Wednesday, May 10, 2017

SHUJAA DHAIFU


“Naye ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti.” Waamuzi 13:5

Ahadi ya Mungu kwamba Samsoni ataanza “kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti” ilitimilika; ila historia ya maisha iligeukaje kuwa giza tupu na ya kutisha kwa yule ambaye alitarajiwa kuwa sifa kwa Mungu na utukufu kwa taifa! Samsoni angalikuwa mwaminifu kwa wito wake wa kimbingu, kusudi la Mungu lingalitimizwa kwa heshima na utukufu wake. Lakini alijisalimisha kwa majaribu na kujithibitisha kutokuwa mtiifu kwa wito aliokabidhiwa, hivyo utume wake ukaishia kwenye kushindwa, gereza, na hatimaye kifo.

Kimwili, Samsoni alikuwa mtu mwenye nguvu kuliko wote duniani; ila katika kujitawala, uadilifu, na msimamo thabiti, alikuwa miongoni mwa walio dhaifu mno duniani. Wengi hudhani kuwa na hisia au tamaa zisizotawalika ni ishara ya nguvu za kitabia; ila ukweli yeye ambaye anatawaliwa na kusukumwa na hisia zake huyo ndiye mtu dhaifu mno. Mtu mkuu shujaa hujulikana kwa jinsi anavyotawala hisia zake; na wala si kwa jinsi anavyoyumbishwa na hisia hizo.

Uongozi wa Mungu na ulinzi wake umekuwa juu ya Samsoni, ili aweze kukamilisha kazi aliyoitiwa. Tangia mwanzo kabisa alizungukwa na mazingira kufanikisha nguvu za kimwili, akili timamu, na uadilifu kiroho. Ila chini ya ushirikiano na marafiki waovu aliachilia kumshikilia Mungu, aliye usalama wake pekee, akaishia kusombwa na mawimbi ya uovu. Wale waliopewa majukumu na Mungu wapatapo majaribu wawe na hakika Mungu atawatunza; ila iwapo kwa hiari yao, kwa jeuri, watajisalimisha chini ya nguvu za mjaribu, wataanguka mapema au baadaye.

Wale Mungu anaokusudia wawe vyombo vyake kwa ajili ya kazi maalumu, Shetani hutumia uwezo wake mkuu kuwapotosha. Anatushambulia katika maeneo yetu ya udhaifu, akitenda kazi kupitia udhaifu wetu wa kitabia kuweza kumtawala mtu katika nyanja zote; naye anajua udhaifu huo wa kitabia iwapo unakumbatiwa, yeye atashinda. Ila hakuna yeyote apaswaye kushindwa. Mwanadamu hakuachwa peke yake kupambana dhidi ya nguvu za uovu. Msaada tele kutoka mkono imara wa Mungu umeahidiwa kwa kila roho yenye shauku kupokea msaada huo.

No comments: