Friday, May 26, 2017

NI KWA JINSI GANI YESU KRISTO ALIITIMIZA TORATI NA MANABII?


Yesu alipozungumzia “torati na manabii” alimaanisha mafundisho ya Agano la Kale, ambayo kwa wakati huo ndiyo yaliyokuwa kiini cha imani ya wacha-Mungu. Yesu anasema hakuna kuondoa au kubatilisha/kufuta mamlaka ya Agano la Kale. Hakuja kupindua, kubatilisha, wala kufuta bali kuendeleza au kuitekeleza.

Yesu aliitimiza torati na manabii kwa kujisalimisha Yeye binafsi kuwa mtii wa sheria (Yohana 15:10), kwa kuipatia utoshelevu kamili uliohitajika kulingana na haki ya Mungu. Haki ya Mungu ilidai mauti ya mwasi wa sheria Yake. Kristo aliitimiza kwa kufa kwa niaba ya mdhambi. Aliitimiza sheria kwa kuifanya sheria iwe kanuni Yake ya mwenendo na maisha, kwa kuifundisha kwa watu kikamilifu, kuipatia maana halisi. 

Yesu alikuja kutimiza kusudi husika la torati na manabii. Alikuja kukuza vidokezo na hazina za kweli, kugeuza kanuni na maagizo yaliyokuwa yamewekwa na wanadamu mahali pa Amri za Mungu (rejea Mathayo 15:9; Marko 7:7-9). Alikuja kutimiza haki yote (Mathayo 3:15) kwa njia ya utii kamili wa kanuni za Sheria ya Mungu. Alikuja kutimiza chochote kilichokuwa kielelezo au mfano Wake. Yeye ndiye alikuwa “mwili” halisi (Wakolosai 2:17). Sheria ya Musa iliundwa kwa mfumo wa kafara na taratibu za kidini zilizokusudiwa kumwakilisha Kristo na kuelekeza katika ujio Wake. Hizi zilitimizwa wakati alipojitoa nafsi Yake Kafara kwa Mungu.

Kristo alithibitisha na kusisitiza sheria ya Mungu kwa kina zaidi, katika maana yake pana na ya ndani zaidi. Kwa wenge, ilifahamika kwamba kuua ni kufanya tu tendo husika la kuondoa uhai, lakini Yesu alifundisha kwamba hata chuki tu dhidi ya mtu ni sawa na uuaji. Pia kuhusu zinaa na uasherati alisema vinahusisha uendekezaji wa mawazo na fikra chafu za tamaa ya mwili. Alionesha kwamba utekelezaji kamili wa sheria huanzia moyoni. Utii wa andiko la sheria kwa nje huanza na utii utokanao na nia ya rohoni.

Hivyo ni hatari kabisa kudhani kwamba Kristo amewaruhusu watu Wake kutupilia mbali maagizo yoyote ya sheria Yake takatifu ya Mungu. Kuvunja amri moja ni sawa na kuwa mkosaji wa zote (Yakobo 2:10, 11). Haki ya Kristo, inayohesabiwa kwetu bure kwa imani pekee, huhitajika na kila mmoja anayeingia katika ufalme Wake wa neema au utukufu; kiumbe kipya aliyefanyika katika Kristo huwa na badiliko kamili la maisha liendanalo na utii wa Amri Zake.

“Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua Yeye, ikiwa tunashika amri Zake. Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri Zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake. Lakini yeye alishikaye neno Lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli. Katika hili twajua ya kuwa tumo ndani Yake. Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani Yake, imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama Yeye alivyoenenda.” 1 Yohana 2:3-6.

No comments: