Wednesday, May 10, 2017

BWANA AKAMKUMBUKA


“Samsoni akamwita Bwana, akasema, Ee Bwana MUNGU, unikumbuke, nakuomba, ukanitie nguvu, nakuomba.” Waamuzi 16:28

♻Katika mateso na kudhalilishwa, kukejeliwa na Wafilisti, Samsoni alijifunza zaidi kuhusu udhaifu wake kuliko alivyojua hapo awali; na maumivu hayo yakamwongoza kwenye toba. Kadiri nywele zake zilivyokua, nguvu zake taratibu zilirejea; ila adui zake wakimtambua kama mfungwa asiye na msaada; wakawa hawana hofu naye.

♻Wafilisti walishangilia kwamba ushindi wao umetokana na miungu yao; nao wakasherehekea, wakimtukana Mungu wa Israeli. Sherehe iliandaliwa kwa heshima ya Dagoni, mungu mwenye umbo la samaki; mlinzi wa baharini”. Toka kila kijiji na mji wa bonde lote la Wafilisti watu na wakuu wao walihudhuria. Umati wa watu ulilijaza hekalu lao kubwa na wengine wakawa orofani. Lilikuwa tukio la kucheza na kustarehe. Kulikuwepo utoaji wa kafara, nyimbo na ngoma. Ndipo, katika hitimisho la kutukuza ukuu wa Dagoni, Samsoni alisogezwa mbele. Kelele za kejeli zilitawala ukumbi wote. Watu na watawala walimbeza Samsoni na kumtukuza mungu wao ambaye amempindua “mtesi wa taifa lao.”

♻Baada ya muda, akijifanya kana kwamba ni mchovu, Samsoni aliwasihi wamruhusu aegemee kwenye nguzo mbili zinazoshikilia jengo. Kwa kimya aliomba ombi, “Ee Bwana MUNGU, unikumbuke, nakuomba, ukanitie nguvu, nakuomba, mara hii tu, Ee Mungu, ili nipate kujilipiza kisasi juu ya Wafilisti.” Baada ya ombi hilo akainama, akazishikilia nguzo hizo mbili, kwa nguvu zake zote; ile nyumba ikawaangukia hao wakuu, na watu wote waliokuwa ndani yake. “Basi wale watu aliowaua wakati wa kufa kwake walikuwa wengi kuliko wale aliowaua wakati wa uhai wake.”

♻Sanamu hiyo pamoja na waumini wake, kuhani na mtu wa kawaida, shujaa kwa mwungwana, walizikwa chini ya magofu ya hekalu la Dagoni. Na miongoni mwao alikuwepo shujaa mkuu ambaye Mungu alimchagua apate kuwakomboa watu wake.

♻ Shindano, badala ya kuwa kati ya Samsoni na Wafilisti, likawa baina ya Yehova na Dagoni, na hivyo BWANA alijitetea mwenyewe akidhihirisha uweza na mamlaka yake juu ya dunia.

No comments: