Thursday, May 25, 2017

MAKUNDI MAWILI YATAKAYOFUNGA HISTORIA YA MWISHO WA DUNIA

 Na Pr. Joackim Msembele.

Malaika wakipeleka ukweli wa Mungu wa sasa wa onyo la mwisho kwa dunia inayoangamia kwa sababu ya makosa na dhambi za wakazi wa dunia hii.
 

JE! UNAJUA KINACHOTOKEA SASA HIVI NA KINACHOTAKA KUTOKEA HIVI KARIBUNI? ENDELEA KUSOMA UJUMBE HUU KWA MAKINI.
“Tena kutakuwa na ishara katika jua na mwezi, na nyota na katika nchi dhiki ya mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake: watu wakivunjika mioyo kwa hofu na kwa kutazamia mambo yatakayoupata ulimwengu. Kwa kuwa nguvu za mbinguni zitatikisa. Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adam akija katika wingu pamoja na nguvu na utukufu mwingi.
Basi mambo hayo yaanzapo kutokea changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia” (Luka 21:25-28).
 

KUNDI LA KWANZA
“ “Dunia hii itafanywa tupu kabisa, na kuharibiwa kabisa, maana BWANA amenena neno hilo. Dunia inaomboleza, inazimia; ulimwengu unadhoofika, unazimia; watu wakuu wa dunia wanadhoofika. Tena dunia imetiwa unajisi kwa watu wanaoikaa; kwa maana wameziasi sheria, wameibadili amri, wamevunja agano la milele. Ndiyo sababu laana imeila dunia hii, na hao wanaoikaa wameonekana kuwa na hatia. Ndiyo sababu watu wanaoikaa dunia wameteketea, watu waliosalia wakawa wachache tu.” (Isaya 24:3, 4, 5, 6)
Kuomboleza na kuzimia kwa dunia ni pamoja na – Majanga ya asilii yanayotokea, kama vile; mabadiliko ya tabia ya nchi yanayosababisha ongezeko la joto duniani na kuleteleza; mafuriko, ukame, kuyeyuka kwa barafu kaskazini mwa ncha ya dunia na hata katika mlima wa Kilimanjaro, vimbunga na matetemeko ya ardhi, nk.
 

Kudhoofika na kuzimia kwa ulimwengu ni pamoja na kuvunjika kwa maadili; kama vile kubaka hata watoto, kuua albino, kuoana jinsia moja, machafuko ya siasa, migomo ya wafanyakazi, nk.
Kudhoofika kwa watu wakuu wa dunia:
Kila kiongozi wanchi hatawali kwa raha, misongo mingi; kukosolewa kwingi; maandamano ya raia kila mahali. Uchaguzi ukipita hakuna anayeridhika. Tuhuma nyingi za wizi wa kura; na wengine hata kung’ang’ania madaraka hata kama kura zimetangazwa na kuonekana wameshindwa. Hayo yote yanawalenga watu wakuu wa dunia. Ni unabii wa kufungwa kwa histaoria ya mwisho wa dunia.

Haya yote yanatokea ni kwa sababu wameziasi sheria, wameibadili amri, wamelivunja agano la milele. Katika amri 10 za Mungu, ulimwengu umeasi amri ya 1 hadi ya 4 ambazo Yesu alisema ndiyo amri kuu tena ni ya kwanza (Mathayo 22:35-38). Ulimwengu umeasi amri zifuatazo: ya-
Usiwe na miungu mingine ila mimi.
Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni wala kilicho chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, BWANA, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu.
Usilitaje bure jina la BWANA, Mungu wako, maana BWANA hatamhesabia kuwa hana hatia mtu alitajaye jina lake bure.
Ikumbuke siku ya sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni sabato ya BWANA Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yoyote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako.
Maana, kwa siku sita BWANA alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo BWANA akaibarikia siku ya sabato akaitakasa.” (Kutoka 20:3-11)
Amri hizi haziko kwenye vitabu vya sheria vya mahakama za nchi zote duniani. Na watu wengi hawana habari. Ndiyo sababu laana imeila dunia hii.


MWISHO WAKE UTAKUWAJE?
“Dunia kuvunjika, imevunjika sana; dunia kupasuka, imepasuka sana dunia kutikisika inatikisika sana; dunia inalewa-lewa kama mlevi, nayo inawaya-waya kama machela; na mzigo wa dhambi zake utailemea; nayo itaanguka,wala haitainuka tena.” (Isaya 24:19-20)

Dhambi ni nzito kuliko bomu la nyuklia. Mabomu ya nyuklia yanafanyiwa majaribio, lakini dunia haitikisiki ila dhambi haitaitikisa tu dunia bali itaiangusha dunia na haitainuka tena.
Dhambi ni uasi wa sheria za Mungu ambazo ni pamoja na amri nne (4) zilizotajwa hapo juu. Ndiyo maana Mungu anataka watu wote wazitii amri zote za Mungu ambapo ndani yake inasema pia watu wote waitakase sabato na kutokuabudu na kutumikia sanamu. Hebu soma maneno yafuatayo uone namna ambavyo Mungu anajifunua kwa wajawake.
“BWANA asema hivi, shikeni hukumu, mkatende haki; kwa maana wokovu wangu u karibu kuja, na haki yangu kufunuliwa. Heri afanyaye haya, na mwanadamu ashikaye sana; azishikaye sabato asizivunje, auzuiaye mkono wake usifanye uovu wowote. Wala mgeni, aambatanaye na BWANA, asisema hivi, Hakika yake BWANA atanitenga na watu wake; wala towashi asiseme, Mimi ni mti mkavu. Kwa maana BWANA awaambia hivi matowashi, wanazishika sabato zangu, na kuyachagua mambo ya nipendezayo, na kulishika sana agano langu; Nitawapa hawa nyumbani mwangu, na ndani ya kuta zangu, kumbukumbu na jina,lililo jema kuliko kuwa na wana na binti; nitawapa jina lidumlo milele, lisilokatiliwa mbali. Na wageni, walioandamana na BWANA ili wa mhudumu, na kulipenda jina la BWANA, kuwa watumishi wake: kila aishikae sabato asiivunje, na kulishika sana agano langu; Nitawaleta hao nao hata mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; makafara yao na dhabihu zao zitakubaliwa juu ya madhabahu zangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote. Bwana MUNGU, akusanyaye waliofukuzwa katika Israeli asema, pamoja na hao nitamkusanyia na wengine zaidi ya hao walio wake waliokusanywa.” (Isaya 56:1-8).
“Basi, imesalia raha ya sabato kwa watu wa Mungu.” (Waebrania 4:9) “Yeye asemaye Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli kweli haimo ndani yake.” (1Yoh. 2:4).hii ni kundi la kwanza, limeziasi sheria 4 za kwanza.


KUNDI LAPILI – kundi hili ni kwa watu gani?
“Piga kelele, usiache, Paza sauti yako kama tarumbeta; uwahubiri watu wangu kosa lao. Na nyumba ya Yakobo dhambi zao.” (Isaya 58:1) watu wake ni akina nani?
“Zitakaseni sabato zangu; zitakuwa ishara kati ya mimi na ninyi mpate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA Mungu wenu.” (Ezekiel 20:20).
Lakini hawa watu wake wanaozitakasa sabato pia wana makosa na dhambi.
Dhambi yao kubwa ni kutokuwaambia wengine ujumbe muhimu wa Mungu wa wakati huu.

HAYA MAKUNDI MAWILI NI YAPI?
Makundi mawili yanayofunga historia ya mwisho wa dunia ni:

Kundi la 1. AWASIOTUNZA SABATO YA BWANA MUNGU.
Kundi la 2. WANAOITUNZA SABATO YA BWANA MUNGU.
Kila kundi litakuwa na watu watakao kwenda mbinguni na watakaoshindwa kwenda mbinguni.
Rehema ilishawahi kufungwa mara nne katika kipindi cha nyuma cha historia ya dunia hii. Nyakati hizo ni;
Wakati wa Nuhu
Wakati wa Sodoma na Gomora
Katika mwaka wa 70 B.K.
Katika mwaka1844
Kila wakati mlango wa rehema ulipotaka kufungwa, Mungu alikuwa akitoa alama ya kuokolewa kabla ya tukio kama ifuatavyo:


KIPINDI CHA:- ALAMAYA KUOKOLEWA NI KWA:-
Nuhu ---------- kuingia ndani ya Safina
Sodoma na Gomora ----- Kukimbilia Mlimani au Soari
Katika mwaka wa 70 B.K. -------- Kukimbilia Mlimani
Katika mwaka wa 1844 ---------- Kukimbilia Mlimani.


NI NINI ALAMA YA KUOKOLEWA KATIKA KIPINDI HIKI CHA KUFUNGA HISTORIA YA DUNIA?
Alama ya kuokolewa kwa wasiotunza sabato za BWANA Mungu, ni kutii sabato ya BWANA Mungu, na amri na amri zingine zilizoachwa.
Alama ya kuokolewa kwa wanaozitunza sabato za BWANA Mungu, ni kuwa taarifu wengine kwa bidii juu ya wajibu na ujumbe huu muhimu.
Kila mtu aliye hai ana nafasi ya kuokolewa au kupotea. Mpendwa msomaji, kumbuka kuwa kuna BWANA Mungu aliyekuumba wewe na kuna Shetani ambaye hakukuumba wewe. Katika pande hizi mbili unapiga kura yako kwa nani? Ndugu msomaji nakusihi kwa neema yake Yesu piga kura yako kwa BWANA Mungu nawe utaokolewa na kuishi milele. Hii ndiyo thamani ya ubinadamu.
“Amini, nawaambieni, kizazi hiki hakitaPIta hata hayo yote yatimie. Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo; Kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima.
Basi, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba ili mpate kuokoka katika hayo yote yatakayotokea, na kusimama mbele za mwana wa Adam” (Luka 21:32-36).
“Hapa ndipo penye subira ya watakatifu hao wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu” (Ufunuo 14:12).
Usitatanike kuelewa siku ya sabato ni ipi; hebu soma, Math 28:1-6, Marko 15:42-47; 16:1-6, Luka 23:44-56; 24:1-3 na Yoh 19:31-42; 20-1.
Yesu hakubadilisha sabato (Math 5:17-19 na Zab 89:34), ila mfalme Konstantino wa Rumi ndiye aliibadilisha sabato ya Biblia ya siku ya saba ya juma (jumamosi) na kuipelekea siku ya kwanza ya juma (jumapili) mnamo tarehe 7 Machi, 321, B.K. (Historia ya Kanisa la Kikristo, Toleo la 7 la mwaka 1902, Gombo la 3, uk. 380). Kufanya ibada siku ya kwanza ya juma (jumapili) ni mapokeo ya mfalme Konstantino wa Rumi, na kinyume na Biblia. (Soma; Mathayo 15:3-9 na Marko7:6-9).
Kuabudu siku ya jumapili BWANA Mungu anasema ni mapokeo “Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami, Nao waniabudu bure, wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu …. Ninyi mwaiacha amri ya Mungu na kuyashika mapokeo ya wanadamu, Akawaambia, Vema Mwaikataa amri ya Mungu mpate kuyashika mapokeo yenu”. (Mathayo 15:8-9; Marko 7:8-9).
 

MUNGU ASEMA MWONGO NI NANI? “Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake.” (1Yohana 2:4).
Wewe unataka kuwa mkristo wa aina gani? Mkristo mwongo ambaye hataki kutii amri za Mungu au mkristo wa kweli ambaye anatii amri zote za Mungu? Chaguo lako ni lipi leo? Yesu leo anakusihi chagua kuwa mkristo wa kweli na thamani ya maisha yako itakuwa ya kudumu milele.
Ujumbe huu unatakiwa upelekwe kwa kila mkazi wa dunia hii. Na kwa hiyo tafadhali mpendwa msomaji, zalisha nakala nyingi kadiri iwezekanavyo na kumpa kila mtu unayekutana naye kwa ajili ya utukufu wa Mungu.

No comments: