Wednesday, May 10, 2017

SIRI NI HII


📖“Lakini hakujua ya kuwa BWANA amemwacha.” Waamuzi 16:20
______________
Siku kwa siku Delila alimsumbua kwa maswali, hadi “roho yake ikadhikika hata kufa;” hata hivyo mvuto fulani ulimnasa asimudu kujinasua. Hatimaye Samsoni alizidiwa nguvu na mwanamke huyo, akaamua kumfunulia siri ya nguvu zake. “Wembe haukupita kwenye kichwa changu kamwe; maana mimi nimekuwa Mnadhiri wa Mungu, tangu tumboni mwa mama yangu. Nikinyolewa ndipo nguvu zangu zitanitoka, nami nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu.”

Mjumbe alitumwa kwa jopo la viongozi wa Wafilisti, akiwahimiza wafike upesi pasipo kukawia. Wakati shujaa amelala, nywele zake nyingi kichwani mwake zilinyolewa. Kama alivyokuwa amefanya mara tatu zilizopita, aliita, “Samsoni, Wafilisti wanakuja!” Kwa haraka akaamka, akidhania kudhihirisha nguvu zake kama ilivyokuwa hapo awali, na kuwaangamiza; ila mikono yake dhaifu ilishindwa kufanya makuu, akatambua “BWANA amemwacha.”

Baada ya kunyolewa, Delila alijaribu kumsumbua ili kujaribu nguvu zake, kwani Wafilisti hawakuthubutu kumsogelea hadi walipojua nguvu zake zimetoweka. Ndipo wakamkamata, wakamng’oa macho, kisha wakamchukua hadi Gaza. Hapa alifungwa kwa minyororo gerezani akitumikishwa kazi ngumu.

Ni aibu iliyoje kwa yeye aliyekuwa Mwamuzi na Shujaa katika Israeli!—sasa yu dhaifu, kipofu, mfungwa, aliyedhalilishwa kutumikia huduma ya kitumwa. Hatua kwa hatua amekaidi masharti ya wito wake mtakatifu. Mungu amemvumilia kwa kipindi kirefu; ila kwa sasa, kwa hiari yake mwenyewe, alipojisalimisha kwenye nguvu za uovu, kwa kufunua siri ya nguvu zake, BWANA alimwacha. Hapakuwepo mwujiza maalumu ndani ya nywele zake, ila zilikuwa ishara ya utii wake kwa Mungu; na alipoisalimisha ishara hiyo ya utii ili kukidhi haja za tamaa zake za mwili; mbaraka huo uliowakilishwa kupitia ishara hiyo nao ukatoweka.

Kama kichwa cha Samsoni kingalinyolewa pasipo kosa kwa upande wake, nguvu zake zingalibakia. Ila mwenendo wake umekuwa ukipingana na mamlaka ya Mungu kana kwamba tayari ameshazikata nywele za kichwa chake. Hivyo Mungu alimwacha avune matokeo ya upumbavu wake.

No comments: