PAMOJA NA YESU USHINDI NI WA HAKIKA.
Fungu la tafakari: “Yeye ashindaye
atayarithi haya” Ufunuo 21:17.
Makusudi ya somo hili: Kujua kwamba juhudi
ya kushinda inahitajika na kufaa zaidi.
UTANGULIZI..
Maisha haya yanatakiwa kuwa
matayarisho ya maisha yajayo. Lakini maonyo juu ya hatari ya maisha haya ni
lazima yazingatiwe. Tabia inapasa kukamilika. Kila dhambi ni lazima ishindwe.
Mungu ameweka mambo haya kama sharti, ili iwezekane kupata thawabu ya
mshindaji.
Biblia inasema katika kitabu cha Warumi 12:21; Usishindwe
na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.
Ubaya unaonekana ulimwenguni. Unaelezwa katika 1Yohana
2:16 kuwa ni “tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima” Tunapaswa
kujihadhari daima ili kwamba mambo haya yasitushinde.
Kushindwa mara moja kunamwacha mtu bila ulinzi wa
Mungu. Kawaida moja mbaya, kama haipingwi kwa nguvu, itatia nguvu minyororo ya
chuma ya shetani, na kufunga nyanja zote za mtu kamili.
Lazima tuzaliwe na mungu ndipo tutakuwa na uwezo wa
kuushinda ulimwengu, maana tutakuwa na nguvu ndani yetu. Tusalimishe nia na
mapenzi yetu kwake. 1Yohana 5:4.
Kama wakristo lazima waidhibiti na kuitawala miili
yao, kuziweka hamu zao za chakula na tamaa zao zote chini ya dhamiri
zilizoelimishwa, waone kuwa ni wajibu wao kwa Mungu kuzitii sheria ambazo
zinatawala afya na maisha, watapata mbaraka wa nguvu za kimwili na kiakili.
Watapata nguvu za kimaadili (moral power) za kupigana na shetani.
Watu wanaweza kushinda kwa njia ya Yesu Kristo peke
yake. “ Pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote. Yohana 15:5.
Kinga ya pekee dhidi ya uovu ni uwepo wa Kristo ndani
ya moyo kwa njia ya imani kwa haki yake. Hatuwezi kamwe kuyazuiya matokeo
mabaya ya kujipenda nafsi, kujifurahisha kwa
anasa , na kujaribiwa kutenda dhambi, isipokuwa tumeunganishwa kabisa na
Mungu. ... Pasipo kuwa na ujuzi binafsi wa Kristo, na kuwa na ushirika naye
unaoendelea, tunakuwa bado tuko chini ya hatarti ya kuvamiwa na adui, na
tutaishi kuyafanya matakwa ya adui.
Lakini Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana
wetu Yesu Kristo. 1Wakorintho 15:57; Ufunuo 12:11.
Wengi wanataka thawabu ya mwisho na ushindi ambao
unatolewa kwa washindi, lakini hawako tayari kustahimiri magumu, taabu, na
kujikana nafsi, kama alivyofanya Mwokozi. Tutashinda tu kwa njia ya utii na
juhudi zinazoendelea.
Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho
ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa kula matunda ya mti wa uzima, ulio
katika bustani ya Mungu.
Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho
ayaambia makanisa. Yeye
ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili.
Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho
ayaambia makanisa. Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa, nami
nitampa jiwe jeupe, na juu ya jiwe hilo limeandikwa jina jipya asilolijua mtu
ila yeye anayelipokea.
Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala
sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina lake
mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake. Ufunuo 2:7,11,17;3:5.
...“Utapata jina jipya” Ufunuo 3:12.
...”Utaketi pamoja na Kristo” Ufunuo 3:21;21:7.
Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio
halikuyasikia, wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu, mambo ambayo Mungu
amewaandalia wampendao 1Wakorintho 2:9.
RAFIKI YANGU NINAKUALIKA TUUNGANE NA MWOKOZI WETU ILI
TUPATE UZIMA, MAMBO AMBAYO JICHO “HALIKUYAONA” YATAKUWA YETU. KILA MTU ANAPASWA
AWE MSHINDI ILI ASIYAKOSE MEMA HAYA.
No comments:
Post a Comment