Friday, May 26, 2017

NI KWA JINSI GANI YESU KRISTO ALIITIMIZA TORATI NA MANABII?


Yesu alipozungumzia “torati na manabii” alimaanisha mafundisho ya Agano la Kale, ambayo kwa wakati huo ndiyo yaliyokuwa kiini cha imani ya wacha-Mungu. Yesu anasema hakuna kuondoa au kubatilisha/kufuta mamlaka ya Agano la Kale. Hakuja kupindua, kubatilisha, wala kufuta bali kuendeleza au kuitekeleza.

Yesu aliitimiza torati na manabii kwa kujisalimisha Yeye binafsi kuwa mtii wa sheria (Yohana 15:10), kwa kuipatia utoshelevu kamili uliohitajika kulingana na haki ya Mungu. Haki ya Mungu ilidai mauti ya mwasi wa sheria Yake. Kristo aliitimiza kwa kufa kwa niaba ya mdhambi. Aliitimiza sheria kwa kuifanya sheria iwe kanuni Yake ya mwenendo na maisha, kwa kuifundisha kwa watu kikamilifu, kuipatia maana halisi. 

Yesu alikuja kutimiza kusudi husika la torati na manabii. Alikuja kukuza vidokezo na hazina za kweli, kugeuza kanuni na maagizo yaliyokuwa yamewekwa na wanadamu mahali pa Amri za Mungu (rejea Mathayo 15:9; Marko 7:7-9). Alikuja kutimiza haki yote (Mathayo 3:15) kwa njia ya utii kamili wa kanuni za Sheria ya Mungu. Alikuja kutimiza chochote kilichokuwa kielelezo au mfano Wake. Yeye ndiye alikuwa “mwili” halisi (Wakolosai 2:17). Sheria ya Musa iliundwa kwa mfumo wa kafara na taratibu za kidini zilizokusudiwa kumwakilisha Kristo na kuelekeza katika ujio Wake. Hizi zilitimizwa wakati alipojitoa nafsi Yake Kafara kwa Mungu.

Kristo alithibitisha na kusisitiza sheria ya Mungu kwa kina zaidi, katika maana yake pana na ya ndani zaidi. Kwa wenge, ilifahamika kwamba kuua ni kufanya tu tendo husika la kuondoa uhai, lakini Yesu alifundisha kwamba hata chuki tu dhidi ya mtu ni sawa na uuaji. Pia kuhusu zinaa na uasherati alisema vinahusisha uendekezaji wa mawazo na fikra chafu za tamaa ya mwili. Alionesha kwamba utekelezaji kamili wa sheria huanzia moyoni. Utii wa andiko la sheria kwa nje huanza na utii utokanao na nia ya rohoni.

Hivyo ni hatari kabisa kudhani kwamba Kristo amewaruhusu watu Wake kutupilia mbali maagizo yoyote ya sheria Yake takatifu ya Mungu. Kuvunja amri moja ni sawa na kuwa mkosaji wa zote (Yakobo 2:10, 11). Haki ya Kristo, inayohesabiwa kwetu bure kwa imani pekee, huhitajika na kila mmoja anayeingia katika ufalme Wake wa neema au utukufu; kiumbe kipya aliyefanyika katika Kristo huwa na badiliko kamili la maisha liendanalo na utii wa Amri Zake.

“Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua Yeye, ikiwa tunashika amri Zake. Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri Zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake. Lakini yeye alishikaye neno Lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli. Katika hili twajua ya kuwa tumo ndani Yake. Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani Yake, imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama Yeye alivyoenenda.” 1 Yohana 2:3-6.

Thursday, May 25, 2017

MAKUNDI MAWILI YATAKAYOFUNGA HISTORIA YA MWISHO WA DUNIA

 Na Pr. Joackim Msembele.

Malaika wakipeleka ukweli wa Mungu wa sasa wa onyo la mwisho kwa dunia inayoangamia kwa sababu ya makosa na dhambi za wakazi wa dunia hii.
 

JE! UNAJUA KINACHOTOKEA SASA HIVI NA KINACHOTAKA KUTOKEA HIVI KARIBUNI? ENDELEA KUSOMA UJUMBE HUU KWA MAKINI.
“Tena kutakuwa na ishara katika jua na mwezi, na nyota na katika nchi dhiki ya mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake: watu wakivunjika mioyo kwa hofu na kwa kutazamia mambo yatakayoupata ulimwengu. Kwa kuwa nguvu za mbinguni zitatikisa. Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adam akija katika wingu pamoja na nguvu na utukufu mwingi.
Basi mambo hayo yaanzapo kutokea changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia” (Luka 21:25-28).
 

KUNDI LA KWANZA
“ “Dunia hii itafanywa tupu kabisa, na kuharibiwa kabisa, maana BWANA amenena neno hilo. Dunia inaomboleza, inazimia; ulimwengu unadhoofika, unazimia; watu wakuu wa dunia wanadhoofika. Tena dunia imetiwa unajisi kwa watu wanaoikaa; kwa maana wameziasi sheria, wameibadili amri, wamevunja agano la milele. Ndiyo sababu laana imeila dunia hii, na hao wanaoikaa wameonekana kuwa na hatia. Ndiyo sababu watu wanaoikaa dunia wameteketea, watu waliosalia wakawa wachache tu.” (Isaya 24:3, 4, 5, 6)
Kuomboleza na kuzimia kwa dunia ni pamoja na – Majanga ya asilii yanayotokea, kama vile; mabadiliko ya tabia ya nchi yanayosababisha ongezeko la joto duniani na kuleteleza; mafuriko, ukame, kuyeyuka kwa barafu kaskazini mwa ncha ya dunia na hata katika mlima wa Kilimanjaro, vimbunga na matetemeko ya ardhi, nk.
 

Kudhoofika na kuzimia kwa ulimwengu ni pamoja na kuvunjika kwa maadili; kama vile kubaka hata watoto, kuua albino, kuoana jinsia moja, machafuko ya siasa, migomo ya wafanyakazi, nk.
Kudhoofika kwa watu wakuu wa dunia:
Kila kiongozi wanchi hatawali kwa raha, misongo mingi; kukosolewa kwingi; maandamano ya raia kila mahali. Uchaguzi ukipita hakuna anayeridhika. Tuhuma nyingi za wizi wa kura; na wengine hata kung’ang’ania madaraka hata kama kura zimetangazwa na kuonekana wameshindwa. Hayo yote yanawalenga watu wakuu wa dunia. Ni unabii wa kufungwa kwa histaoria ya mwisho wa dunia.

Haya yote yanatokea ni kwa sababu wameziasi sheria, wameibadili amri, wamelivunja agano la milele. Katika amri 10 za Mungu, ulimwengu umeasi amri ya 1 hadi ya 4 ambazo Yesu alisema ndiyo amri kuu tena ni ya kwanza (Mathayo 22:35-38). Ulimwengu umeasi amri zifuatazo: ya-
Usiwe na miungu mingine ila mimi.
Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni wala kilicho chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, BWANA, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu.
Usilitaje bure jina la BWANA, Mungu wako, maana BWANA hatamhesabia kuwa hana hatia mtu alitajaye jina lake bure.
Ikumbuke siku ya sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni sabato ya BWANA Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yoyote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako.
Maana, kwa siku sita BWANA alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo BWANA akaibarikia siku ya sabato akaitakasa.” (Kutoka 20:3-11)
Amri hizi haziko kwenye vitabu vya sheria vya mahakama za nchi zote duniani. Na watu wengi hawana habari. Ndiyo sababu laana imeila dunia hii.


MWISHO WAKE UTAKUWAJE?
“Dunia kuvunjika, imevunjika sana; dunia kupasuka, imepasuka sana dunia kutikisika inatikisika sana; dunia inalewa-lewa kama mlevi, nayo inawaya-waya kama machela; na mzigo wa dhambi zake utailemea; nayo itaanguka,wala haitainuka tena.” (Isaya 24:19-20)

Dhambi ni nzito kuliko bomu la nyuklia. Mabomu ya nyuklia yanafanyiwa majaribio, lakini dunia haitikisiki ila dhambi haitaitikisa tu dunia bali itaiangusha dunia na haitainuka tena.
Dhambi ni uasi wa sheria za Mungu ambazo ni pamoja na amri nne (4) zilizotajwa hapo juu. Ndiyo maana Mungu anataka watu wote wazitii amri zote za Mungu ambapo ndani yake inasema pia watu wote waitakase sabato na kutokuabudu na kutumikia sanamu. Hebu soma maneno yafuatayo uone namna ambavyo Mungu anajifunua kwa wajawake.
“BWANA asema hivi, shikeni hukumu, mkatende haki; kwa maana wokovu wangu u karibu kuja, na haki yangu kufunuliwa. Heri afanyaye haya, na mwanadamu ashikaye sana; azishikaye sabato asizivunje, auzuiaye mkono wake usifanye uovu wowote. Wala mgeni, aambatanaye na BWANA, asisema hivi, Hakika yake BWANA atanitenga na watu wake; wala towashi asiseme, Mimi ni mti mkavu. Kwa maana BWANA awaambia hivi matowashi, wanazishika sabato zangu, na kuyachagua mambo ya nipendezayo, na kulishika sana agano langu; Nitawapa hawa nyumbani mwangu, na ndani ya kuta zangu, kumbukumbu na jina,lililo jema kuliko kuwa na wana na binti; nitawapa jina lidumlo milele, lisilokatiliwa mbali. Na wageni, walioandamana na BWANA ili wa mhudumu, na kulipenda jina la BWANA, kuwa watumishi wake: kila aishikae sabato asiivunje, na kulishika sana agano langu; Nitawaleta hao nao hata mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; makafara yao na dhabihu zao zitakubaliwa juu ya madhabahu zangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote. Bwana MUNGU, akusanyaye waliofukuzwa katika Israeli asema, pamoja na hao nitamkusanyia na wengine zaidi ya hao walio wake waliokusanywa.” (Isaya 56:1-8).
“Basi, imesalia raha ya sabato kwa watu wa Mungu.” (Waebrania 4:9) “Yeye asemaye Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli kweli haimo ndani yake.” (1Yoh. 2:4).hii ni kundi la kwanza, limeziasi sheria 4 za kwanza.


KUNDI LAPILI – kundi hili ni kwa watu gani?
“Piga kelele, usiache, Paza sauti yako kama tarumbeta; uwahubiri watu wangu kosa lao. Na nyumba ya Yakobo dhambi zao.” (Isaya 58:1) watu wake ni akina nani?
“Zitakaseni sabato zangu; zitakuwa ishara kati ya mimi na ninyi mpate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA Mungu wenu.” (Ezekiel 20:20).
Lakini hawa watu wake wanaozitakasa sabato pia wana makosa na dhambi.
Dhambi yao kubwa ni kutokuwaambia wengine ujumbe muhimu wa Mungu wa wakati huu.

HAYA MAKUNDI MAWILI NI YAPI?
Makundi mawili yanayofunga historia ya mwisho wa dunia ni:

Kundi la 1. AWASIOTUNZA SABATO YA BWANA MUNGU.
Kundi la 2. WANAOITUNZA SABATO YA BWANA MUNGU.
Kila kundi litakuwa na watu watakao kwenda mbinguni na watakaoshindwa kwenda mbinguni.
Rehema ilishawahi kufungwa mara nne katika kipindi cha nyuma cha historia ya dunia hii. Nyakati hizo ni;
Wakati wa Nuhu
Wakati wa Sodoma na Gomora
Katika mwaka wa 70 B.K.
Katika mwaka1844
Kila wakati mlango wa rehema ulipotaka kufungwa, Mungu alikuwa akitoa alama ya kuokolewa kabla ya tukio kama ifuatavyo:


KIPINDI CHA:- ALAMAYA KUOKOLEWA NI KWA:-
Nuhu ---------- kuingia ndani ya Safina
Sodoma na Gomora ----- Kukimbilia Mlimani au Soari
Katika mwaka wa 70 B.K. -------- Kukimbilia Mlimani
Katika mwaka wa 1844 ---------- Kukimbilia Mlimani.


NI NINI ALAMA YA KUOKOLEWA KATIKA KIPINDI HIKI CHA KUFUNGA HISTORIA YA DUNIA?
Alama ya kuokolewa kwa wasiotunza sabato za BWANA Mungu, ni kutii sabato ya BWANA Mungu, na amri na amri zingine zilizoachwa.
Alama ya kuokolewa kwa wanaozitunza sabato za BWANA Mungu, ni kuwa taarifu wengine kwa bidii juu ya wajibu na ujumbe huu muhimu.
Kila mtu aliye hai ana nafasi ya kuokolewa au kupotea. Mpendwa msomaji, kumbuka kuwa kuna BWANA Mungu aliyekuumba wewe na kuna Shetani ambaye hakukuumba wewe. Katika pande hizi mbili unapiga kura yako kwa nani? Ndugu msomaji nakusihi kwa neema yake Yesu piga kura yako kwa BWANA Mungu nawe utaokolewa na kuishi milele. Hii ndiyo thamani ya ubinadamu.
“Amini, nawaambieni, kizazi hiki hakitaPIta hata hayo yote yatimie. Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo; Kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima.
Basi, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba ili mpate kuokoka katika hayo yote yatakayotokea, na kusimama mbele za mwana wa Adam” (Luka 21:32-36).
“Hapa ndipo penye subira ya watakatifu hao wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu” (Ufunuo 14:12).
Usitatanike kuelewa siku ya sabato ni ipi; hebu soma, Math 28:1-6, Marko 15:42-47; 16:1-6, Luka 23:44-56; 24:1-3 na Yoh 19:31-42; 20-1.
Yesu hakubadilisha sabato (Math 5:17-19 na Zab 89:34), ila mfalme Konstantino wa Rumi ndiye aliibadilisha sabato ya Biblia ya siku ya saba ya juma (jumamosi) na kuipelekea siku ya kwanza ya juma (jumapili) mnamo tarehe 7 Machi, 321, B.K. (Historia ya Kanisa la Kikristo, Toleo la 7 la mwaka 1902, Gombo la 3, uk. 380). Kufanya ibada siku ya kwanza ya juma (jumapili) ni mapokeo ya mfalme Konstantino wa Rumi, na kinyume na Biblia. (Soma; Mathayo 15:3-9 na Marko7:6-9).
Kuabudu siku ya jumapili BWANA Mungu anasema ni mapokeo “Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami, Nao waniabudu bure, wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu …. Ninyi mwaiacha amri ya Mungu na kuyashika mapokeo ya wanadamu, Akawaambia, Vema Mwaikataa amri ya Mungu mpate kuyashika mapokeo yenu”. (Mathayo 15:8-9; Marko 7:8-9).
 

MUNGU ASEMA MWONGO NI NANI? “Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake.” (1Yohana 2:4).
Wewe unataka kuwa mkristo wa aina gani? Mkristo mwongo ambaye hataki kutii amri za Mungu au mkristo wa kweli ambaye anatii amri zote za Mungu? Chaguo lako ni lipi leo? Yesu leo anakusihi chagua kuwa mkristo wa kweli na thamani ya maisha yako itakuwa ya kudumu milele.
Ujumbe huu unatakiwa upelekwe kwa kila mkazi wa dunia hii. Na kwa hiyo tafadhali mpendwa msomaji, zalisha nakala nyingi kadiri iwezekanavyo na kumpa kila mtu unayekutana naye kwa ajili ya utukufu wa Mungu.

Wednesday, May 10, 2017

BWANA AKAMKUMBUKA


“Samsoni akamwita Bwana, akasema, Ee Bwana MUNGU, unikumbuke, nakuomba, ukanitie nguvu, nakuomba.” Waamuzi 16:28

♻Katika mateso na kudhalilishwa, kukejeliwa na Wafilisti, Samsoni alijifunza zaidi kuhusu udhaifu wake kuliko alivyojua hapo awali; na maumivu hayo yakamwongoza kwenye toba. Kadiri nywele zake zilivyokua, nguvu zake taratibu zilirejea; ila adui zake wakimtambua kama mfungwa asiye na msaada; wakawa hawana hofu naye.

♻Wafilisti walishangilia kwamba ushindi wao umetokana na miungu yao; nao wakasherehekea, wakimtukana Mungu wa Israeli. Sherehe iliandaliwa kwa heshima ya Dagoni, mungu mwenye umbo la samaki; mlinzi wa baharini”. Toka kila kijiji na mji wa bonde lote la Wafilisti watu na wakuu wao walihudhuria. Umati wa watu ulilijaza hekalu lao kubwa na wengine wakawa orofani. Lilikuwa tukio la kucheza na kustarehe. Kulikuwepo utoaji wa kafara, nyimbo na ngoma. Ndipo, katika hitimisho la kutukuza ukuu wa Dagoni, Samsoni alisogezwa mbele. Kelele za kejeli zilitawala ukumbi wote. Watu na watawala walimbeza Samsoni na kumtukuza mungu wao ambaye amempindua “mtesi wa taifa lao.”

♻Baada ya muda, akijifanya kana kwamba ni mchovu, Samsoni aliwasihi wamruhusu aegemee kwenye nguzo mbili zinazoshikilia jengo. Kwa kimya aliomba ombi, “Ee Bwana MUNGU, unikumbuke, nakuomba, ukanitie nguvu, nakuomba, mara hii tu, Ee Mungu, ili nipate kujilipiza kisasi juu ya Wafilisti.” Baada ya ombi hilo akainama, akazishikilia nguzo hizo mbili, kwa nguvu zake zote; ile nyumba ikawaangukia hao wakuu, na watu wote waliokuwa ndani yake. “Basi wale watu aliowaua wakati wa kufa kwake walikuwa wengi kuliko wale aliowaua wakati wa uhai wake.”

♻Sanamu hiyo pamoja na waumini wake, kuhani na mtu wa kawaida, shujaa kwa mwungwana, walizikwa chini ya magofu ya hekalu la Dagoni. Na miongoni mwao alikuwepo shujaa mkuu ambaye Mungu alimchagua apate kuwakomboa watu wake.

♻ Shindano, badala ya kuwa kati ya Samsoni na Wafilisti, likawa baina ya Yehova na Dagoni, na hivyo BWANA alijitetea mwenyewe akidhihirisha uweza na mamlaka yake juu ya dunia.

UTAVUNA ULICHOPANDA


📖Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi, Wewe usiku-bali.” Mithali 1:10

👉🏼Samsoni wakati wa matatizo makuu yaliyomsibu alikuwa na chimbuko lile lile la nguvu kama ilivyokuwa kwa Yusufu. Angaliweza kuchagua jema au baya kama apendavyo. Badala ya kushikilia nguvu za Mungu, aliruhusu tamaa yake mbaya imtawale. Uwezo wa kufikiri ulipotoshwa, uwezo wa kimaadili ulichafuliwa. Mungu alikuwa amemwita Samsoni kwa wadhifa wa jukumu kubwa, heshima, na manufaa; ila kwanza angalipaswa kujua uongozi kwa kujifunza utii kwa sheria za Mungu.

👉🏼Yusufu alikuwa mtu huru mwenye maamuzi huru. Mema na mabaya yalikuwa mbele yake. Angaliweza kuchagua njia ya usafi, utakatifu, heshima, au njia ya uasherati na vitendo vya aibu. Alichagua njia sahihi, naye Mungu alitukuzwa. Samsoni, chini ya majaribu ya jinsi iyo hiyo, ambayo alijisababishia yeye mwenyewe, alijiachia akatekwa na tamaa mbaya. Njia aliyoichagua ilimfanya aishie kwenye aibu, majanga, na hatimaye kifo. Kuna utofauti gani ukilinganisha na maisha ya Yusufu.

👉🏼BWANA katika Neno lake alikuwa ameweka wazi kuwa watu wake hawapaswi kujifungamanisha na wale wasiompenda au kumcha. Watu wa jinsi hiyo hawataridhika kupewa heshima na upendo ule waustahilio pekee. Bali watadumu kutafuta kupata kutoka kwa mke au mume mcha Mungu upendeleo maalumu utakaohusika kupotoka na kuyaacha mapenzi ya Mungu.

👉🏼Kwa mwanamume mcha Mungu, na kwa kanisa alilojifungamanisha nalo, mke au rafiki wa kidunia ni mpelelezi kwenye kambi hiyo, ambaye atakuwa akitafuta daima kila fursa kusaliti mtumishi wa Kristo, na kumfichua kwa mashambulizi ya adui.

👉🏼Historia ya Samsoni hutoa fundisho kwa wale ambao tabia zao hazijaundwa, ambao hawajaingia kwenye jukwaa la maisha ya shughuli. Vijana wanaoingia kwenye shule zetu na vyuo watapata kila darasa la kuulisha ubongo. Iwapo wanatamani michezo na mizaha; iwapo wanachagua kuacha mema na kukumbatia uovu, wanayo fursa hiyo. Dhambi na utakatifu vipo mbele yao, na uchaguzi ni wao. Ila hebu wakumbuke kuwa “Kile mtu apandacho, ndicho atakachovuna.”

SIRI NI HII


📖“Lakini hakujua ya kuwa BWANA amemwacha.” Waamuzi 16:20
______________
Siku kwa siku Delila alimsumbua kwa maswali, hadi “roho yake ikadhikika hata kufa;” hata hivyo mvuto fulani ulimnasa asimudu kujinasua. Hatimaye Samsoni alizidiwa nguvu na mwanamke huyo, akaamua kumfunulia siri ya nguvu zake. “Wembe haukupita kwenye kichwa changu kamwe; maana mimi nimekuwa Mnadhiri wa Mungu, tangu tumboni mwa mama yangu. Nikinyolewa ndipo nguvu zangu zitanitoka, nami nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu.”

Mjumbe alitumwa kwa jopo la viongozi wa Wafilisti, akiwahimiza wafike upesi pasipo kukawia. Wakati shujaa amelala, nywele zake nyingi kichwani mwake zilinyolewa. Kama alivyokuwa amefanya mara tatu zilizopita, aliita, “Samsoni, Wafilisti wanakuja!” Kwa haraka akaamka, akidhania kudhihirisha nguvu zake kama ilivyokuwa hapo awali, na kuwaangamiza; ila mikono yake dhaifu ilishindwa kufanya makuu, akatambua “BWANA amemwacha.”

Baada ya kunyolewa, Delila alijaribu kumsumbua ili kujaribu nguvu zake, kwani Wafilisti hawakuthubutu kumsogelea hadi walipojua nguvu zake zimetoweka. Ndipo wakamkamata, wakamng’oa macho, kisha wakamchukua hadi Gaza. Hapa alifungwa kwa minyororo gerezani akitumikishwa kazi ngumu.

Ni aibu iliyoje kwa yeye aliyekuwa Mwamuzi na Shujaa katika Israeli!—sasa yu dhaifu, kipofu, mfungwa, aliyedhalilishwa kutumikia huduma ya kitumwa. Hatua kwa hatua amekaidi masharti ya wito wake mtakatifu. Mungu amemvumilia kwa kipindi kirefu; ila kwa sasa, kwa hiari yake mwenyewe, alipojisalimisha kwenye nguvu za uovu, kwa kufunua siri ya nguvu zake, BWANA alimwacha. Hapakuwepo mwujiza maalumu ndani ya nywele zake, ila zilikuwa ishara ya utii wake kwa Mungu; na alipoisalimisha ishara hiyo ya utii ili kukidhi haja za tamaa zake za mwili; mbaraka huo uliowakilishwa kupitia ishara hiyo nao ukatoweka.

Kama kichwa cha Samsoni kingalinyolewa pasipo kosa kwa upande wake, nguvu zake zingalibakia. Ila mwenendo wake umekuwa ukipingana na mamlaka ya Mungu kana kwamba tayari ameshazikata nywele za kichwa chake. Hivyo Mungu alimwacha avune matokeo ya upumbavu wake.

NINI SIRI?


“Delila akamwambia Samsoni, Tafadhali uniambie asili ya nguvu zako nyingi, na jinsi uwezavyo kufungwa, ili uteswe.” Waamuzi 16:6.

Waisraeli walimweka Samsoni kuwa Mwamuzi juu yao, naye alitawala juu ya Israeli kwa miaka ishirini. Ila kosa moja hufungua njia kwa kosa jingine. Alivutiwa na mihemko ya kianasa iliyomwongoza kwenye anguko. “Alimpenda mwanamke mmoja katika bonde la Soreki,” siyo mbali sana na nyumbani kwao. Jina la mwanamke huyo alikuwa Delila, “mwangamizi.” Wafilisti walitazama kwa makini mwenendo wa huyu adui yao, na alipojidhalilisha mwenyewe kwa kujifungamanisha na mwanamke huyu wa Kifilisti, walinuia, kupitia Delila, kukamilisha mpango wa kumwangamiza.

Jopo la watu wa heshima lenye kuundwa na mtu mmoja mmoja toka kila jimbo la Wafilisti walisafiri hadi bonde la Soreki. Hawakuthubutu kumshambulia akiwa anamiliki hazina ya nguvu zake tele, bali ilikuwa ni mpango wao kujifunza, ikiwezekana, siri ya nguvu zake. Hivyo walimhonga Delila atafute siri ya nguvu za Samsoni kisha awafunulie.

Kadiri msaliti alivyomsonga Samsoni kwa maswali, alimdhihaki kwa kumwambia nguvu zake zaweza kutoweka, awe sawa na watu wengine dhaifu, iwapo mambo fulani yatatendeka. Kila aliloambiwa alijaribisha, ila akagundua ni uongo kwani nguvu zake hazikutoweka. Kisha akamlilia akisema, “Mbona umenidanganya mara zote hizi, ukisema wanipenda, na roho yako haipo pamoja nami?” . . . Mara tatu Samsoni ameona ushahidi dhahiri kuwa Wafilisti wamepanga njama kumwangamiza kupitia huyu mpenzi wake; ila pale mpango huo ulipoonekana kukwama; mwanamke huyo alilia sana akidai amemhadaa, hampendi, naye mumewe akapumbazika asitambue hatari iliyoko mbele yake.
Mwamuzi huyu wa Israeli alitumia saa nyingi mbele ya mwanamke huyu mlaghai, saa ambazo angalizitumia kwa mafanikio na maendeleo ya watu wake. Tamaa hizi zenye kupofusha ziwezazo kumfanya shujaa aonekane dhaifu kabisa, zilikuwa zimeshamtawala akili na dhamiri.

Ukengeufu wa Samsoni ulikuwa taratibu na wa hakika. Mwanzoni hakudhamiria kufunua siri, ila kwa hiari amejitosa mwenyewe ndani ya wavu wa msaliti wa roho, na kamba zangu zilikuwa zikimsonga kutoka kila upande.

SHUJAA DHAIFU


“Naye ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti.” Waamuzi 13:5

Ahadi ya Mungu kwamba Samsoni ataanza “kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti” ilitimilika; ila historia ya maisha iligeukaje kuwa giza tupu na ya kutisha kwa yule ambaye alitarajiwa kuwa sifa kwa Mungu na utukufu kwa taifa! Samsoni angalikuwa mwaminifu kwa wito wake wa kimbingu, kusudi la Mungu lingalitimizwa kwa heshima na utukufu wake. Lakini alijisalimisha kwa majaribu na kujithibitisha kutokuwa mtiifu kwa wito aliokabidhiwa, hivyo utume wake ukaishia kwenye kushindwa, gereza, na hatimaye kifo.

Kimwili, Samsoni alikuwa mtu mwenye nguvu kuliko wote duniani; ila katika kujitawala, uadilifu, na msimamo thabiti, alikuwa miongoni mwa walio dhaifu mno duniani. Wengi hudhani kuwa na hisia au tamaa zisizotawalika ni ishara ya nguvu za kitabia; ila ukweli yeye ambaye anatawaliwa na kusukumwa na hisia zake huyo ndiye mtu dhaifu mno. Mtu mkuu shujaa hujulikana kwa jinsi anavyotawala hisia zake; na wala si kwa jinsi anavyoyumbishwa na hisia hizo.

Uongozi wa Mungu na ulinzi wake umekuwa juu ya Samsoni, ili aweze kukamilisha kazi aliyoitiwa. Tangia mwanzo kabisa alizungukwa na mazingira kufanikisha nguvu za kimwili, akili timamu, na uadilifu kiroho. Ila chini ya ushirikiano na marafiki waovu aliachilia kumshikilia Mungu, aliye usalama wake pekee, akaishia kusombwa na mawimbi ya uovu. Wale waliopewa majukumu na Mungu wapatapo majaribu wawe na hakika Mungu atawatunza; ila iwapo kwa hiari yao, kwa jeuri, watajisalimisha chini ya nguvu za mjaribu, wataanguka mapema au baadaye.

Wale Mungu anaokusudia wawe vyombo vyake kwa ajili ya kazi maalumu, Shetani hutumia uwezo wake mkuu kuwapotosha. Anatushambulia katika maeneo yetu ya udhaifu, akitenda kazi kupitia udhaifu wetu wa kitabia kuweza kumtawala mtu katika nyanja zote; naye anajua udhaifu huo wa kitabia iwapo unakumbatiwa, yeye atashinda. Ila hakuna yeyote apaswaye kushindwa. Mwanadamu hakuachwa peke yake kupambana dhidi ya nguvu za uovu. Msaada tele kutoka mkono imara wa Mungu umeahidiwa kwa kila roho yenye shauku kupokea msaada huo.

KABLA MTOTO HAJAZALIWA

📖“Ndipo huyo Manoa akamwomba Bwana, akisema, Ee Bwana, nakuomba, yule mtu wa Mungu uliyemtuma na aje kwetu mara ya pili, atufundishe hayo yatupasayo kumfanyia huyo mtoto atakayezaliwa.” Waamuzi 13:8.

💐Mungu mwenyewe alimtokea mkewe manoa na kumwambia kuwa atakuwa na mtoto mwanamume, na kwamba atakuwa mtu mkubwa atakayekomboa Israeli. Kisha akampatia maelekezo kamili kuhusu namna atakavyomlisha. Hebu tuuchukulie ujumbe huu kama unaotolewa maalumu kwa kila mama hapa duniani. Iwapo unataka watoto wako wawe na akili safi na bora, yakupasa uwe na kiasi katika mambo yote. Hakikisha moyo wako ni safi na akili yako ni timamu, ili kurithisha uzao wako afya bora ya kiakili na kimwili.

💐Kila mama anapaswa kulijua jukumu lake. Apate kujua kuwa tabia ya watoto wake itategemea zaidi mno tabia yake kabla na baada ya kuwazaa, kuliko ilivyo mivuto mingine ya nje iwe mizuri au mibaya. Mama aliye mwalimu bora kwa watoto wake, sharti kabla ya kuwazaa, adumishe mazoea ya kujikana nafsi na kujitawala; kwani huwarithisha sifa zake binafsi za kitabia, ziwe nzuri au dhaifu.
💐Washauri wasiofaa huwahimiza wakina mama umuhimu wa kukidhi kila tamaa na uchu wa chakula, ila ushauri huo ni potofu. Mama kwa agizo la Mungu ameagizwa kudhihirisha kiwango cha juu cha kujitawala. Na akina baba na akina mama wapaswa kujumuika pamoja katika jukumu hili. Wazazi wote wawili, hurithisha tabia zao kwa watoto wao, kiakili, kimwili, kimwenendo na kishauku yao ya ulaji.

💐Wengi huchukulia kimzaha somo la kiasi. Hujidanganya kuwa BWANA hajihusishi na mambo madogo madogo kama vile kula na kunywa. Ila endapo Mungu hajihusishi, mbona akajifunua kwa mkewe Manoa, akitoa maelekezo kamili, akimsisitiza mara mbili awe mwangalifu kutokuyapuuzia.

💐Wazazi wengi huchukulia madhara ya mivuto ya kipindi kabla ya mtoto kuzaliwa ni jambo dogo la kupuuziwa; ila mbingu hazichukulii hivyo. . . . Kwa maneno yaliyoongelewa kwa mama huyu wa Kiebrania, Mungu huongea kwa wakina mama wote wa zama zote.

Tuesday, May 2, 2017

MUNGU NI CHEO CHENYE NAFSI 3

MUNGU BABA, MUNGU MWANA NA MUNGU ROHO MTAKATIFU. 

KWA NINI MUNGU MWANA YAANI YESU KRISTO ALIKUFA MSALABANI NA SIYO MUNGU BABA AU MUNGU ROHO MTAKATIFU?
 
1. Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu ni baraza uumbaji ambalo liliamua Mungu Mwana yaani Yesu Kristo awe msemaji na Mtendaji mkuu. Yohana 1:1-3, 14 "Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu. 
 Vyote vilifanyika kwa huyo: wala pasipo yeye hakukufanyika cho chote kilichofanyika... Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu: nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba: amejaa neema na kweli. "
 
Wakolosai 1:14-20 "... ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi: naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana: ikiwa ni viti vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka: vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye. Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa: naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote. Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae: na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake, akisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake:kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni.".
 
Yesu ndiye aliyemwambia Adamu, "walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika". Ndiyo sababu Yesu anaitwa Neno. Msemaji mkuu wa serikali ya mbinguni.
Yesu alikufa msalabani kwa niaba ya mwanadamu. Kwa kuwa ndiye aliyesema 'utakufa hakika'. Kama asingekufa na wanadamu wasamehewe basi shetani angedai kuwa Mungu ni mwongo. Ndiyo maana neema na haki zilibusiana msalabani. Yaani neema mwanadamu asamehewe dhambi alipotenda. Haki mwanadamu atii amri na maagizo ya Mungu baada ya kusamehewa dhambi. Yesu alikufa msalabani ili kumtetea mwanadamu asife na pia kutetea maagizo au amri zake zisipuuzwe. Ndiyo maana mtu anapoasi anamrudisha Yesu msalabani. 

Waebrania 6:4-6 "Kwa maana hao waliokwisha kupewa nuru, na kukionja kipawa cha mbinguni, na kufanywa wahirika wa Roho Mtakatifu, na kulionja neno zuri la Mungu, na nguvu... Kwa kuwa wamsulubisha Mwana wa Mungu mara ya pili...".