Sunday, September 7, 2014

UJUMBE WA MALAIKA WA KWANZA

Ujumbe wa malaika wa kwanza ni wito wa kumwabudu Mungu Muumbaji. Kwa kweli, lugha yenyewe inatukumbusha sisi juu ya maneno yale yaliyotumika katika amri ya nne. Malaika wa kwanza asema hivi: “Mcheni Mungu, na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja. Msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji” (Ufunuo 14:7). Vilevile, amri ya nne yatuambia sisi kumwabudu Mungu kwa sababu yeye ni Muumbaji wa vitu vyote mbinguni, duniani, na baharini. Yatuambia kwamba siku ya pekee ambayo Mungu ameitenga kwa ajili ya ibada ni siku ya saba ya juma - siku ya Sabato yake takatifu (angalia Kutoka 20:8-11).

UJUMBE WA MALAIKA WA PILI

Ujumbe wa malaika wa pili ni huu: “Umeanguka, umeanguka Babeli, mji ule ulio mkubwa, maana ndio uliowanywesha mataifa yote mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake” (Ufunuo 14:8). Babeli lilikuwa ni taifa katika Agano la Kale ambalo liliishambulia Israeli, yaani, watu wa Mungu, na kuwachukua mateka. Babeli lilikuwa ni taifa lililojaribu kuifutilia mbali ibada ya Mungu wa kweli wa mbinguni na mahali pake kuweka miungu ya kipagani. Na hivyo Babeli ikawa ishara iliyowakilisha majeshi yote yatakayowapinga watu wa Mungu katika siku za mwisho. Kwa hiyo malaika huyu wa pili anasema kwamba Babeli umeanguka kwa sababu umeyafanya mataifa yote ya dunia kunywa mvinyo ya uasherati wake, yaani, hiyo ni njia ya kusema kwamba majeshi yanayopigana na Mungu katika siku hizi za mwisho yatajaribu kumlazimisha kila mmoja kutoa utii wake kwa majeshi hayo kuliko kwa Mungu. Imewakilishwa kama “uasherati,” au uzinzi. Kutokumtii Mungu kunaonyeshwa katika Biblia kama uzinzi wa kiroho, jambo hili lote linatufikisha kwenye hoja ya utii.
 

UJUMBE WA MALAIKA WA TATU

Malaika wa tatu anatangaza hivi: “Mtu awaye yote akimsujudu huyo mnyama na sanamu yake, na kuipokea chapa katika kipaji cha uso wake, au katika mkono wake, yeye naye atakunywa katika mvinyo ya ghadhabu ya Mungu iliyotengenezwa, pasipo kuchanganywa na maji, katika kikombe cha hasira yake; naye atateswa kwa moto na kiberiti mbele ya malaika watakatifu, na mbele za Mwana-Kondoo” (Ufunuo 14:9,10). Maneno haya machache ni onyo muhimu kabisa ambalo Mungu amepata kulitoa katika Biblia. Anatuonya sisi dhidi ya kuisujudu mamlaka hii ambayo inapingana naye, naye anatuonya sisi tusipokee chapa yake. Mamlaka hii ni nani au ni kitu gani na alama yake ni alama gani?
Je umewahi kumuomba MUNGU akufunulie ili uweze kuepukana na mapigo 7?
Tafakari.