“Naye ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti.” Waamuzi 13:5
Ahadi ya Mungu kwamba Samsoni ataanza “kuwaokoa Israeli na mikono ya
Wafilisti” ilitimilika; ila historia ya maisha iligeukaje kuwa giza tupu
na ya kutisha kwa yule ambaye alitarajiwa kuwa sifa kwa Mungu na
utukufu kwa taifa! Samsoni angalikuwa mwaminifu kwa wito wake wa
kimbingu, kusudi la Mungu lingalitimizwa kwa heshima na utukufu wake.
Lakini alijisalimisha kwa majaribu na kujithibitisha kutokuwa mtiifu kwa wito aliokabidhiwa, hivyo utume wake ukaishia kwenye kushindwa, gereza, na hatimaye kifo.
Kimwili, Samsoni alikuwa mtu mwenye nguvu kuliko wote duniani; ila
katika kujitawala, uadilifu, na msimamo thabiti, alikuwa miongoni mwa
walio dhaifu mno duniani. Wengi hudhani kuwa na hisia au tamaa
zisizotawalika ni ishara ya nguvu za kitabia; ila ukweli yeye ambaye
anatawaliwa na kusukumwa na hisia zake huyo ndiye mtu dhaifu mno. Mtu
mkuu shujaa hujulikana kwa jinsi anavyotawala hisia zake; na wala si kwa
jinsi anavyoyumbishwa na hisia hizo.
Uongozi wa Mungu na ulinzi
wake umekuwa juu ya Samsoni, ili aweze kukamilisha kazi aliyoitiwa.
Tangia mwanzo kabisa alizungukwa na mazingira kufanikisha nguvu za
kimwili, akili timamu, na uadilifu kiroho. Ila chini ya ushirikiano na
marafiki waovu aliachilia kumshikilia Mungu, aliye usalama wake pekee,
akaishia kusombwa na mawimbi ya uovu. Wale waliopewa majukumu na Mungu
wapatapo majaribu wawe na hakika Mungu atawatunza; ila iwapo kwa hiari
yao, kwa jeuri, watajisalimisha chini ya nguvu za mjaribu, wataanguka
mapema au baadaye.
Wale Mungu anaokusudia wawe vyombo vyake kwa
ajili ya kazi maalumu, Shetani hutumia uwezo wake mkuu kuwapotosha.
Anatushambulia katika maeneo yetu ya udhaifu, akitenda kazi kupitia
udhaifu wetu wa kitabia kuweza kumtawala mtu katika nyanja zote; naye
anajua udhaifu huo wa kitabia iwapo unakumbatiwa, yeye atashinda. Ila
hakuna yeyote apaswaye kushindwa. Mwanadamu hakuachwa peke yake
kupambana dhidi ya nguvu za uovu. Msaada tele kutoka mkono imara wa
Mungu umeahidiwa kwa kila roho yenye shauku kupokea msaada huo.
No comments:
Post a Comment