Monday, June 16, 2014

HIVI MWISHO WA DUNIA UTAKUWAJE?



DANIEL NA SIKU ZETU

                (SOMA DANIELI 12 YOTE)

Yapo mawazo mengi wanayosema watu kuhusu mwisho wa dunia. Wengine wanasema watakatifu watanyakuliwa kwenda mbinguni na waovu wote wataangamizwa; dunia itabaki tupu. Wengine wanasema kanisa peke yake ndilo litanyakuliwa; watu waliobaki wataendelea kuishi duniani, na injili itahubiriwa kwa Wayahudi; ndipo Mpinga Kristo atakuja na kufanya mambo yake. Wengine wanasema mbinguni watakwenda tu wale 144,000, watu wengine wote waliobaki makao yao ni hapa duniani; na ya Kwamba dunia hii haiwezi kuharibiwa. Kwa hiyo wanaangalia majengo mazuri na kusema moyoni "Nitarithi jumba hili". Je! Biblia inatupa picha gani juu ya mwisho wa dunia? Na tunaposema tunaishi siku za mwisho tuna maana gani? Zilianza lini kuhesabiwa? Hebu Danieli atuambie katika Sura hii ya 12.
Mwanzo wa siku za mwisho (Dan. 12:5-7): Tunaona kipindi kile kile cha Danieli 7:25 kinatajwa hapa tena na "mtu yule aliyevikwa nguo za kitani" [Kristo] anayeonekana pia katika Ufu. 10:1-7. Soma pia Mt. 17:1,2; Mk. 9:2,3. Anasema hivi, "Itakuwa wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati; tena watakapokuwa wamekwisha kuvunja nguvu za hao watu watakatifu, ndipo mwisho wa mambo hayo yote yatakapotimizwa" (fungu la 7). Maneno hayo aliyatoa akijibu swali la mmoja aliyemwuliza, "Je! itakuwa muda wa miaka
mingapi hata mwisho wa mambo haya ya ajabu? (fungu la 6). "Mambo ya ajabu" ni mauaji yaliyofanywa na Upapa katika Zama zile za Giza ulipoua zaidi ya watakatifu milioni 50, ambayo yalimshangaza pia hata Yohana (Ufu. 17:6). Kanisa kuua kanisa ni ajabu kuu!
Litakwenda mbingu ya nani? Nyakati 3 1/2 ni miaka 3 1/2 au miezi 42 au siku 1260 za unabii ambazo ni miaka 1260 ya Ufalme wa Papa wa Awamu ya Kwanza (538-1798). Kipindi hicho kimetajwa tena na tena katika unabii (Dan. 7:25; Ufu. 12:6,14; 13:5; 11:2,3; Mt. 24:21,22). Katika Dan. 11:33,34 anasema, "... wataanguka kwa upanga, na kwa moto, na kwa kufungwa, na kwa kutekwa nyara, siku nyingi [538-1798]. Upapa ulitumia upanga, moto, kifungo, kuteka nyara kama unabii unavyosema katika kuwaua watakatifu. Mateso yalikuwa mabaya mno kuliko ya watu wasiomjua Mungu. Ufalme wa Papa ulioitawala dunia (Ulaya Magharibi) ulivunjwa na Wafaransa mapema mwaka 1798. Kuanzia hapo fungu la Dan. 12:4 likaanza kutimia. Maarifa ya kidini, kisayansi na kiteknolojia yaliongezeka kasi kwa namna ya ajabu. Zama za Giza hazikuwa na maendeleo yo yote. Wana-sayansi na Wanadini waliofuata Biblia walikuwa wanauawa. Mwaka 1798 ndio mwanzo wa "Siku za Mwisho". Mwisho wake utakuwa katika Awamu ya Pili inayokuja ya Ufalme wa Papa ----- "tena watakapokuwa wamekwisha kuvunja nguvu za hao watu watakatifu" (Dan. 12:7). Historia inajirudia yenyewe. Mateso na mauaji ya watakatifu yatakuja tena atakapotawala Papa (Ufu. 6:9-11) ----- "wakaambiwa wastarehe bado muda mchache, hata itakapotimia hesabu ya wajoli wao na ndugu zao, watakaouawa vile vile kama wao." Wengi hawaamini maneno hayo; lakini wanapaswa kungoja mpaka yatakapotimia ndipo watakapoamini (Yoh. 14:29).
Kusimamishwa kwa Chukizo la Uharibifu au Mwanzo wa Ufalme wa Papa (Upapa):
Rumi ya Kipagani iliangushwa na makabila ya kipagani ya Ulaya Kaskazini mwaka 476 B.K. Tangu siku za Mfalme Konstantino, mwaka 330, Askofu wa Roma au Papa aliachiwa kutawala mji wa Roma. Kwa hiyo Dola ya Magharibi ya Rumi ilipoanguka, Papa aliendelea kutawala mji ule. Alishika hatamu za utawala juu ya Ulaya Magharibi kuanzia mwaka 538 baada ya kuzing'oa falme tatu - Waheruli (493), Wavandali (534), na Waostrogothi (mapema 538).
Mataifa yale mengine ya Ulaya yalipokea Ukatoliki kwa upanga wa Mfalme Clovis wa Ufaransa. Kwa hiyo, yakajikuta yako tena chini ya Papa, (538-1798). Clovis alifanikiwa kuyafanya Wakatoliki mwaka 508 (Dan. 12:11,12). Kuanzia mwaka huo wa 508 zinahesabiwa siku au miaka 1290 na 1335. Chukizo la Uharibifu lilisimamishwa [lilitawala] kuanzia 538 - 1798 (yaani, miaka 508 + 1290 = 1798 barabara). Mwaka ule wa 1798 ukawa ndio mwanzo wa siku za mwisho. Hukumu ikawekwa mbinguni kumpimia adhabu yake mwaka 1844, yaani, mwisho wa miaka ile 2300 ya Dan. 8:14 (yaani, miaka 508 + 1335 = 1843-1844). Mwaka ukianza tarehe 2 Januari unamalizika katika mwaka unaofuata.
Kuna heri gani kwa watu watakaoufikia mwaka 1844, mwaka ambao Hukumu ilianza mbinguni? Wale walio na hekima "watajitakasa na kujifanya weupe" (Dan. 12:3,9,10); tena watasimama kama Danieli katika "kura" yao, yaani, majina yao yatabaki katika Kitabu cha Uzima mbinguni pamoja na watakatifu wote waliotangulia (Dan. 12:13). Isitoshe heri nyingine ni ile ya kufufuliwa katika ufufuo wa pekee (Dan. 12:2; Ufu. 14:13) kwa wale wote walioshiriki kuihubiri Injili ya Milele kwa uaminifu (Ufu. 14:6-12). Injili hiyo inayoitwa "Ujumbe wa Malaika Watatu" ilianza kuhubiriwa 1840-1844 na bado inahubiriwa. Ufufuo wa watakatifu wote utafuata mara tu baada ya ufufuo huo wa mseto utakaokuwa na wale waliomchoma pamoja na wale waliowatesa sana watu wa Mungu (Ufu. 1:7; 1 The. 4:16,17[18]).

MWISHO WA DUNIA UTAKUWAJE?
 Tumeona jinsi Ufalme wa Papa ulivyotawala katika Awamu ya Kwanza (538-1798) na ya kwamba unakwenda kutawala dunia tena. Hiyo itakuwa ni awamu yake ya pili na ya mwisho. Maangamizi ndiyo yatakayokuwa mwisho wa Ufalme huo. Mfuatano wa matukio ni huu ----- Papa atawala awamu ya pili, mateso na mauaji ya watakatifu yaanza tena kwa kipindi kifupi sana, Kristo, Kuhani wetu Mkuu, anamaliza kazi yake ya Maombezi katika Hekalu la Mbinguni na kuufunga mlango wa kutubu au wa rehema kwa tamko la Ufu. 22:11. Watu wa Mungu wametiwa muhuri wa Mungu katika vipaji vya nyuso zao; na watu wa Mnyama wamepata alama ya mnyama vipajini mwao na katika mikono yao. Wakati wa taabu unaanza (Dan. 12:1) Mikaeli (Kristo) anapotawazwa (anaposimama) katika Jiji la Yerusalemu juu; pepo za vita zilizozuiwa zaachiliwa na vita inatapakaa kila mahali ikileta maafa mengi(Ufu. 7:1-4), vimbunga na maafa mengine yanatokea, ndipo silaha ya Mungu ya kutisha sana kwa wale walioikanyaga Sabato yake itakapotumika (Mapigo 7 ya Ufunuo 16). Wale wote watakaomfuata Papa majina yao yataondolewa katika kitabu cha uzima (Kut. 32:32,33; Ufu. 13:8). Mtihani wa siku za mwisho ni Amri ya Nne [Sabato](Ufu. 3:10; 14:9,10).
Mchezo wa kuiweka Jumapili badala ya Sabato [Jumamosi] utakuwa na athari mbaya mno kwa dunia nzima (Isa. 24:1-6,19,20; Ufu. 19:11-21). Ole kwa wafalme wa dunia hii! Ole kwa kila mtu asiyesimama upande wa Yesu Kristo katika Pambano hili Kuu! Karibu sana litafikia mwisho wake. Watoto wa Mungu wamechoka na dunia hii wanataka kwenda kupumzika mbinguni kwa miaka 1000, na Yesu anasema. " Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo" (Ufu. 22:11). Je! u tayari kumlaki Bwana? Je! utasimama imara hata kama mbingu zikianguka, na kuiinua juu Bendera ya Imanueli [Kristo] iliyoandikwa "Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao Amri [Kumi] za Mungu, na Imani ya Yesu" (Ufu. 14:12). Hivi karibuni dunia hii itabaki tupu, ndugu yangu. Kuanzia leo chagua kuingia Paradiso pamoja na Kristo (Luka 23:42,43; 2 Kor. 6:2). Huenda usisikie mwito mwingine kama huu. Amua leo!


No comments: