana. Balaamu alijua kuwa laana yake isingeweza kuwadhuru Israeli. Mungu alikuwa katika upande wao, na kadiri walivyodumu kuwa waaminifu Kwake hakuna uwezo wowote mwovu wa kidunia au jehanamu ambao ungeweza kuwashinda. Lakini kiburi chake kilidanganywa kwa maneno ya wale wajumbe, “Yeye umbarikiye hubarikiwa, na yeye umlaaniye hulaaniwa.” Rushwa ya zawadi za thamani na matarajio ya kutukuzwa viliamsha tamaa yake. Alikubali kwa ulafi hazina zilizoahidiwa kwake, na kisha, wakati akidai kuwa mtii kamili kwa mapenzi ya Mungu, alijaribu kukubaliana na matakwa ya Balaki….
Dhambi ya tamaa ya mali, ambayo Mungu anaitaja kama ibada ya sanamu, ilikuwa imemfanya kuwa mhanga wa mazingira, na kupitia kosa hili moja Shetani alipata nafasi ya kumtawala kabisa. Hili ndilo lililosababishia uangamivu wake. Daima yule mjaribu anaendelea kuwasilisha manufaa na heshima za kiulimwengu ili kuwashawishi watu waache utumishi wa kazi ya Mungu. Anawaambia kwamba uangalifu wao uliopita kiasi ndio unaowazuia wasipate mafanikio. Kwa namna hiyo wengi wanashawishika ili kuthubutu kutoka kwenye njia ya uadilifu kamili. Hatua moja mbaya huifanya nyingine kuwa rahisi zaidi, na huendelea kuwa na ufidhuli zaidi na zaidi. Watafanya na kuthubutu mambo ya kutisha sana mara wanapokuwa wamejiingiza mara moja chini cha utawala wa ulafi na tamaa ya ukuu. Wengi hujidanganya kwamba wanaweza kutoka kwenye uadilifu kamili kwa muda fulani,… na baada ya kufanikisha lengo lao, wanaweza kubadilisha mwenendo wao wakati watakapoona kuwa vyema. Watu wa namna hiyo wanajifunga wenyewe katika mtego wa Shetani, na ni kwa nadra kwamba watajinasua.

Friday, April 14, 2017

ANATUPENDA JINSI TULIVYO

Kwa kawaida watu hupenda kile kinachowaongezea furaha au faida fulani. Ni vigumu kwa binadamu kupenda kisichomvutia na kinachomtia hasara au kumpenda kiumbe aliyejitangaza mwenyewe kuwa adui. “Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.” (Warumi 5:8) Tangu dhambi ilipoingia duniani, sisi wanadamu tumekuwa adui wa Mungu. Tumekuwa tukimkimbia Mungu kila anapotusogelea. “Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha.” (Mwanzo 3:9-10)

Maagizo ya Mungu yamejenga uadui nafsini mwetu. “Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.” (Warumi 8:7) Hali hiyo ilipelekea maisha kuwa yasiyo na amani jambo lililohitaji uingiliaji kati wa haraka. Mungu aliuondoa uadui huo kwa kifo cha Yesu pale msalabani. “Akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.” (Wakolosai 2:14-15)

Upendo huu wa kuwapenda rafiki zako ambao bado wanakuchukulia kuwa ni adui yao unapatikana kwa Mungu pekee. “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.” (Yohana 15:13) Upendo huu hauangalii kama anayependwa ataitikia upendo huo na kukubali kurejeshwa kwa mahusiano ama ataendelea na dhana yake ya uadui. Upendo ulio tayari kutoa uhai kwa ajili ya wengine. Mungu hatupendi kwa matarajio kuwa tutampenda. Anawapenda wote wema kwa wabaya na angependa nasi tupendane kwa bila kubagua. “Ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.” (Mathayo 5:45)

Upendo wa Mungu ni tabia yake ambayo haitegemei mazingira. “Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake.” (1 Yohana 4:16). Upendo wa kibinadamu ungekuwa kama ule wa Mungu ungekuwa haulazimishwi na faida utakazozipata kwa unayempenda. Tabia yetu ya upendo ungejengwa juu uthamani wa kila kiumbe kilichoumbwa na Mungu na wala si mwonekano wa nje tu wa viumbe hivyo, tusingeshuhudia unyanyapaa uliopo. “Maana mkiwapenda wale wawapendao ninyi, mwaonyesha fadhili gani? Kwa kuwa hata wenye dhambi huwapenda wale wawapendao.” (Luka 6:32)
Mwanadamu ni kiumbe anayestahili kupendwa kwa sababu kuu mbili. Anastahili kupendwa kwa sababu aliumbwa katika viwango vya juu vya ubora. “Mtu ni kitu gani hata umkumbuke, Na binadamu hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; Umemvika taji ya utukufu na heshima.” (Zaburi 8:4-5) Mwanadamu amefanyika katika viwango vya ubora ulio chini kidogo ya ule wa Mungu. “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.” (Mwanzo 1:26)

Sababu ya pili kwa nini mwanadamu ni wa thamani na anayestahili kupendwa ni ule ukweli kuwa alikombolewa kwa thamani kubwa kuliko thamani zote za duniani na mbinguni. “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo.” (1 Petro 1:18-19). Amgusaye mwanadamu ni sawa na yule aigusaye mboni ya jicho la Mungu. “Kwa maana Bwana wa majeshi asema hivi, Ili nitafute utukufu amenituma kwa mataifa wale waliowateka ninyi; maana yeye awagusaye ninyi aigusa mboni ya jicho lake.” (Zekaria 2:8)

Mungu anatualika kujifunza upendo wake mkuu kwa wanadamu. “Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu.” (Waefeso 3:17-19) Mungu anatupenda tulivyo.

HAKUNA UDHURU WA KUTENDA DHAMBI

“Wakamghadhibisha penye maji ya Meriba, Hasara ikampata Musa kwa ajili yao, Kwa sababu waliiasi roho yake, Akasema yasiyofaa kwa midomo yake”
(Zaburi 106:32, 33).

Kama Musa na Haruni wangelikuwa wanaendekeza hali ya kujistahi au kuendekeza roho ya hasira licha ya onyo na karipio la Mungu, hatia yao ingelikuwa kubwa sana. Lakini hawakuwa na hatia ya dhambi ya kukusudia au kudhamiria; walikuwa wameangushwa na jaribu la ghafla, na majuto yao yalifanyika mara moja, tena toka moyoni. Bwana aliikubali toba yao, ingawa kwa sababu ya madhara ambayo dhambi yao ingeliweza kuyasababisha miongoni mwa watu, asingeliweza kufutilia mbali adhabu hiyo…..
Mungu alikuwa amewasamehe watu maasi makubwa zaidi, lakini asingeliweza kushughulikia dhambi ya viongozi hawa kama alivyofanya kwa wale waliokuwa wakiongozwa. Alikuwa amempatia Musa nafasi ya heshima kubwa kuliko mwanadamu yeyote duniani…. Ukweli kwamba Musa alikuwa amepata nuru na maarifa makubwa kiasi hicho uliifanya dhambi yake kuwa mbaya zaidi. Uaminifu wa wakati uliopita hautaweza kuwa udhuru wa kusamehe kosa hata moja. Kadiri nuru na fursa anazopewa mwanadamu zinapokuwa kubwa zaidi, ndivyo pia wajibu wake unavyokuwa mkubwa zaidi, kadiri kosa lake linavyokuwa baya zaidi, na pia ndivyo adhabu yake huwa kali zaidi..
Musa hakuwa na hatia ya kufanya uovu mkubwa, kama ambavyo watu wanaweza kuliangalia suala hili…. Lakini endapo Mungu alishughulikia dhambi hii vikali sana kiasi hicho kwa mtumishi wake huyu mwaminifu na aliyeheshimiwa kuliko wote, hatawezi kuipuuzia dhambi kwa wengine…. Wote wanaodai kuwa wacha Mungu wako chini ya wajibu mtakatifu sana wa kulinda roho zao, na kujitawala wanapokabiliwa na uchokozi mkubwa zaidi. Wajibu uliowekwa juu ya Musa ulikuwa mkuu sana; ni wanadamu wachache ndio watakaojaribiwa kama ilivyokuwa kwake; hata hivyo hili halikuruhusiwa kuwa udhuru wa kupuuzia dhambi yake. Mungu aliandaa mpango wa kutosha kwa ajili ya watu Wake; na kama wakitumainia nguvu zake, kamwe hawataweza kuwa wahanga wa mazingira. Jaribu zito sana kuliko yote haliwezi kuwa udhuru wa dhambi. Hata kama shinikizo lililoletwa ili kuikabili roho litakuwa kubwa kiasi gani, uasi ni tendo letu sisi wenyewe. Haipo katika nguvu ya dunia wala jehanamu kumshurutisha yeyote kutenda uovu. Shetani anatushambulia katika maeneo yale ambayo tu dhaifu, lakini hatupaswi kushindwa. Hata kama shambulizi ni kali au lisilotarajiwa kiasi gani, Mungu ametupatia msaada, na katika uwezo wake tunaweza kushinda.

Thursday, April 13, 2017

ZAHAMA KATIKA ISRAELI

“Walifanya ndama huko Horebu, Wakaisujudia sanamu ya kuyeyuka. Wakaubadili utukufu wao Kuwa mfano wa ng’ombe mla majani” Zaburi 106:19, 20.

Wakati Musa akiwa hayupo, mamlaka ya kufanya maamuzi yalikasimishwa kwa Haruni, na umati mkubwa ukakusanyika kulizunguka hema lake, wakiwa na dai hili: “Haya! Katufanyizie miungu itakayokwenda mbele yetu, kwa maana Musa huyo… hatujui yaliyompata.” Kuhusu lile wingu, walisema, . . . sasa limetulia kabisa pale mlimani; na lisingeendelea tena kuelekeza safari zao. . . . Zahama kama hiyo ilimhitaji mtu thabiti, mwenye uamuzi imara, na ujasiri usioyumba; yule ambaye ameinua juu heshima ya Mungu kuliko umaarufu wa kupendwa na watu, usalama binafsi, au uhai wenyewe. Lakini kiongozi huyu wa Israeli hakuwa na sifa hizi za kitabia.
Haruni alipingana na watu hawa kinyonge, lakini tabia yake ya kutetereka na woga katika wakati huo hatari sana uliwafanya tu watu hao kuwa washupavu zaidi…. Wapo baadhi walioendelea kuwa waaminifu kwa agano lao pamoja na Mungu, lakini sehemu kubwa sana ya watu hao ilijiunga katika uasi….
Haruni alihofia usalama wake mwenyewe; na badala ya kusimama kwa uadilifu ili kutetea heshima ya Mungu, alikubaliana na madai ya umati huo. . . .
Alitengeneza sanamu ya ndama wa kuyeyusha, kwa kuiga mfano wa miungu ya Misri. Watu hao wakatangaza, “Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri.” Na Haruni kwa uovu akaruhusu tu fedheha hii dhidi ya Yehova. Na alifanya zaidi ya hili. Baada ya kuona jinsi mungu huyo wa dhahabu alivyopokelewa kwa ridhaa, alijenga madhabahu mbele yake, kisha akatangaza akisema, “Kesho itakuwa sikukuu kwa Bwana.”
Tangazo hili lilienezwa kwa matarumbeta toka kundi moja hadi lingine katika mahema yao yote…. Chini ya kisingizio cha kuadhimisha “sikukuu kwa Bwana,” walijiingiza katika shamrashamra za ulafi na ufisadi.
Ni mara nyingi kiasi gani, hata katika siku zetu, ambapo kupenda anasa kunafunikwa kwa “mtindo wa utauwa!” Dini inayowaruhusu wanadamu wajihusishe katika uendekezaji wa ubinafsi au tamaa za kimapenzi, huku wakiendelea kufanya taratibu zao za ibada, huwavutia watu wengi sana wakati huu kama ilivyokuwa katika siku za Israeli.
Na bado wapo akina Haruni wanaoshawishika kirahisi, ambao, wakati wakiendelea kushikilia nyadhifa za uongozi kanisani, watakubaliana na shauku za wale ambao hawajaongoka, na hivyo huwahamasisha katika dhambi.

ALIPOTEZA SUBIRA YAKE

"Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno” (Yakobo 1:4).

Bila kujali ukweli kuwa Musa alikuwa mwanadamu mpole zaidi miongoni mwa wanadamu walioishi usoni pa nchi, katika tukio mojawapo alijiletea ghadhabu ya Mungu….
Shutuma za watu zilizompata na asizozistahili, zilimfanya kwa muda kitambo asahau kwamba manung’uniko yao hayakuwa juu yake, bali dhidi ya Mungu; na badala ya kuhuzunika kwa sababu Roho wa Mungu alikuwa akitukanwa, alikasirishwa, akachukizwa, na katika namna ya ushupavu na pupa, aliupiga ule mwamba mara mbili akisema: “Sikieni sasa, enyi waasi; je! Tuwatokezee maji katika mwamba huu?”…
Musa alidhihirisha udhaifu mkuu mbele ya watu. Alionesha bayana kukosa kujitawala, roho inayofanana na ile waliyokuwa nayo wale wanung’unikaji. Angelipaswa kuonesha mfano wa ustahimilivu na saburi mbele ya umati huo, waliokuwa tayari kujipatia udhuru wa makosa yao, chuki, na manung’uniko yasiyokuwa na maana, kwa ajili ya udhihirisho wa kosa hili kwa upande wake.
Dhambi kubwa kabisa ilikuwa kujitwalia nafasi ya Mungu. Nafasi ya heshima ambayo Musa alikuwa ameshikilia hadi hapa haikuhafifisha hatia yake, bali iliikuza zaidi. Mpaka hapa alikuwa mtu asiyekuwa na hatia, lakini sasa ameanguka. Wengi katika nyadhifa za namna hiyo wangeweza kudhani kwamba dhambi yao ingesamehewa kwa sababu ya maisha yao ya muda mrefu ya uaminifu usioyumba.
Lakini hapana; lilikuwa ni jambo baya kabisa kwa mtu ambaye alikuwa ameheshimiwa na Mungu kuonesha udhaifu wa kitabia katika kudhihirisha hisia ya hasira kali kuliko kama vile ambavyo angelikuwa na wadhifa mwingine wa madaraka chini ya hapo. Musa alikuwa mwakilishi wa Kristo, lakini inahuzunisha kiasi gani jinsi taswira hiyo ilivyoharibiwa! Musa alikuwa ametenda dhambi, na uaminifu wake uliopita usingeweza kumponya katika dhambi ya sasa….
Musa na Haruni wafe bila kuingia Kanaani, wakabiliwe na adhabu ileile iliyowapata wale waliokuwa katika nyadhifa za chini. Walisujudia katika kujisalimisha, ingawa kwa uchungu wa moyo ambao haukuelezeka; lakini upendo wao na imani yao kwa Mungu havikutikiswa…. Lakini ni wachache wanaotambua ubaya wa dhambi…. Uzoefu wa Musa na Haruni… huonesha kwamba siyo jambo salama kutenda dhambi katika neno au wazo au tendo.

"Rehema za Bwana ni mpya kila siku asubuhi.”
(Maombolezo 3:22, 23).