Sunday, February 23, 2014

CHAKULA NA ATHARI ZAKE KWA BINADAMU

JE! CHAKULA KINAWEZA KUATHIRI AKILI YAKO?
(SOMA DANIELI 1 YOTE)
 
Amini usiamini, chakula kinaweza kuathiri akili yako, na afya yako ya kimwili na
kiroho. Chakula cha daraja la kwanza ambacho Mungu alimpa mwanadamu kilikuwa cha
nafaka, kokwa na matunda (Mwanzo 1:29). Dhambi ilipoingia ilileta laana sio tu kwa
viumbe vyote bali hata kwa ardhi. Kwa hiyo Mungu akamwongezea mwanadamu mboga
za majani katika lishe yake ya awali (Mwanzo 3:18). Gharika ilikaa juu ya nchi kwa miezi
mitano au siku 150 na kuharibu mimea yote (Mwanzo 7:24). Kwa hiyo Mungu
akamwongezea mwanadamu katika lishe yake "nyama" kutoka kwa wanyama safi tu
(Mwa. 8:3,4 imebainishwa na Law. 11:1-47; Kum. 14:1-21). Injini ya petroli hutumia
petroli tu; injili ya dizeli ni dizeli tu. Ukitaka gari lako life weka dizeli katika injini ya
petroli au petroli katika injini ya dizeli. Mtengenezaji ndiye anayejua gari lake litatumia
mafuta gani, sio mtumiaji. Vile vile, Mungu anajua chakula kinachofaa kwa mwili wa
mwanadamu, sio mwanadamu kujichagulia cho chote kuwa chakula. Wabishi wataharibu
injini za magari yao (miili yao).
Mungu aliumba wanyama safi na wanyama najisi juma lile la kwanza la uumbaji.
Kifo cha Yesu msalabani hakikuwa kwa kusudi la kuwabadilisha wanyama najisi kuwa
wanyama safi, bali wanadamu wenye dhambi kuwa watakatifu. Wale wanaotaka kuwa
watakatifu watajiepusha kula nyama inayotokana na wanyama najisi; lakini wale wasiotaka
utakatifu wataswaga kila kitu (Law. 11:41,43,46,47; Kum. 14:1-4). Mungu hamlazimishi
mtu, kama vile mtengenezaji wa injini ya gari asivyomlazimisha mtu kutumia mafuta
aliyopendekeza. Lakini matokeo mwilini ni ya hakika.
Kisa cha Petro katika Matendo 10:9-16 kimetafsiriwa chini yake katika fungu la 25
hadi 29. Hayo yalikuwa ni maono tu, si kitu halisi; hata hivyo Petro alikataa katakata
kuchinja na kula wanyama najisi ingawa ni Mungu mwenyewe aliyemwamuru kufanya
hivyo mara tatu. Mungu hana kigeugeu; alisema wanyama najisi wasiliwe, basi, hawawezi
kuliwa milele (Mal. 3:6; Zab. 89:34). Watu wanamsingizia bure Petro wanapochinja
wanyama najisi na kula; yeye alikataa katakata. Lakini kuna adhabu kali sana kwa wale
wanaoendelea kula nguruwe, panya, na machukizo yote ya Mataifa (wapagani). Soma
Isaya 65:2-6; 66:15-17).
Pombe haikuwa sehemu ya kinywaji ambacho Mungu alimpa mwanadamu; maji
safi na salama ndicho kinywaji bora kuliko vyote kwa mwanadamu (Mithali 20:1; 23:29-
35). Walevi hawataurithi ufalme wa Mungu (1 Kor. 6:9,10; Gal. 5:21). Kuna wengi
wanaosema, "Mimi nakunywa sana, lakini silewi." Tatizo la pombe sio kulewa tu, bali ni
zile athari zinazotokana na kunywa pombe ambayo ina sumu mbaya ya alkoholi. Sumu
hiyo huathiri vibaya moyo, mishipa ya fahamu, nyama za mwili na kadhalika. Mungu
atamharibu mtu ye yote anayeuharibu mwili wake kwa makusudi kwa njia yo yote ile -----
pombe, tumbako, madawa ya kulevya, na kadhalika (1 Kor. 3:16,17). Pia kuna vinywaji
vinavyopendwa na watu wengi aina ya 'Cola', Kahawa, na Majani ya Chai ambavyo
huidhuru mishipa ya fahamu, ubongo na mwili. Viepukwe.
Asomaye Na Afahamu - 4
Hebu sasa na tuwaangalie wale vijana wanne wa Kiebrania, mateka kutoka
Yerusalemu, wakiwa katika jiji lile la Babeli mwaka ule wa 606 au 605 K.K. Walikuwa na
umri kati ya miaka 18 na 20. Kutokana na hekima yao walichaguliwa kujiunga na vijana
wengine wa Babeli katika Chuo cha Kishenzi [Kipagani] cha Babeli kwa mafunzo ya miaka
mitatu. Wakapewa majina ya miungu ya Babeli ----- Danieli akaitwa Belteshaza, Hanania
akaitwa Shadraka, Mishaeli akaitwa Meshaki, na Azaria akaitwa Abednego (Dan. 1:6,7).
Mfalme akaamuru wale chakula cha mfalme ili wanenepe na kuwa na akili nyingi. Kusudi
lake lilikuwa zuri sana. Lakini, je! chakula kile cha mfalme ambacho kilikuwa na nyama
najisi, kilikolezwa kwa viungo vingi vinavyodhuru mwili, na huenda kilikuwa na vileo
kingeweza kuleta afya bora na akili safi? (Dan. 1:1-5). Vijana hao wanne wa Kiebrania
walikuwa wamelelewa katika mazingira tofauti. Walifuata kanuni za afya na chakula
ambacho Mungu aliwapa wanadamu kula. Walijiepusha na nyama ya aina yo yote ile
pamoja na divai (maji matamu ya zabibu) kwa vile wao walikuwa wanadhiri wa Bwana
(Hesabu 6:1-5). Kwa hiyo agizo hilo la mfalme kwao likawa mtihani mgumu sana.
"Danieli aliazimu moyoni mwake ya kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha mfalme,
wala kwa divai aliyokunywa; basi akamwomba yule mkuu wa matowashi ampe ruhusa
asijitie unajisi" (Dan. 1:8). Ni ujasiri ulioje! Ombi lake halikuwa rahisi kukubaliwa na
msimamizi yule kwa vile angekatwa kichwa kama wangeonekana wamekondeana (Dan.
1:10). Basi Danieli akamwambia, "Tafadhali utujaribu sisi watumishi wako muda wa siku
kumi; na watupe mtama [nafaka, kokwa, mboga za majani, matunda] tule, na maji
tunywe. Kisha nyuso zetu zitazamwe mbele yako, na nyuso za wale vijana wanaokula
chakula cha mfalme..." (Dan. 1:13). Akawakubalia ombi hilo. Je! mambo yalikuwaje
kiafya baada ya siku zile kumi tu? "Nyuso zao zilikuwa nzuri zaidi [wanawake
wanaohangaika na vipodozi vinavyodhuru afya wangezingatia hilo], na miili yao ilikuwa
imenenepa zaidi, kuliko wale vijana wote waliokula chakula cha mfalme. Basi yule
msimamizi akaiondoa posho yao ya chakula [cha mfalme], na ile divai waliyopewa
wanywe, akawapa mtama [nafaka, kokwa, mboga za majani, matunda] tu" (Dan. 1:15,16).
Chakula cha matajiri au wafalme tunachokitamani sana hakileti afya mwilini.
Chakula rahisi cha mimea na maji safi na salama ni lishe bora. Kwa akili safi na mwili
wenye afya, ulionenepa kiafya sio kwa ugonjwa, tumia vyakula vya mimea na maji safi na
salama, na kufuata Kanuni zile 8 za Afya. Wana sayansi wamegundua kuwa wale
wanaokula vyakula vya mimea bila nyama wanaishi maisha marefu sana kuliko wanaokula
nyama. Danieli naye aliishi zaidi ya miaka 80 kufikia kipindi cha utawala wa Koreshi (Dan.
1:21; 10:1). Hebu tuwafuatilie vijana wale wanne mwisho wa mafunzo yao ya miaka
mitatu. Mfalme Nebukadreza aliwaonaje?
"Naye mfalme akazungumza nao; na miongoni mwao wote hawakuonekana
waliokuwa kama Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria... Na katika kila jambo la
hekima na ufahamu alilowauliza mfalme, akawaona kuwa wanafaa mara kumi zaidi
ya waganga na wachawi waliokuwa katika ufalme wake" (Dan.1:19,20).
Kwa nini tuhangaike sana na suala la afya ya mwili wetu, je! maisha ya kiroho si
bora zaidi? "Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako
[kimwili], kama vile roho yako ifanikiwavyo" (3 Yohana 2). Wahenga walisema, "Akili
timamu katika mwili wenye afya." Ni shauri la kuzingatiwa sana. Kanuni ya Biblia ni hii:
"Basi, mlapo, mnywapo, au mtendapo neno lo lote fanyeni yote kwa utukufu wa
Mungu" (1 Kor. 10:31). Tunawajibika kuitunza miili yetu katika hali ya afya nzuri kadiri
iwezekanavyo (l Kor. 6:19,20; 1 Pet. 1:18,19; Rum.12:1,2). Suala la afya linahusu
wokovu wetu. Mungu anaweza kututumia kama Danieli (Dan. 1:17).

No comments: